Nimebeba mimba mbili zote nimezaa pacha (watoto wawili), naogopa kubeba mimba tena ingawa ninahitaji kuongeza mtoto lakini mmoja, sitaki tena pacha.
Nikifikiria msoto niliopitia kuwalea waliotangulia sitaki tena lakini sitaki kuishia hapo ingawa nataka kulea kama wenzangu mtoto mmoja kwa kujidai. Hawa wanne ni kama niliwalea kwa kupania maana bila kupambana mlima ni mrefu mno kuupanda.
Hongera sana kwa kubarikiwa baraka ya kupata watoto wawili wawili. Kuhusu kuogopa kupata pacha tena nakuelewa au unaeleweka kabisa kwani shughuli ya kuwalea si ya kitoto.
Pia huwa ni changamoto kubwa kihisia, kisaikolojia, na kimaisha. Ingawa hujasema changamoto zaidi ilikuwa kwenye nini.
Wengine hutetereka kwenye kipato kwani malezi yao huwa na gharama kubwa pia, kama ni malezi ya kawaida inajulikana ukizaa pacha lazima uzifunge zikaze.
Siku nyingine elezea kidogo namna ulivyofanikiwa kuwalea pacha wako ili kuwatia moyo wanaotaka au wanaotarajia kuwapata.
Tukirudi kwenye swali lako la msingi, ni kawaida kuhisi hofu au wasiwasi kuhusu kubeba tena mimba, hasa unapojua changamoto zinazohusiana na kuzaa pacha, lakini pia unahisi haja ya kuongeza familia.
Hii ni hali inayogusa moyo na akili kwa wakati mmoja, na ni muhimu kuikabili kwa hekima na utulivu huku ukimtanguliza Mungu mbele maana ndiyo kila kitu katika safari hii. Kama nilivyoanza kwa kukupongeza kupata watoto pacha ni baraka kamwe usichukulie kama mkosi, kuna wanaotoa fedha nyingi kuwapata.
Hata hivyo nakubaliana nawe kuwa kuzaa pacha kunaweza kuleta mzigo mkubwa wa mwili na akili, na kuhitaji muda mrefu wa urejeshaji, hali ambayo mara nyingi huacha alama za hofu kwa mimba inayofuata.
Ni muhimu kwanza kutambua kuwa hisia hizi si za ajabu wala hatarishi; ni sehemu ya kujilinda kiakili na kipaumbele cha familia.
Kwa mama ambaye tayari amebeba pacha, kugundua kuwa kuna uwezekano wa kuzalisha pacha tena inaweza kuwa chanzo kikubwa cha wasiwasi, lakini hofu hii isikuzuie kufanikisha azma yako ya kuongeza mtoto.
Kuna njia za kiasili na za matibabu ambazo zinaweza kupunguza uwezekano wa pacha. Ushauri wa matibabu kutoka kwa daktari wa wanawake ni muhimu ili kupanga ovulation au kutumia mbinu zinazodhibiti idadi ya mayai yanayoongezeka.
Mbinu hizi ni salama na zinaweza kuhakikisha kuwa mimba inayofuata itakuwa ya mtoto mmoja, kama inavyotakiwa.
Pia usisite kuonana na wataalamu wa saikolojia au wanasaikolojia wa uzazi wanaweza kusaidia katika mazungumzo ya kina, kutoa mbinu za kupunguza hofu, na kusaidia kukubali hali halisi.
Ukikutana na wataalamu hawa utakuwa huna wasiwasi, huku ukiendelea kufuatilia taratibu za kupata mtoto mmoja na ikitokea ukapata pacha kulingana na asili yako, hutakuwa na wasiwasi tena kwa sababu utakuwa umejengwa vema kisaikolojia kulipokea hilo.
Binafsi naamini ukipata mtoto au watoto hii hofu yote itaondoka kwani akili itahamia kwenye malezi ikichanganyika na furaha ya kuongeza familia.
Kama uliweza mwanzo bila kujali ulipitia njia zipi, wakija wengine au mwingine utaweza pia.
Nina imani ukifuata mbinu hizi utakuwa sawa na utaendelea na mpango wa kuongea familia bila hofu. Nakutakia mafanikio katika hatua hii ya kuongeza familia.
