Dar es Salaam. Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) kwa kushirikiana na Bohari ya Dawa (MSD) wamepanga kambi maalumu ya upimaji magonjwa ya moyo na mengine yasiyoambukiza.
Kambi hiyo inayotarajiwa kutoa huduma hizo, itaanzia jijini Dar es Salaam kesho Jumanne, Desemba 23, 2025 ikihusisha waandishi na wahariri wa vyombo vya habari, kisha kambi ya makundi yote itafanyika jijini Arusha kuanzia Desemba 29, 2025 hadi Januari 6, 2026.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, leo Jumatatu Desemba 22, 2025, Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Dk Peter Kisenge amesema huduma hiyo ni mwendelezo wa juhudi za taasisi hiyo katika kuhakikisha Watanzania wenye uhitaji wanafikiwa na huduma ili kudhibiti maradhi ya moyo na magonjwa yasiyo ambukiza nchini.
“Kwa upendo mkubwa tunayo furaha kuwajulisha Watanzania kuanzia Desemba 29, 2025 hadi Januari 6, 2026 tutaanza kambi Arusha, katika Hospitali ya Arusha Lutheran Center, tutapima makundi yote, watoto na watu wazima,” amesema.
Amesisitiza kuwa kama isemavyo kauli mbiu ya taasisi hiyo, ‘Afya ya moyo ni jukumu letu’ taasisi hiyo imekuwa ikizunguka na kuweka kambi katika mikoa mbalimbali nchini ili kuhakikisha watu wote wenye matatizo hayo wanafikiwa.
“Niwaombe wananchi, tunapomaliza mwaka na kuanza mwaka, hakikisha unapima mwili wako ujue hali ya afya yako na moyo wako ili kujiwekea mazingira salama,” amesema.
Kuhusu waandishi na wahariri wa vyombo vya habari, Mkurugenzi huyo amesema, JKCI imekuwa na utaratibu wa kuyafikia makundi mbalimbali, awamu hii ni zamu ya kundi hilo kama lilivyoahidiwa awamu iliyopita.
“Katika utaratibu wetu kuyafikia makundi mbalimbali, tulitoa ahadi pia kwa waandishi na wahariri wa vyombo vya habari, hivyo niwakaribishe jitokezeni kwa wingi kuanzia kesho na kesho kutwa pale ofisi yetu ya Oysterbay, huduma zote zitatolewa bure,” amesema.
Alitaja huduma zitakazotolewa, amesema kutakuwa na upimaji wa moyo na magonjwa yasiyoambukiza, sambamba na utoaji wa huduma za matibabu kwa watakaokutwa na matatizo.
Akitaja sababu za kuuchagua Mkoa wa Arusha, Mkurugenzi huyo amesema kuwa ni mkoa unaopokea watalii wengi, akiitaja pia kuwa mwakani utahusika na mashindano ya fainali za Kombe la Mataifa Afrika (Afcon), hali inayoufanya kuwa mkoa wa kimkakati kupatiwa huduma hiyo.
“JKCI tumekuwa tukitoa huduma hizi, tumezunguka zaidi ya mikoa 20, tumekutana na wagonjwa zaidi ya 26 elfu ambao asilimia 12 kati yao walikuwa hawajijui kama wana tatizo hilo.
“Wapo watoto ambao walikuwa na matundu ya moyo walikuwa hawajijui wanatumia dawa za mafua bila kujua tatizo walilokuwa nalo,” amefafanua.
Amesema katika kambi iliyofanyika Arusha awamu iliyopita mwitikio ulikuwa mkubwa hali iliyoonesha uhitaji mkubwa wa huduma hiyo katika kanda hiyo.
Akitaja umuhimu wa kupima afya ya moyo na magonjwa yasiyoambukiza, Mkurugenzi huyo amegusia suala la gharama za matibabu.
Amesema gharama ya matibabu ya moyo ni kubwa sana kwa mtu binafsi kuimudu, akishukuru mchango wa Serikali na wadau katika kuchangia matibabu kwa wasioweza kumudu gharama.
“Matibabu ya moyo yana gharama kubwa sana kuibeba mtu binafsi, lakini tunashukuru Serikali yetu hivi karibuni tunakwenda kuwa na bima kwa wote itakayosaidia hilo.
“Kwa sasa, gharama nyingi wamekuwa wakilipiwa na Serikali, kwa kufuata taratibu zilizowekwa, huku na sisi taasisi tumekuwa tukitoa msamaha wa takribani Sh200 milioni kila mwaka kwa watoto,” amesema.
Ameongeza kuwa, pia wadau mbalimbali wamekuwa wakichangia, akitolea mfano mwaka jana ambao Taasisi hiyo ilichangisha zaidi ya Sh3 bilioni kwa ajili ya kulipia wagonjwa wasioweza kumudu gharama za matibabu hayo.
Akielezea hali ya tatizo la magonjwa hayo nchini, Mkurugenzi wa Magonjwa ya Moyo wa taasisi hiyo, Dk Tatizo Waane amesema taasisi imeiteua kanda ya kaskazini kunufaika na kambi hiyo kutokana na uhitaji mkubwa wa huduma hiyo uliopo katika mkoa wa Arusha na mikoa jirani.
“Kwa uzoefu wetu wa miaka 20, JKCI tumebaini kuwa asilimia kubwa ya wagonjwa wanaopatikana na magonjwa hayo wanatoka mikoa ya kaskazini, hivyo, kuweka kambi hiyo kupitia hospitali ya Lutheran tutaweza kusaidia kukabiliana na tatizo hilo,” amesema.
Akitaja baadhi ya tabia zinazochangia watu kupata magonjwa ya moyo na mengine yasiyoambukiza, Mtaalamu huyo amesema baadhi ya tabia zinazopelekea magonjwa haya ni pamoja na unywaji wa pombe kupita kiasi, kutokufanya mazoezi, msongo wa mawazo na kuwa na uzito kupitiliza.
“Ni vyema kuzingatia mambo haya muhimu na kupima afya mara kwa mara ili kuhakikisha unabaki salama na kuepuka gharama kubwa za matibabu,” amesisitiza.
Kwa upande wake, Meneja wa Mawasiliano na Uhusiano wa MSD, Etty Kusiluka amesema MSD imejipanga vyema kuhakikisha vifaa na dawa zote zinazohitajika katika kambi hiyo zinapatikana kwa wakati ili kurahisisha utoaji huduma.
“Sisi MSD ni mdau muhimu katika kuwezesha huduma hizo kwakuwa wataalamu hao watahitaji bidhaa za afya kukamilisha upimaji na matibabu ya magonjwa yatakayobainika.
“Mpaka sasa JKCI wameshawasilisha mahitaji yao ya vifaa na dawa wanazohitaji, kwa hiyo sisi tutakuwepo pale kuhakikisha tunawapatia mahitaji hayo,” amesema.
