Dar es Salaam. Majanga ya moto yameendelea kuwa mzigo kwa wafanyabiashara nchini mwaka 2025, kutokana na kuongezeka kwa matukio katika maeneo mbalimbali ya biashara, hususan katika majengo ya biashara ya Kariakoo, jijini Dar es Salaam na maeneo mengine mikoani.
Eneo la Kariakoo, linalotambulika kama kitovu cha biashara, kwa mwaka huu limekumbwa na matukio mengi ya moto yaliyoathiri mali na shughuli za kiuchumi kwa wafanyabiashara.
Mbali na matukio yaliyotokea kabla ya Desemba, tukiwa ukingoni mwa mwaka, wiki iliyopita, Desemba 19, baadhi ya wafanyabiashara wa Kariakoo walijikuta katika wakati mgumu baada ya moto mkubwa kuteketeza maduka kadhaa katika mitaa ya Magila na Likoma.
Askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji Mkoa wa Kilimanjaro wakati wanazima moto katika vyumba viwili vya biashara katika Mtaa wa Dar es Salaam uliopo Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro Oktoba 11, 2025.
Tukio hilo lilizua taharuki na kurejesha kumbukumbu za majanga ya moto yaliyotokea siku za nyuma.
Ajali hiyo iliongeza idadi ya ajali za moto zilizoripotiwa upande wa Kariakoo kwa mwaka 2025, ikiwa ni pamoja na ile iliyotokea Novemba 16, ambapo duka moja liliteketea kwa moto katika Mtaa wa Uhuru.
Kwa mujibu wa taarifa za awali, ajali nyingi za moto zilizotokea Kariakoo zinadaiwa kusababishwa na hitilafu ya umeme.
Hali hiyo imeendelea kuzua maswali kuhusu usalama wa mifumo ya umeme inayotumika katika majengo mengi ya biashara, huku wito ukitolewa kwa mamlaka husika kuchukua hatua za haraka kudhibiti tatizo hilo.
Mfululizo wa matukio hayo umeacha athari kubwa za hasara, huzuni na sintofahamu kwa wafanyabiashara na wananchi wanaotegemea Kariakoo na maeneo mengine yaliyoathirika kwa shughuli zao za kila siku, huku mustakabali wa biashara zao ukiendelea kuwa kitendawili.
Muonekano wa maduka yaliyoteketea moto katika eneo la Salmini, Kata ya Chemchem, Manispaa ya Tabora.
Akizungumza na Mwananchi Ijumaa, Desemba 16, 2025, jijini Dar es Salaam, Mkaguzi Msaidizi wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Mkoa wa Ilala, Mohamed Mlangwa, alisema kwa taarifa za awali ajali nyingi za moto chanzo chake ni hitilafu ya umeme, hivyo wanaendelea kuchunguza na taarifa zitatolewa baada ya uchunguzi kukamilika.
Pia, ujenzi holela, msongamano wa watu na biashara, mifumo ya umeme chakavu, matumizi ya majengo yasiyo rasmi na uhaba wa vifaa vya dharura vimeendelea kuitengeneza kama bomu linalosubiri kulipuka.
Kila moto unaowaka unawaacha wafanyabiashara wakihesabu upya mwanzo wa maisha yao wakiwa hawajamaliza kulipa mikopo ya mizigo iliyoteketea.
Mbali na hasara ya mali, matukio haya yameongeza presha ya kisaikolojia kwa wafanyabiashara waliowahi kuunguliwa, huku wengine wakisema hulala usingizi wa manga’amung’amu wakihofia kupigiwa simu usiku kuwa duka limewaka moto.
Moto katika biashara za maduka
Katika mitaa ya Msimbazi, Narung’ombe, Mchikichi, Uhuru na sehemu nyingine za Kariakoo, majengo kadhaa yaliungua kwenye matukio tofauti, yakiteketeza maduka ya viatu, manukato na stoo za bidhaa za thamani kubwa.
Agosti 31, moto uliteketeza chumba kimoja cha duka kati ya 100 katika jengo la Mtaa wa Aggrey na Sikukuu.
Septemba 22, stoo ya viatu katika jengo la ghorofa nane iliungua na kusababisha ghorofa tatu (tano, sita na saba) kuathirika, huku hasara ikifikia mamilioni ya shilingi.
Oktoba 4, moto mwingine ulitokea Mtaa wa Msimbazi, siku 13 tu baada ya stoo ya mizigo kuungua Narung’ombe.
Novemba 16, duka lingine liliungua katika Mtaa wa Uhuru, chanzo chake hakikujulikana na uchunguzi unaendelea.
Mbali na jiji la Dar es Salaam, Januari 21, katika jiji la Dodoma, maduka 14 yaliteketea katika eneo la biashara, wafanyabiashara wakilia kukosa msaada wa haraka kutokana na barabara nyembamba zilizozuia magari ya zimamoto kufika kwa wakati.
Handeni, Tanga, Januari 8, maduka mawili ya vyombo na kutengenezea mikate yaliteketea kwa moto unaodhaniwa kusababishwa na hitilafu ya umeme.
Katika Wilaya ya Kahama, mkoani Shinyanga, Oktoba 25, moto uliteketeza vyumba sita vya biashara, huku mkuu wa mkoa huo, Mboni Mhita, akisema wafanyabiashara wanatakiwa kufanya ukaguzi wa mara kwa mara na kuacha kujiunganishia umeme kienyeji.
Watengeneza samani nao yaguswa
Watengeneza samani ni miongoni mwa walioathirika kwa moto mwaka huu, kwani Aprili 21, karakana na vibanda 16 vya samani viliteketea mkoani Morogoro.
Baadhi ya maduka yaliyoungua na Moto Barabara ya Nane katika Mtaa wa Mwanagaza jijini Dodoma.
Machi 17, moto pia uliteketeza soko la mbao Sabasaba jijini Mwanza na kuwaathiri wafanyabiashara 30 kati ya 1,000.
Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, aliwataka wafanyabiashara kuzingatia matumizi ya vifaa vya kuzimia moto na kukata bima ya moto, huku akisisitiza kuwa si majanga yote Serikali huwajibika kugharamia hasara.
Novemba 25, ghala la mbao na maduka ya samani eneo la Keko, Dar es Salaam, yaliungua, huku Desemba 5, kukishuhudiwa kiwanda cha samani Boko Msikitini kikiteketea usiku, mashuhuda wakisema ni tukio la pili kutokea katika eneo hilo.
Julai 12, soko la Mashine Tatu mkoni Iringa, moto ulioteketeza vibanda 429 vya ndani na 86 vya nje ya soko hilo.
Agosti 15, soko la Kawe, jijini Dar es Salaam liliungua, Serikali ikitangaza mpango wa dharura na wa muda mrefu kuwasaidia wafanyabiashara, ikiwemo kutoa Sh100 milioni na kuwahamisha kwa muda.
Siyo biashara pekee zilizoathirika
Julai 20, jengo la Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) mkoani Lindi liliwaka moto ulioanzia katika chumba cha kuhifadhia nyaraka.
Januari 30, jengo lenye ofisi za Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), mkoa wa Kikodi, Kariakoo, nalo liliungua kwa moto katika ghorofa moja, hali iliyolazimu ofisi kuhamishwa kwa muda.
Mkandarasi, Almas Ally, amesema baadhi ya wamiliki wa majengo hulazimisha kupunguza gharama za ujenzi kwa kupuuza viwango vya usalama, hali inayosababisha majengo kukosa mifumo sahihi ya umeme.
Zaidi ya maduka 17 pamoja na stoo za kuhifadhia bidhaa zilivyoteketea kwa moto usiku wa Juni 10, 2025 katika eneo la Buseresere, Wilaya ya Chato mkoani Geita.
“Wamiliki wamekuwa wakialalamika kutokuwa na fedha kwa sababu wametumia kwenye manunuzi ya vitu vingine, hivyo hulazimisha ubanaji wa bajeti kwa wakandarasi,” amesema Ally.
Mhandisi wa umeme, Josephina Mutashobya, amesema matumizi ya nyaya duni na kuunganisha umeme bila kuzingatia ‘data sheet’ ni chanzo kikubwa cha moto, akisisitiza umuhimu wa kuajiri mafundi na wahandisi wenye usajili.
“Wajenzi wa nyumba za biashara, masoko na maghorofa wanatakiwa kuajiri fundi mwenye usajili au anayesimamiwa na mhandisi mwenye taaluma ili kuepuka ajali ambazo zinaweza kuzuilika kama moto,” amesema Josephine.
Kamishna Msaidizi wa Zimamoto Mkoa wa Dar es Salaam, Peter Mabusi, amesema matukio mengi ya moto Kariakoo yanasababishwa na kujiunganishia umeme kiholela, matumizi ya majengo bila ukaguzi na kubadili matumizi ya majengo bila kuboresha mifumo ya umeme.
Amesema uchunguzi wa kina unaendelea, huku akiwataka wamiliki wa majengo na wafanyabiashara kuhakikisha mifumo ya umeme ni salama ili kuzuia majanga yanayoendelea kuharibu maisha na uchumi wa wananchi.
“Tunachunguza ghorofa zote zilizoathirika tukishirikiana na vyombo vya usalama na mamlaka nyingine, lengo letu ni kuhakikisha hatari kama hizi zinapunguzwa na usalama wa kila mtu unadumishwa,” amesema Mabusi.
