::::::
Serikali imesema itaendelea kuwekeza katika utekelezaji wa shughuli za maendeleo na kutoa fursa za kiuchumi na kijamii kwa makundi maalum, yakiwemo wanawake, vijana, watoto, wazee na wafanyabiashara ndogondogo, ili kujenga Taifa jumuishi lenye ustawi na haki.
Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum, Dkt. Dorothy Gwajima, wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa mipango ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2025/26 chini ya uongozi wa Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan.
Dkt. Gwajima amesema Serikali imejikita kuwekeza katika sekta zinazoajiri watu wengi zikiwemo kilimo, utalii, viwanda, ujenzi, michezo, sanaa za ubunifu na madini, kwa lengo la kuongeza ajira na kipato kwa makundi maalum.
Amesema katika kuimarisha malezi na ustawi wa watoto, Serikali inaendelea kushirikiana na wadau kutoa elimu kwa wazazi na walezi kuhusu malezi bora kupitia mwongozo wa wajibu wa wazazi, huku akisisitiza ushiriki wa baba na mama kwa pamoja.
Kwa mujibu wa Waziri huyo, hatua hizo zinalenga kuhakikisha ukuaji bora wa watoto kimwili, kiakili na kisaikolojia pamoja na kuzuia changamoto za kijamii zinazoweza kujitokeza baadaye maishani.
Aidha, amesema Serikali imechukua hatua za makusudi kulinda na kutunza wazee na wasiojiweza, ikiwemo kuwapatia mamilioni ya wazee vitambulisho vya matibabu na bima ya afya bila malipo, pamoja na kuendesha Makazi ya Wazee 13 nchini.
Kwa upande wa usawa wa kijinsia na ustawi wa jamii, Dkt. Gwajima amesema Serikali imeendelea kuweka mazingira rafiki kwa wanawake kushiriki katika uongozi, kuimarisha uwezeshaji wa kiuchumi na kushirikiana na Mashirika Yasiyo ya Kiserikali kupambana na ukatili wa kijinsia.







