Dar es Salaam. Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Benson Bagonza amesema kuna uhitaji mkubwa wa maridhiano ya kweli ili kuliunganisha Taifa na kurejesha mshikamano huku akibainisha mambo matano aliyoyataja kuwa ni ‘sumu’ inayopaswa kuepukwa katika mchakato huo.
Askofu Bagonza ametaja sumu hizo kuwa ni matumizi ya hila, kutafuta mshindi, kuukwepa ukweli, matumizi mabaya ya madaraka na kujinufaisha binafsi au kimakundi kupitia maridhiano.
Askofu Bagonza amesema hayo leo Jumapili Desemba 21, 2025, katika Ibada ya Ubarikio wa Wachungaji wa Dayosisi ya Karagwe Usharika wa Lukajange- Kanisa kuu, mkoani Kagera.
Katika Ibada hiyo, Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, George Simbachawene alikuwa mgeni maalumu akimuwakilisha Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba.
Askofu Bagonza amesisitiza, endapo mambo hayo hayataepukwa, maridhiano hayawezi kuzaa matunda wala kuponya Taifa.
Ushauri huo umeungwa mkono na Waziri Simbachawene akisema Serikali inakubaliana na msingi huo kwa kuwa unakwenda sambamba na dhamira ya Rais, Samia Suluhu Hassan ya kujenga Taifa lenye umoja, haki, mshikamano na amani ya kudumu.
“Nataka niwahakikishe, kwa niaba ya Serikali, naijua dhamira ya Rais Samia kwa Taifa letu, ndiyo maana ameunda Tume ya Uchuguzi haraka sana, tume hii itatupa ukweli, na kwa kuwa mjadala utakuwa wa wazi baada ya kupatikana kwa ripoti kutoka kwenye tume hiyo, tutajadiliana na tutakosoana kama Taifa, ili nchi yetu iweze kupona,”amesema Simbachawene.
Novemba, 2025, Rais Samia akizindua Tume ya Uchunguzi wa Matukio ya Uvunjifu wa Amani yaliyojitokeza wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, alisema tume hiyo inapaswa kuchunguza kiini cha vurugu na malalamiko yaliyowasukuma vijana kuingia mitaani, ikiwamo kubaini ni haki gani waliyoamini wameikosa.
“Tunatarajia ikatuangalizie sababu hasa iliyoleta kadhia ile ni nini? Kiini cha tatizo ni nini? Na wakati inatokea kadhia ile vijana waliingizwa barabarani kudai haki? Tunataka kujua haki gani ambayo vijana hawa wameikosa ili tuweze kuifanyia kazi na wapate haki yao,” alisema Rais Samia akiielekeza tume hiyo.
Akizungumza katika ibada hiyo, Askofu Bagonza amesema awali alitaja makundi machache yaliyohitaji maridhiano, lakini kwa sasa hali imebadilika na Taifa linahitaji maridhiano zaidi kuliko wakati wowote ule.
Amesema nje ya maridhiano hakuna uhakika wa Taifa kufikia malengo yake kwa sababu hata wanaolalamikiwa nao wana malalamiko yao.
“Taifa lenye manung’uniko ni gumu kuliongoza, hivyo maridhiano yanahitajika kwa gharama yoyote,” amesema Askofu Bagonza akisisitiza kuwa maridhiano hayo yanapaswa kuwa ya kweli, si ya juu juu au ya kisiasa.
Akieleza sumu ya kwanza, Askofu Bagonza amesema ni matumizi ya hila, akisema mara nyingi hila hupewa majina mazuri kwa kisingizio cha masilahi ya Taifa, jambo linaloharibu misingi ya maridhiano.
Amesisitiza Taifa haliwezi kuongozwa kwa ujanja ujanja, akimkumbuka hayati Mwalimu Julius Nyerere aliyewahi kulionya Taifa dhidi ya uongozi wa namna hiyo.
Sumu ya pili aliyoitaja ni kutafuta ushindi katika mchakato wa maridhiano.
Amesema hakuna mshindi wala mshindwa katika maridhiano ya kweli, akisema ushindi wa upande mmoja huandaa mazingira ya vurugu na migogoro mipya siku za baadaye.
“Ushindi katika maridhiano huwa si ushindi wa kweli, bali ni vurugu zilizowekwa akiba,” amesema Askofu Bagonza.
Sumu ya tatu ameitaja kuwa ni kuukwepa ukweli akisema maridhiano ya kweli hujengwa juu ya ukweli, hata kama ukweli huo unaumiza pande zote.
Amesema duniani kote, mifano ya maridhiano yaliyofanikiwa imejengwa juu ya kusema ukweli bila kulaumiana, akibainisha bila ukweli, hakuna uponyaji wa Taifa.
Sumu ya nne ni matumizi mabaya ya madaraka akisema wakati wa maridhiano, wale wenye madaraka wanapaswa kuyaweka pembeni na kuingia katika mchakato kama wahusika wanaotafuta uponyaji, akifananisha maridhiano na chumba cha wagonjwa ambao wote ni majeruhi.
Sumu ya tano ni kujinufaisha na maridhiano, akisema tamaa ya kupata nafasi, masilahi au faida binafsi kabla au baada ya maridhiano ni mgongano wa masilahi utakaoharibu mchakato mzima.
Amesema ikiwezekana watu wa aina hiyo wasishirikishwe katika mchakato huo wa maridhiano.
Pia, amesema maridhiano ya kweli yana gharama za kiuchumi, kijamii, kisiasa na kisera, ambazo Taifa linapaswa kuzikubali ili kujenga Tanzania mpya.
Askofu huyo amesisitiza kuwa, miiko ya Taifa iliyokiukwa, dawa yake ni toba ya dhati.
Hata hivyo, amempongeza Waziri Mkuu, Dk Mwigulu kwa kuhimiza uwazi na kuruhusu watu kufunguka katika mikutano yake, akisisitiza kuwa, wale wanaothubutu kusema wanapaswa kubaki salama ili kuwahamasisha wengine kutoa maoni yao kwa masilahi mapana ya Taifa.
Akizungumza katika ibada hiyo, Waziri Simbachawene amesema Serikali imepokea kwa heshima na ushauri huo, aliouita kuwa mzito hasa katika kipindi hiki.
Amesema msingi wa maridhiano tayari umeshawekwa na Rais Samia alipounda Tume ya Uchunguzi wa matukio hayo na kuwateua wajumbe wanaoheshimika katika Taifa kushughulikia.
Amesema dhamira ya Rais Samia ni kutaka kuona ukweli unapatikana na Taifa linajadili kwa uwazi ili kupona.
“Serikali inakubaliana na msingi huu kwa sababu ndio msingi ambao Rais wetu ameuweka. Maridhiano hayawezi kujengwa kwa hila, kwa masilahi ya muda mfupi au kwa kukwepa ukweli,” amesema Simbachawene.
Mchambuzi wa masuala ya siasa, Samson Sombi akizungumza na Mwananchi, amesema ni muhimu kwa wanasiasa kujiepusha na tabia ya kutumia mchakato wa maridhiano ya kitaifa kwa masilahi binafsi ya kisiasa.
Amesema maridhiano yanapaswa kutumika kama nyenzo ya kuliunganisha Taifa na kuliponya dhidi ya migawanyiko.
Sombi amesema anaunga mkono kauli ya Askofu Bagonza, kuhusu umuhimu wa maridhiano ya kweli na tahadhari dhidi ya mambo yanayoweza kudhoofisha.
Amesema mambo yote yaliyotajwa na askofu, yakiwamo ya kutafuta ushindi, kuukwepa ukweli, matumizi mabaya ya madaraka na kujinufaisha binafsi, yanapaswa kuepukwa ili maridhiano yawe na tija kwa Taifa.
Sombi amesema dhamira ya Rais Samia kuhusu maridhiano tayari imeonekana wazi kupitia hatua mbalimbali, ikiwamo ya kuundwa kwa Tume ya Uchunguzi, ambayo ni hatua muhimu katika kufikia lengo la kujenga Tanzania mpya yenye mshikamano, amani na haki.
“Maridhiano ni muhimu kama alivyosema askofu. Mambo yote aliyoyataja ni ya msingi na hayapaswi kupuuzwa. Hata Rais wetu ameonesha dhamira ya dhati ya maridhiano na uwepo wa tume ni hatua muhimu kuelekea tunakotaka kama Taifa, yaani kujenga Tanzania mpya yenye mshikamano,” amesema Sombi.
