Dar es Salaam. Wakati baadhi ya wananchi katika maeneo mbalimbali nchini wakiendelea kukabiliwa na upungufu wa huduma ya maji safi na salama, Serikali imetangaza mpango wa kuunganisha miradi ya maji katika gridi ya Taifa kama suluhu ya kudumu ya changamoto hiyo.
Mpango huo unalenga kuongeza ufanisi katika uzalishaji na usambazaji wa maji kwa kuunganisha miradi yote mikubwa na midogo, ili kuhakikisha huduma ya maji inapatikana kwa uhakika katika maeneo ya mijini na vijijini, bila ya kutenganisha ufanisi wa maeneo hayo.
Hata hivyo, Kaimu Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Fulgence Massawe amesema leo Jumapili Desemba 21, 2025 kuwa, haoni uwezekano wa kutekelezeka kwa wazo la kuunganisha nchi nzima kwa gridi ya Taifa ya maji, akisisitiza kuwa Tanzania haina uhaba wa maji, bali changamoto iliyopo ni usimamizi wa rasilimali zilizopo na vipaumbele vya kitaifa.
Massawe amesema nchi zilizoendelea zimefanikiwa kukabiliana na changamoto ya maji kwa kuvuna maji ya mvua na kuyahifadhi kwa matumizi ya baadaye.
“Vyanzo vya maji vinategemea jiografia ya maeneo husika, hivyo si rahisi kusambaza maji kutoka eneo moja kwenda jingine bila kuzingatia gharama na uhalisia wa uzalishaji. Kila eneo linapaswa kuwa na chanzo chake cha uhakika kulingana na mazingira yake.”
Massawe amepongeza juhudi za Serikali katika kanda ya kati na kanda ya ziwa, hususan mradi wa kuchukua maji kutoka Ziwa Victoria, akisema hatua kama hizo zinawezekana pia kwa maeneo mengine kama Kilimanjaro au Arusha, lakini kila eneo linapaswa kuwa na mkakati wake maalumu.
“Ni muhimu Serikali itunge sera kuitaka kila halmashauri kuwa na mkakati wa uhakika wa vyanzo vya maji, Serikali ilitakiwa kusimamia utekelezaji wake,” ameshauri
Lakini akizungumza leo Jumapili Desemba 21, 2025, Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba wakati anakagua Mradi wa maji unaojengwa kwa Sh119 bilioni Ruangwa, amesema, Serikali inalazimika kuhakikisha thamani ya fedha za walipa kodi inaonekana kupitia miradi ya maji inayotekelezwa.
Dk Mwigulu amesisitiza kuwa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) imeweka kipaumbele kikubwa katika kuwapatia Watanzania huduma ya majisafi na salama.
Waziri mkuu huyo amesema mabadiliko ya tabianchi yameathiri kwa kiasi kikubwa upatikanaji wa maji, hali ambayo imesababisha changamoto kuendelea kujitokeza hata katika maeneo yenye miundombinu ya maji.
“Mabadiliko ya tabianchi ni tatizo la dunia nzima. Kama Watanzania, tuna wajibu wa kuchukua hatua za kukabiliana nalo. Serikali imepiga hatua kubwa katika utekelezaji wa Ilani ya sasa, tunaenda kwenye gridi ya Taifa ya maji, tunaimarisha uwiano wa utekelezaji wa miradi mikubwa na midogo ili kukabiliana na tatizo la maji kwa ufanisi,” amesema Dk Mwigulu.
Kupitia hatua hiyo, mbali ya kuongeza ufanisi wa miradi ya maji, amesema Serikali inalenga kupunguza upotevu na kuboresha usimamizi wa rasilimali za maji kwa manufaa ya wananchi.
Makandarasi wazembe kutengwa
Katika hatua nyingine, Dk Mwigulu ameapa Serikali kutowapa miradi ya maendeleo makandarasi watakaoshindwa kutekeleza majukumu yao kwa viwango vinavyokubalika na kwa muda uliopangwa, hatua inayolenga kulinda fedha za umma na kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora kwa wakati.
Dk Mwigulu amewataka makandarasi kuhakikisha fedha wanazopokea zinaendana na kazi inayotekelezwa, akisisitiza kuwa, Serikali haitavumilia uzembe wala ubadhirifu wa rasilimali za umma.
“Hakishapokea fedha mkandarasi, tunataka tuione thamani ya fedha hiyo kwenye kazi iliyofanyika,” amesema Dk Mwigulu.
Amemuelekeza Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Maji na Usafi wa Mazingira Vijijini (Riwasa) kufanya tathmini ya miradi yote iliyopokea malipo ya awali na mengineyo na kubainisha wazembe.
“Tunahitaji kuona thamani ya fedha kwenye kazi iliyotekelezwa. Pale tutakapobaini mkandarasi amefanya kazi kidogo isiyoendana na fedha alizolipwa, tutachukua hatua kali ikiwamo kuwanyima fursa ya kupewa miradi mingine ya Serikali,” amesema Dk Mwigulu.
Msajili wa Bodi ya Usajili wa Makandarasi (CRB), Rhoben Nkori amesema kuwa Sheria ya Ununuzi wa Umma inaelekeza kuwa mkandarasi anayeshindwa kutekeleza miradi kwa mujibu wa mkataba, anapaswa kunyimwa fursa au kufungiwa kabisa kushiriki katika miradi ya umma.
Amesema kwa mujibu wa sheria, makandarasi wanawajibika kutekeleza majukumu yao kwa kuzingatia masharti ya kisheria na mikataba waliyoingia, ikiwamo kutekeleza miradi kwa wakati, kwa viwango vinavyotakiwa na kwa kuzingatia thamani na hadhi waliyopewa.
“Endapo mkandarasi atakiuka masharti hayo, sheria ya makandarasi huchukua mkondo wake kulingana na ukubwa wa kosa alilofanya, hatua kali zaidi ni kufutiwa kabisa usajili na kuondolewa katika orodha ya wakandarasi,” amesema Nkori.
Amesema ili mkandarasi aweze kutekeleza miradi ya ujenzi ni lazima awe na usajili hai katika orodha ya makandarasi, akibainisha kuwa CRB imewahi kuchukua hatua mbalimbali dhidi ya makandarasi wengi waliokiuka taratibu, hatua ambazo zote zipo kwenye kumbukumbu za bodi hiyo.
Waziri wa Maji, Jumaa Aweso amesema ujenzi mradi huo wa maji uliokaguliwa na Waziri Mkuu wilayani Ruangwa ulitokana na ombi maalumu la aliyekuwa mbunge wa Ruangwa na Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa.
Aweso amesema Majaliwa aliomba utekelezaji wa mradi huo baada ya kubaini kuwa licha ya wananchi kupata maji, yalikuwa na chumvi nyingi kutokana na aina ya madini yaliyopo eneo hilo, hali iliyokuwa ikihatarisha afya zao.
“Baada ya ombi hilo, Rais alitoa maelekezo ya mradi kuanza mara moja ili wananchi wapate majisafi na salama. Mradi huu unagharimu Sh119 bilioni na fedha zote tayari zimetolewa kwa mkandarasi, hakuna deni lolote,” amesema Aweso.
Mbunge wa Ruangwa na Naibu Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Kaspar Mmuya amesema kukamilika kwake kutawanufaisha zaidi wakazi 100,000 wa jimbo hilo.
Mmuya amesema hali ya upatikanaji wa maji mwaka 2020 ilikuwa asilimia 55 kwa maeneo ya mjini na asilimia 60 vijijini, lakini katika kipindi cha Serikali ya Awamu ya Sita upatikanaji wa maji umeongezeka hadi kufikia asilimia 71 mjini na asilimia 74 vijijini.
Amesema kukamilika kwa mradi huo kutafanya zaidi ya asilimia 90 ya wananchi wa Ruangwa kupata huduma ya majisafi na salama, huku akisema mradi huo ni miongoni mwa mafanikio makubwa ya kusikilizwa kwa kilio cha wananchi na utekelezaji wa ahadi za Serikali.
