Mitazamo tofauti kuhusu Krismasi | Mwananchi

Dar es Salaam. Katika jamii ya kisasa inayokabiliwa na changamoto za kiuchumi, kijamii na kiutu, maisha ya kujali wengine wakati wa sikukuu ya Krismasi yameendelea kutajwa kuwa nguzo muhimu ya mshikamano na utu.

Hata hivyo, baadhi ya watu wanahoji kuwa mwenendo huo wakati mwingine hujaa maigizo na hauakisi ipasavyo uhalisia wa maisha ya kila siku.

Zaidi ya kuwa sherehe ya kidini, Krismasi imejengeka kama kipindi cha kukumbushana wajibu wa kutoa, kushirikiana na kuwajali wengine bila kujali tofauti za imani, kabila au hali ya maisha. Ni wakati unaotumiwa kuhimiza mshikamano wa kijamii na kuimarisha misingi ya utu.

Katika miji na vijiji mbalimbali, msimu wa Krismasi hushuhudia ongezeko la vitendo vya ukarimu, ikiwemo utoaji wa msaada kwa wahitaji kama watoto yatima, wazee, wagonjwa na familia zenye kipato cha chini.

Mashirika mbalimbali, taasisi za kidini na watu binafsi huungana kukusanya vyakula, mavazi, vifaa mbalimbali na misaada mingine, ambayo hupelekwa kwa wahitaji kama ishara ya mshikamano na kujali, hasa kwa makundi yaliyo katika mazingira magumu.

Wadau wa masuala ya jamii wanasema utamaduni wa kutoa zawadi na misaada wakati wa Krismasi unabeba ujumbe mpana wa kibinadamu unaopaswa kuendelezwa katika maisha ya kila siku, badala ya kusubiri msimu wa sikukuu pekee.

Akizungumza na Mwananchi leo Desemba 22, 2025, Richard Maiko amesema kutoa na kuwajali wengine ni misingi muhimu ya kujenga jamii imara yenye utu. Amesema Krismasi huwakumbusha watu kuwa tofauti za kidini au kiitikadi hazipaswi kuwa kikwazo cha kuishi kwa upendo, amani na mshikamano.

Maiko amesema katika mazingira ya sasa, ambayo baadhi ya watu wanakabiliwa na upweke, msongo wa mawazo na kukata tamaa, kushirikiana na kujali wengine inakuwa tiba muhimu kwa watu wa aina hiyo.

Ameongeza kuwa kipindi cha Krismasi huwakutanisha familia na majirani kushirikiana chakula na shughuli mbalimbali, hali inayochangia pia kuimarisha uhusiano na kupunguza migawanyiko ya watu.

Ameeleza kuwa viongozi wa dini na jamii wamekuwa wakiwahimiza wananchi kuendeleza maadili ya maisha ya Krismasi hata nje ya muktadha wa kidini, kwa lengo la kujenga jamii inayojali utu wa kila mmoja, inayothamini amani na kuweka mbele ustawi wa wote.

Akizungumzia hilo, Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT) Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza, amesema sherehe za Krismasi zimekuwa za muda mfupi na mara nyingi hujaa maigizo badala ya kuakisi uhalisia wa maisha ya kila siku.

Amesema kipindi hicho kimekuwa kikitumiwa na watu kualika wenzao kula pamoja na kusahau tofauti zao, lakini hali hiyo hudumu kwa muda mfupi na baada ya sikukuu hizo, chuki na migawanyiko hurudi kama ilivyokuwa awali.

Amesema Krismasi inapaswa kuwa somo la kujitoa, kujali na kuishi katika upendo endelevu, badala ya kuwa tukio la muda mfupi linaloisha bila kuleta mabadiliko ya kweli katika maisha ya watu.

“Nafikiri tungeangalia maadili baada ya Krismasi, si wakati wa Krismasi, kwa sababu kila mtu anakuwa kama mwigizaji, anavaa nguo nzuri ilhali siku nyingine anavaa matambara, anapika wali wakati siku zote anakula ugali,” amesema Askofu Bagonza.

Ameongeza kuwa baadhi ya watu hujitahidi kupamba nyumba zao wakati wa Krismasi ilhali siku nyingine nyumba hizo hubaki katika hali ya kawaida.

Pia amesema wapo waumini wanaokwenda kanisani na kutoa sadaka kubwa siku ya Krismasi, wakati tangu Januari hawakuwa wakishiriki ibada za Jumapili wala jumuiya.

“Anaenda Krismasi na anatoa sadaka yote ambayo angeitoa tangu Januari. Kwa nini hakuwa anakuja? Viongozi wa Serikali wanatoa mchele na mafuta kwa watoto yatima na wasiojiweza, kabla ya Krismasi walikuwa wanakula wapi?” amehoji.

Kwa mujibu wa Askofu Bagonza, Krismasi imegeuka kuwa sikukuu ya maigizo zaidi kuliko uhalisia wake, akitolea mfano matangazo ya punguzo la bei ya bidhaa mbalimbali, huku akijiuliza kwa nini punguzo hilo haliendelezwi siku nyingine za mwaka.

“Kwangu natamani kuona maisha baada ya Krismasi, si Krismasi yenyewe, kwa sababu imekuwa ya kuigiza zaidi kuliko uhalisia wake,” amesema Bagonza.

Askofu huyo amewahimiza waumini na Watanzania kwa ujumla kuishi maadili ya Krismasi kwa mwaka mzima ili sikukuu hiyo iwe na maana ya kweli katika kujenga jamii yenye upendo, mshikamano na haki.

Mtaalamu wa saikolojia, Charles Kalungu, amesema licha ya Krismasi kuwa sikukuu ya kidini, kwa upande wa kijamii husherehekewa kwa namna mbalimbali, ikiwemo kupika vyakula maalumu, kufanya matembezi na kukaa pamoja na familia.

Amesema Krismasi ni miongoni mwa siku zilizotengwa mahsusi kwa watu kukutana na kuimarisha mshikamano wa kifamilia.

Ameeleza kuwa siku ya kwanza Wakristo huenda kanisani kwa ibada, kisha hufuata muda wa kula na kusherehekea pamoja.

Kalungu ameongeza kuwa baada ya Krismasi hufuata Siku ya Boxing Day, ambayo kwa mujibu wa desturi hutumika kutoa zawadi za ghafla zisizopangwa awali, akisisitiza kuwa sikukuu hiyo ni siku ya baraka na furaha kwa jamii nzima.

Amesema Krismasi ni ukumbusho kwa waumini kuimarisha imani zao na kuzaliwa upya katika Kristo, ingawa kila familia ina namna yake ya kusherehekea.

Kalungu ameongeza kuwa kadri miaka inavyosonga, utaratibu wa sherehe hubadilika, hususan katika upishi wa vyakula na mapambo, hali inayotokana na ugumu wa hali ya kiuchumi.

“Siku hizi upikaji wa vyakula na hata mapambo yamebadilika. Zamani ilipokaribia Krismasi, maeneo mengi yalipambwa, lakini kwa sasa ugumu wa maisha umechangia kupunguza shamrashamra hizo,” amesema.

Pia amesema kuwa awali watu walikuwa wakisafiri kwa wingi kwenda kuwatembelea ndugu na jamaa, jambo lililosaidia kuimarisha umoja, lakini utamaduni huo umeanza kupungua.

Kalungu amesema kuwa mabadiliko ya kijamii, utandawazi na maendeleo yamechangia kupungua kwa uzito wa maadhimisho ya sikukuu hiyo, hali inayofanya baadhi ya watu kutoipa kipaumbele kama ilivyokuwa zamani.

Ametoa wito kwa jamii kuendelea kuthamini na kufanya mambo muhimu yenye kuimarisha mshikamano, imani na maadili wakati wa sikukuu za Krismasi.