Ouma matumaini kibao Mapinduzi 2026

KOCHA msaidizi wa Singida Black Stars, David Ouma amesema michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 wanaibeba kwa ukubwa kwa kuitumia kwa ajili ya kuiweka timu katika ubora tayari kwa michuano ya kimataifa.

Singida BS ni kati ya timu 10 zitakazoshiriki michuano hiyo ya Mapinduzi itakayoanza Desemba 28 na kufikia tamati Januari 13 mwakani, huku ikiwa ni timu ambayo itacheza mechi ya ufunguzi dhidi ya watetezi Mlandege inayolishikilia taji hilo kwa misimu miwili mfululizo.

Akizungumza na Mwanaspoti, Ouma amesema ni michuano mikubwa na yenye faida kubwa, hasa kipindi hiki ambacho timu nyingi zipo mapumziko kupisha fainali ya Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) 2025 iliyoanza huko Morocco.

“Hakuna mashindano tunayoshiriki hatuyapi kipaumbele. Kwetu ni fursa nzuri kuwa sehemu ya timu zitakazoshiriki Mapinduzi yatakayokuwa na timu nyingi shindani. Yatatusaidia kuiweka timu kwenye nafasi nzuri,” amesema Ouma na kuongeza;

“Timu tayari imeingia kambini na inaendelea na mazoezi. Itasafiri kwenda Zanzibar Desemba 26 tayari kwa ajili ya michuano hiyo ikitaka kufikia rekodi ya msimu uliopia kwa kucheza fainali na ikiwezekana safari hii tubebe ubingwa kwa mara ya kwanza.”

Ouma amesema michuano hiyo wameipa kipaumbele kwa malengo matatu kutwaa taji, kujenga utimamu wa mwili kwa wachezaji kabla ya kurudi kwa ligi lakini michuano ya kimataifa wakiiwakilisha nchi Kombe la Shirikisho Afrika.

“Wachezaji wote ambao hawajaitwa timu za taifa watakuwa sehemu ya kikosi kitakachokwenda Zanzibar tayari kwa michuano hiyo na malengo ni kurudi na taji baada ya msimu uliopita kushindwa dhidi ya Mlandege.”