TCAA inavyoimarisha usafiri wa anga

Dar es Salaam. Mamlaka ya Usafiri wa Anga Tanzania (TCAA), imesema imepiga hatua kubwa katika kuimarisha usalama na udhibiti wa shughuli za usafiri wa anga nchini kwa mwaka wa fedha 2024/2025, hatua inayochangia kuongezeka kwa uaminifu wa huduma za anga kwa waendeshaji, abiria na wadau wa kimataifa.

Akizungumza hayo wakati wa Mkutano wa 18 wa Mapitio ya Sekta ya Uchukuzi uliofanyika katika Kituo cha Mikutano cha Kimataifa cha Arusha (AICC), jana Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, Salim Msangi, amesema Mamlaka imejikita katika kuboresha kanuni na mifumo ya usafiri wa anga.

Lakini pia amesema imejidhatiti kuimarisha viwango vya uendeshaji wa viwanja vya ndege na ndege, pamoja na kupanua wigo wa ukaguzi ili kuhakikisha huduma za anga zinakuwa salama, bora na za kuaminika kote nchini.

Msangi amesema TCAA imeongeza pia ufuatiliaji wa masuala ya usalama katika viwanja vya ndege na kwa waendeshaji wa shughuli za anga sambamba na kushughulikia hatari za kiusalama vikiwamo vizuizi vinavyozunguka viwanja vya ndege.

“Pia tumeimarisha uzingatiaji wa sheria kupitia ukaguzi wa mara kwa mara na ushirikishwaji wa wadau,” amesema Msangi.

Kwa mujibu wake, hatua hizo zimechangia kuboresha ufanisi wa uendeshaji, kuongeza ubora wa huduma na kuimarisha imani ya wadau wa ndani na nje ya nchi katika mfumo wa usafiri wa anga wa Tanzania.

Kwa miaka mingi, sekta ya usafiri wa anga imehitaji wataalamu wenye ujuzi wa hali ya juu ili kuhakikisha usalama wa safari, utoaji wa huduma bora na ukuaji endelevu wa uchumi. Kupitia TCAA, Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuwezesha Watanzania kupata ujuzi huo na kunufaika moja kwa moja na fursa zinazotokana na sekta hiyo.

Kama mdhibiti wa sekta ya usafiri wa anga, TCAA inasimamia Mfuko wa Mafunzo ya Marubani unaolenga kuwawezesha Watanzania kupata mafunzo ya urubani katika vyuo vya anga vilivyoidhinishwa nje ya nchi kwa kushirikiana na mashirika ya ndege.

Mpango huo unalenga kukabiliana na changamoto ya gharama kubwa za mafunzo ya urubani na kuhakikisha nchi inakuwa na marubani wazawa wenye sifa na viwango vya kimataifa.

Sambamba na hilo, TCAA inaendesha Chuo cha Usafiri wa Anga (CATC) kinachotoa mafunzo ya kitaalamu yanayohitajika moja kwa moja katika uendeshaji wa shughuli za anga.

Miongoni mwa wanufaika wa mafunzo hayo ni Pendo Charles, mhitimu wa kozi ya Ofisa Muongozaji Ndege ambaye kwa sasa anafanya kazi Kituo cha kuongozea ndege cha TCAA Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere.

Pendo anasema mafunzo aliyopata kupitia CATC yalimuwezesha kupata ajira na kushiriki moja kwa moja katika kuhakikisha usalama wa safari za ndege, hatua iliyobadilisha maisha yake.

Kwa mujibu wa Mkurugenzi Mkuu wa TCAA, katika mwaka wa 2024/2025 pekee, Chuo cha Usafiri wa Anga kiliendesha jumla ya kozi 131 zilizohusisha washiriki 1,967, wakiwemo Watanzania 1,799 na wageni 168 kutoka nje ya nchi. Wataalamu hao sasa wanahudumia viwanja vya ndege mbalimbali nchini, wakihakikisha ndege zinaongozwa kwa usalama, taarifa sahihi za anga zinapatikana na teknolojia mpya, ikiwemo matumizi ya drone, zinaendeshwa kwa kufuata sheria na taratibu.

Amesema kwa wananchi wa kawaida, matokeo ya uwekezaji huo yanaonekana kupitia safari salama zaidi, huduma za anga zinazotegemewa na sekta ya usafiri wa anga inayoendelea kukua na kutoa ajira.

Hatua hiyo amesema inaonesha dhamira ya Serikali kupitia TCAA kuwekeza katika watu na maarifa ili kuhakikisha sekta ya anga inaendelea kuimarika na kuwahudumia Watanzania kwa ufanisi na usalama.