Canada. Kuna swali huwa linatushughulisha kama wazazi na wanandoa. Je, inakuwaje baadhi ya wanandoa hufanikisha mambo yanayowashinda wengi katika maisha ya ndoa? Tutaanza na mfano wa Malkia wa Uingereza marehemu Elizabeth (21 Aprili 1926 – 8 Septemba 2022).
Pamoja na matatizo ya hapa na pale, malkia alibainisha kuwa inawezekana kufanikiwa kimaisha na katika ndoa jambo ambalo huwashinda wengi na kusababisha wawe na ndoa zenye changamoto na mazonge kutokana mafanikio yao.
Je, inakuaje kukawa na watu waliofanikiwa kitaaluma, kiuchumi na mengine lakini wakashindwa katika ndoa? Utamuona mtu ni tajiri lakini maskini wa ndoa. Mwingine ni msomi wa kupigiwa mfano lakini asiye na ndoa.
Kuna wenye utajiri wa kuitwa utajiri lakini hawamo katika ndoa au ndoa zao zimevunjika. Jikumbushe watu waliofanikiwa kama vile Mfalme Charles wa Uingereza, Bill Gates, Donald Trump, Jeff Bizos na wengine ambao ndoa ziliwashinda.
Walinganishe na watu wa daraja lao kama vile Warren Buffet na wengine ambao ni matajiri wenye ndoa za kupigiwa mfano. Je, kuna siri gani katika kushinda na au kumudu taasisi tata lakini nyeti ya ndoa?
Maana, utakuta mtu maskini au asiye msomi ana ndoa imara kuliko ya tajiri ilhali wasomi na matajiri zinawashinda. Nenda mbele zaidi. Utakuta mama mrembo asiye na ndoa ilhali yule asiye mrembo anayo tena imara. Inakuwaje matajiri, wasomi, na warembo japo si wote wasiolewe lakini maskini, wasiosoma, na wasio warembo wakaolewa na kuishi kwenye ndoa imaara? Hapa kuna fumbo vile vile somo.
Jiulize kinamama tena matajiri au wasomi aka mishangazi japo hatupendi kushabikia neno hili, wangapi wanaishi bila ndoa tena wengine wakitamani au kutangaza kutaka kuolewa wasiolewe?
Wakati huo huo, unaweza kumkuta muuza baa akiwa kaolewa na anafaidi ndoa! Hivi hapa ndipo msemo wa kuolewa ni majaliwa una maana zaidi? Je, nini kifanyike? Je, wazazi waache kuwasomesha mabinti zao ili waolewe au tubadili mtazamo juu ya wenzetu hawa?
Japo hili haliongelewi, kuna haja ya kuangalia mifumo yetu ya elimu inayowaandaa hawa waathirika. Mfano, siku za hivi karibuni kumekuwapo na madai ya visa vingi vya rushwa ya ngono kwenye baadhi ya vyuo.
Hapa, tukiwa wakweli, waathirika ni kinamama. Kwanini tusibadili mfumo wetu? Mfano, hapa Canada, si rahisi mwalimu kumtaka wala mwanafunzi kutoa rushwa ya ngono.
Hii ni kwa sababu, hapa, tunao mfumo wa kutathminiana baina ya walimu na wanafunzi. Mwalimu anawatathmini wanafunzi ambao pia humtathmini. Pia, ikigundulika kuwapo kwa uchafu huu, mwalimu ataumia na kujutia maisha yake yote.
Mbali na rushwa, kuna tabia binafsi za wahusika hasa wale wasiopenda kuhenyekea maisha yao hadi wakashindwa kuona mbali kiasi cha kugeuza miili yao maduka ya kupatia baadhi ya huduma na mapato kirahisi wasijue madhara yake hapo baadaye.
Hata hivyo, tunaonya na kusisitiza, si wasomi wote ni wa hivyo japo wapo wengi wa hivyo. Kwa wale wanaoshangaa kukuta msomi kaoa mama asiye msomi, hapa wanaweza kupata jibu.
Tukiachana na tatizo la mifumo ya ovyo na kirushwa, tuangalie jamii kwa kujiuliza maswali haya. Je, hapa, tatizo ni wahusika pekee yao au jamii? Nini suluhu ya kadhia hii? Tutajaribu kujibu maswali haya chokonozi na tekenyeshi kifikra.
Kwa mujibu wa American Boys and Men (2025), ni asilimia 50 tu ya wanawake wasomi wanaoolewa tena na wasomi wenzao. Nusu ya idadi iliyobaki, huolewa na watu wasio wasomi. Waliobaki wanabakia bila ndoa. Je, kama jamii, tumejiandaaje kukabili janga hili?
Mwisho, kwa nchi zinazofanya utafiti kama Marekani, tatizo tunaloongelea linaeleweka ukubwa wake. Je, kwa nchi zisizofanya utafiti, tatizo ni kubwa kiasi gani?
Kama jamii na taifa, kuna haja ya kuyadurusu masuala kama haya ili kuwa na ndoa bora na kupata taifa bora hasa ikizingatiwa kuwa ndoa ndizo huzaa wananchi ambao hutegeneza taifa.
Kuna wakati tunadhani kuwa somo la ndoa linapaswa kufundishwa shuleni kuanzia darasa la sita na kuendelea juu. Inawezekana kufanikiwa katika ndoa na mambo mengine, lakini tufanyeje?
