Moshi. Zaidi ya wapagazi 30,000 kutoka vyama vinne nchini wameungana na kuunda umoja wao uitwao Tanzania Association of Porters (TAP), kwa lengo la kuimarisha mshikamano miongoni mwao na kuweka mfumo wa pamoja wa kushughulikia changamoto mbalimbali zinazowakabili katika sekta ya utalii.
Vyama vilivyoungana kuunda TAP ni Tanzania Porters Organization (TPO), Mount Kilimanjaro Porters Society (MKPS), Mount Meru Porters Association (MMPA) na Ngurudoto Crater Porters Association (NCPA).
Akizungumza wakati wa uzinduzi wa TAP uliofanyika katika Ukumbi wa Uhuru Hotel, mkoani Kilimanjaro, Mwenyekiti wa TAP, Mohamed Mkoma, amesema kuanzishwa kwa muunganiko huo kumetokana na changamoto za muda mrefu zilizokuwa zikiwakabili wapagazi kwa kukosekana kwa sauti ya pamoja ya kuwasilisha hoja na malalamiko yao Serikalini.
“Tulikuwa tunapeleka taarifa tofauti Serikalini na hali hiyo ilisababisha mambo yetu mengi kukwama. Tumeamua kuungana ili tuwe na sauti moja itakayomsemea mpagazi kwa niaba ya wote,” amesema Mkoma.
Ameeleza kuwa moja ya changamoto kubwa iliyowakabili wapagazi kwa muda mrefu ni kukosa mfumo rasmi wa malipo, hali iliyosababisha mishahara kuchelewa na kukosa uhakika wa kipato.
“Tunashukuru kuanzia Agosti mwaka huu tumetambulika rasmi katika mfumo wa malipo ya Serikali. Hii ni hatua kubwa na ya kihistoria kwa wapagazi,” ameongeza.
Akizungumza kwa niaba ya Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Ashantu Kijaji, Mkurugenzi Msaidizi wa Utalii, Richie Wandwi, amesema sekta ya utalii haiwezi kukua bila ushirikiano wa karibu kati ya Serikali na sekta binafsi.
“Utalii unategemea uhifadhi wa maliasili na urithi wa Taifa. Vivutio vinavyowaleta watalii vinahitaji mchango wa kila mmoja wetu kuvihifadhi,” amesema Wandwi.
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Waendesha Utalii Tanzania (Tato), Wilbard Chambulo, amewataka wapagazi kufanya kazi kwa nidhamu, uadilifu na weledi ili kulinda taswira ya Taifa na sekta ya utalii kwa ujumla.
Amesema wapagazi ni mabalozi muhimu wa Taifa, kwa kuwa wao ndio walio karibu zaidi na watalii katika safari zao hivyo wanapaswa kuwa na nidhamu na kulinda taswira ya nchi.
“Wapagazi wanambeba mgeni na kwa maana hiyo wanabeba pia bendera ya Taifa. Nidhamu yao ni taswira ya nchi. Ni muhimu waipende kazi yao, wawe waaminifu na waepuke vitendo vinavyoharibu sifa ya sekta kama kudokoa mali za wageni,” amesema Chambulo.
Ameongeza kuwa, kuanzishwa kwa TAP kutawawezesha wapagazi kuwasilisha changamoto zao kwa umoja na nguvu zaidi, tofauti na hapo awali ambapo kila mmoja alikuwa akizungumza kivyake.
Mbunge wa Moshi Mjini, Ibrahim Shayo, amesema wapagazi ni nguzo muhimu katika sekta ya utalii na wanachangia kwa kiasi kikubwa mapato ya Taifa, huku akiahidi kutumia nafasi yake kuwasimamia na kuwatetea.
“Nitakuwa sauti yenu. Nitashirikiana na kampuni za utalii kuhakikisha mnathaminiwa na mnapata haki zenu. Niwaombe muendelee kuwa wavumilivu na kushughulikia changamoto zenu kupitia vikao na mazungumzo,” amesema.
Kwa upande wake, mpagazi Janeth Charles amesema kuanzishwa kwa TAP kutaimarisha uwajibikaji na kulinda haki za wapagazi, ikiwemo kuhakikisha wanapata mishahara yao kwa wakati.
“Zamani mshahara ulikuwa unachelewa sana. Sasa tunaamini tutalipwa kwa wakati na pia tuna mahali pa kukimbilia pale haki zetu zinapokiukwa,” amesema.
