UONGOZI wa Pamba Jiji umefungua mazungumzo ya kupata saini ya kipa wa Mbeya City, Hashim Mussa, baada ya kudaiwa nyota huyo anatafuta changamoto sehemu nyingine, kutokana na kutopata nafasi ya kucheza kikosi cha kwanza mara kwa mara.
Kipa huyo mkataba alionao na City unaisha mwishoni mwa msimu huu, ambapo hadi sasa ameshindwa kupenya kikosi cha kwanza kutokana na uwepo wa Benno Kakolanya, jambo linalomfanya kutafuta sehemu nyingine itakayompa nafasi ya kuonyesha kiwango chake.
Baada ya nyota huyo kuweka wazi anahitaji kucheza mara kwa mara, uongozi wa Mbeya City unafanya mazungumzo ya kuachana naye katika dirisha dogo la Januari litakapofunguliwa, huku Pamba ikiwa ndio iliyoonyesha kumuhitaji.
Hata hivyo, mtu wa karibu na mchezaji huyo, aliliambia Mwanaspoti kiwango kinachoonyeshwa na Yona Amos huenda ikawa ni kikwazo kwake kujiunga na Pamba katika dirisha dogo, kwa sababu malengo yake ni kupata timu itayompa nafasi ya kucheza.
Akizungumzia suala hilo, Ofisa Mtendaji Mkuu wa Pamba Jiji (CEO), Peter Juma Lehhet, amesema wanaendelea kupitia ripoti ya benchi la ufundi ili kuboresha kikosi hicho, ingawa ni mapema kwa sasa kuzungumzia ni mchezaji gani watakayemsajili Januari.
Kipa huyo anashikilia rekodi ya kupandisha timu mbili kutokea Championship hadi Ligi Kuu Bara, ambapo alianza akiwa na kikosi cha maafande wa Mashujaa ya Kigoma msimu wa 2022-2023, kisha msimu uliopita wa 2024-2025, akiichezea Mbeya City.
