Latra yaonya wanaolipisha leseni bila kibali

Songwe. Mamlaka y Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) imepiga marufuku watu wanaochukua tenda za kulipisha leseni za bajaji na pikipiki kufanya msako wa kuwakamata wasiolipa leseni na kuwatoza fedha zinazodaiwa kuwa ni rushwa. Ikieleza hakuna sheria inayowaruhusu kufanya hivyo.

Kauli hiyo ilitolewa na ofisa wa sheria kutoka Latra,  makao makuu Dodoma, Martha Ngaga kwenye semina elekezi iliyotolewa na maofisa wa Latra katika ukumbi wa Jeshi la Polisi uliopo mkoani Songwe, ukihudhuriwa na wamiliki wa vyombo vya moto, madereva, makondakta na askari wa kikosi cha usalama barabarani.

Ngaga alitoa kauli hiyo kwenye kikao hicho baada ya Mwenyekiti wa waendesha bodaboda mkoani Songwe, Omary Mbuba kupongeza   elimu iliyotolewa ya usalama barabarani, lakini wanataka kujua sababu ya waliopewa tenda za kukamata pikipiki zisizo na leseni na kusababisha ajali.

Amesema waliopewa tenda za uwakala wa kukatisha leseni wamekuwa wakivaa sare zenye nembo za Latra na kukimbizana na waendesha pikipiki na bajali kufanya ukaguzi na kusababisha ajali, wakati sheria haiwaruhusu na hakuna hatua za kisheria zinazochukuliwa dhidi yao.

‘’Ndugu mwezeshaji, kila kijiwe cha bodaboda kina viongozi wake, kama mmewapa mamlaka hayo ni bora mngetueleza ili kukwepa migongano iliyopo kwani watu hao wamekuwa wakikusanya fedha zisizo katika mpangilio na kusababisha taharuki,”amesema Mbuba.

Ngaga amesema hakuna sheria inayoruhusu mbia wa kukatisha leseni na kuendesha msako.

Amesema mkataba wa mbia  na Latra ni kukatisha leseni, tena awe kwenye ofisi yake inayotambuliwa na sio kuzunguka mitaani kufanya msako,

“Kosa lingine ni kutumia nembo ya Latra kuzunguka mitaani kukusanya fedha, huku akipiga marufuku mfumo huo na watakaobainika watachukuliwa hatua kali kwa mujibu wa sheria,” amesema Nganga.

Katika semina hiyo, Irene Sawe ambaye ni ofisa sheria wa  Latra,  mkoani Songwe, amesema Serikali imeweka wazi mipango mizuri na ndiyo maana wamekuwa wakiwafikia pale walipo kuwakumbusha madereva na wamiliki wa vyombo vya moto kuzijua sheria.