WANAMICHEZO WAHAMASISHWA KUWA MABALOZI WA NISHATI SAFI YA KUPIKIA


Wanamichezo nchini wamehamasishwa kuwa mabalozi wa nishati safi ya kupikia ili kufikia lengo la Serikali la mwaka 2034 asilimia 80 ya Watanzania wawe wanatumia nishati safi ya kupikia.

Wito huo umetolewa na Bi. Jaina Msuya, mwakilishi wa Mkurugenzi Mkuu wa REA, Mhandisi Hassan Saidy wakati wa hafla ya utoaji wa tuzo kwa wadau, wachezaji, waamuzi na klabu za mchezo wa wavu zilizofanyika jana Jijini Dodoma.

“Katika kutekeleza Mkakati wa Taifa wa Matumizi ya Nishati Safi ya Kupikia, sisi kama REA tunaendelea kufanya jitihada mbalimbali ikiwamo usambazaji wa mitungi ya gesi ya kupikia,majiko banifu kwa bei ya ruzuku pamoja kuziwezesha taasisi zinazolisha watu zaidi ya 100 kutumia mifumo ya nishati safi ya kupikia ili kuhakikisha lengo hilo linafikiwa.

REA inatekeleza Mkakati wa Taifa wa Nishati ya Kupikia kwa kushirikiana na wadau mbalimbali ikiwa ni pamoja na jamii ambayo inajumuisha wanamichezo.

“Matumizi ya nishati safi ya kupikia yana faida nyingi ikiwa ni pamoja na kutunza mazingira na kulinda afya. Wanamichezo ni sehemu ya jamii ya Watanzania hivyo natoa wito tushirikiane na Serikali kuhamasisha jamii yetu itumie nishati safi ya kupikia na tunaomba mkawe mabalozi wetu” amesema Bi Jaina.

Aidha, alisema kuwa utekelezaji wa miradi ya nishati safi ya kupikia una fursa nyingi katika mnyororo wa thamani wa usambazaji ambazo wanamichezo na vijana wanaweza kuzitumia kujiajiri ikiwa ni pamoja na kuwa mawakala wa kusambaza bidhaa hizo vijijini.

REA ni mmoja wa wadhamini wa mashindano ya Mpira wa Wavu Kitaifa kwa mwaka 2025 ambayo yamefanyika Jijini Dodoma na kuhitimishwa Desemba, 19, 2025.