Ilichokisema mahakama hukumu ya aliyegongwa na mwendokasi

Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imeiamuru Kampuni ya UDA Rapid Transport Limited Company (UDART), inayotoa huduma za usafiri wa mabasi yaendayo haraka maarufu mabasi ya mwendokasi, kumlipa fidia ya Sh85 milioni mwenda kwa miguu, Frank Zebaza aliyegongwa na basi lake.

Mahakama hiyo pia imeamuru dereva aliyekuwa akiendesha basi hilo, Hafidhi Ally kumlipa Frank fidia ya adhabu Sh10 milioni, huku ikieleza alivyopuuza sheria na wajibu wake.

Mahakama imetoa uamuzi huo kutokana na kesi hiyo ya madai ya fidia namba 28992 ya mwaka 2024 iliyofunguliwa na Frank dhidi ya UDART, dereva huyo, Shirika la Taifa la Bima na Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG).

Uamuzi huo umetolewa na Jaji Griffin Mwakapeje, baada ya kuridhika na ushahidi wa mdai kuwa gari la kampuni hiyo likiendeshwa na dereva huyo lilihusika katika ajali hiyo.

Katika kesi hiyo, Frank aliiomba mahakama hiyo iwaamuru wadaiwa wamlipe jumla ya Sh600 milioni, Sh350 milioni zikiwa ni fidia maalumu kwa gharama za matibabu na matumizi mengine yanayohusiana.

Sh150 milioni fidia ya madhara ya jumla kwa maumivu na mateso aliyoyapata, na Sh100 milioni ikiwa ni fidia ya adhabu.

Vilevile aliomba alipwe gharama za kesi, riba ya asilimia ya kiwango cha mahakama katika kiasi cha jumla ya malipo ya fidia hiyo kuanzia Septemba 30, 2023 hadi malipo kamili yatakapokamilika na nafuu nyinginezo ambazo mahakama itaona zinafaa.

Ingawa mdaiwa wa kwanza UDART, wa tatu (NIC) na wa nne (AG) walipinga madai hayo, mahakama baada ya kusikiliza pande zote isipokuwa dereva Hafidhi ambaye hakujitetea,  imekubaliana na madai ya Frank ikisema kuwa amethibitisha madai hayo dhidi ya wadaiwa.

Hata hivyo, kuhusu fidia Jaji Mwakapeje amesema risiti halali za matibabu zinaonesha matumizi ya Sh3,850,600, hivyo amesema kinachotolewa hapo kama fidia maalumu, kinacholipwa na mdaiwa wa kwanza ni Sh3,850,600.

Kuhusu fidia ya jumla, Jaji Mwakapeje baada ya kutathmini madhara aliyoyapata mlalamikaji, amesema kwa kuzingatia uzito wa majeraha, athari zake za muda mrefu, na mazingira ya jumla ya shauri hilo, mahakama kwa matumizi sahihi ya busara yake, inatoa Sh85 milioni ambayo italipwa na UDART.

Kuhusu adhabu ya adhabu Jaji Mwakapeje amesema fidia hiyo si ya kufidia hasara, bali ni ya adhabu, na lazima iwe ya uwiano na imlenga moja kwa moja mhusika aliyefanya kosa hilo binafsi.

“Hivyo, mahakama inatoa Sh10 milioni kama fidia ya adhabu, kiasi kinacholipwa na mdaiwa wa pili,” ameamuru Jaji Mwakapeje.

Pia, ameamuru mdai alipwe riba kwa kiwango cha mahakama cha asilimia saba kwa mwaka ya jumla ya fidia yote kuanzia tarehe ya hukumu hadi malipo kamili yatakapofanyika na gharama za kesi.

Katika kesi hiyo, mdai aliwakilishwa na wakili Habiba Katwe, na wadaiwa wa kwanza, wa tatu na wa nne waliwakilishwa na Wakili wa Serikali Mkuu, Jesca Shengena, akisaidiwa na mawakii wa Serikali Mathew Fuko na Abeid Buzohela.

Frank, aliyekuwa shahidi pekee kwa mujibu wa ushahidi wake, Septemba 30, 2022, saa 11:20 jioni, alikuwa anavuka barabara kihalali kwenye kivuko cha waenda kwa miguu (zebra crossing) eneo la Kariakoo (eneo la fire) kando ya Barabara ya Morogoro.

Akiwa kwenye mstari wa tatu mweupe wa zebra na akiwa na haki ya kuvuka barabara kwa kuwa alama za barabarani ziliruhusu waenda kwa miguu kuvuka, aligongwa na gari linalodaiwa kumilikiwa na mdaiwa wa kwanza UDART.

Alipata majeraha makubwa ya kichwa yaliyomfanya apoteze fahamu na alipata fahamu tena akiwa hospitalini, ambapo alielezwa na ndugu zake kuwa polisi walitoa fomu ya PF3 kwa ajili ya matibabu yake.

Alilazwa katika Hospitali ya Taifa Muhimbili (MOI), ambapo kipimo cha CT scan kilibaini kuvunjika kwa fuvu la kichwa upande wa kulia, hali iliyohitaji kufanyiwa upasuaji wa ubongo.

Hivyo, alishauriwa kuishi katika mazingira tulivu wakati wa kupona na alihamia Mikocheni kutoka Makondeko kwa sababu za kiafya.

Kutokana na madhara hayo anaathiriwa na baridi na mwanga, hupata maumivu ya kichwa ya mara kwa mara na kukosa kumbukumbu.

Baadaye alithibitisha kutoka polisi kuwa dereva, Hafidhi Ally, alitiwa hatiani kuhusiana na ajali hiyo na nakala ya uamuzi kama Kielelezo P4.

Shahidi wa kwanza wa utetezi, Amani Kabela ambaye ni ofisa wa madai wa NIC alieleza kuwa  magari ya mdaiwa wa kwanza, UDART yamekatwa bima na mdaiwa wa kwanza wa tatu (NIC).

Alidai kuwa dai la mlalamikaji halikushughulikiwa kwa sababu namba ya usajili wa gari iliyowasilishwa katika dai la awali ilikuwa T132 DGV, ambayo alisema haikuwa imekatwa bima na NIC.

Alieleza kuwa NIC iliandikia mahakama ya wilaya iliyosikiliza shauri la jinai kuomba ufafanuzi juu ya gari lililohusika kati ya T132 DGW au T132 DGV. Mahakama ilijibu ikitaja T132 DGV, jambo lililoifanya NIC kukataa kuwajibika.

Shahidi wa pili upande wa madai Zubeda Ally, Ofisa Sheria wa UDART, alidai mlalamikaji alidai kwa uongo kuwa gari la Udart lilihusika katika ajali kwa kuwa kielelezo cha nne hakiamini kwa kuwa kinaonesha namba za usajili zinazokinzana.

Alidai kuwa kuwa gari lililohusika lilikuwa T132 DGV, ambalo alidai si mali ya UDART, hivyo akaomba shauri litupiliwe mbali dhidi ya UDART.

Hata hivyo, wakati wa maswali ya dodoso alikiri hahusiki na kumbukumbu za ajira na hivyo hakuthibitisha kama dereva aliyehusika katika ajali, Hafidhi, alikuwa mfanyakazi wa UDART wakati husika.

Pia alikubali kuwa hana ushahidi wa maandishi unaoonesha kuwa Hafidhi hakuwa akiendesha gari la UDART tarehe ya ajali, wala uthibitisho wowote kuwa hakusababisha ajali, huku akikiri kuwa kuwa kampuni (UDART) iliarifiwa kuwa Hafidhi alikuwa ameshtakiwa kwa kosa la barabarani.

Katika uamuzi wake, Jaji Mwakapeje amesema jambo la msingi na ambalo halikupingwa, ni kwamba gari lililohusika lilikuwa mali ya UDART.

Amesema kuwa pia haikupingwa kuwa lilikuwa likiendeshwa na Hafidhi, wakati husika na kwamba alikamatwa, alishtakiwa na kutiwa hatiani kwa kosa la uendeshaji hatarishi lililotokana na tukio hilo hilo.

Pia Jaji Mwakapeje amekubaliana na mdai kuwa kuwa ushahidi wake unathibitisha kuwa Hafidhi alitenda kwa uzembe, na kwamba mdai alikuwa akitumia kivuko rasmi cha waenda kwa miguu kihalali baada ya magari kusimamishwa na taa nyekundu.

“Katika shauri hili, mdaiwa wa pili (Hafidhi) aliendelea kuendesha gari kwa dharau kubwa dhidi ya alama za barabarani na haki za waenda kwa miguu, jambo lililosababisha majeraha makubwa ya mwili kwa mlalamikaji,” amesema Jaji Mwakapeje na kusisisitiza:

“Kwa hiyo, kwa kuzingatia ushahidi wa mlalamikaji usiopingwa, na wajibu wa kisheria unaowekwa kwa madereva katika vivuko vya waenda kwa miguu, mahakama inaridhika kwamba mdaiwa wa pili alitenda kwa uzembe.”

Amesema kuwa kwa kanuni ya dhima mbadala ambayo humfanya mwajiri kuwajibika kisheria kwa vitendo visivyo halali vinavyofanywa na mfanyakazi wake wakati wa utekelezaji wa kazi na ndani ya wigo wa ajira yake, UDART nayo inawajibika.

“Msingi wa kanuni hii ni kwamba waajiri wana mamlaka ya kudhibiti namna wafanyakazi wanavyotekeleza majukumu yao na hunufaika kiuchumi na kazi zao; kwa mantiki hiyo, wanapaswa pia kubeba hatari zinazotokana na utekelezaji wa majukumu hayo,” amesema Jaji Mwakapeje.

Amesema kuwa kwa kuzingatiwa kwamba vitendo vya uzembe vilifanywa wakati wa utekelezaji wa kazi na wakati akiendesha gari la mdaiwa wa kwanza mahakama inaona kwamba mdaiwa wa kwanza anawajibika kwa misingi ya dhima mbadala kwa mwenendo usio halali wa dereva wake.

Kuhusu wajibu wa NIC, Jaji Mwakapeje amesema kuwa mahakama imebaini kuwa tofauti ya namba za usajili wa gari lililohusika na ajali, hilo ni kosa la kiuandishi.

Hata hivyo amesema kuwa kutokana na kukosekana kwa ushahidi wa mwisho unaounganisha moja kwa moja gari lililokatwa bima (T132 DGW) na gari lililotajwa katika kumbukumbu za shauri la barabarani (T132 DGV), Mahakama haiwezi, kisheria, kupanua dhima hiyo kwa mkata bima.