Moshi/Dar. Hali Hali ya ukame wa abiria uliokuwa ukionekana katika Kituo Kikuu cha Mabasi cha Magufuli katika siku za hivi karibuni imebadilika baada ya ongezeko la wasafiri kuelekea sikukuu za Krismasi na Mwaka Mpya.
Kutokana na hali hiyo, Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri Ardhini (Latra) imetoa vibali vya muda kwa ajili ya kusaidia kuongeza upatikanaji wa usafiri, huku Shirika la Reli Tanzania (TRC) likiongeza treni moja ya abiria.
Hali ilivyo Dar es Salaam
Jijini Dar es Salaam, siku chache kabla ya Krismasi, hali ya usafiri katika kituo cha Magufuli imeelezwa kuwa nzuri, licha ya mabasi mengi yanayoelekea mikoa ya Kaskazini kuondoka yakiwa yamejaa abiria.
Mmiliki wa mabasi ya RN Express, Nelson Kimaro amesema tangu Desemba 21, 2025 kumekuwa na ongezeko kubwa la abiria, hali inayofanya upatikanaji wa mabasi kuwa mgumu katika baadhi ya safari.
“Ukifika stendi ukaulizia gari la kwenda Arusha au Kilimanjaro, utakuta mengi yamejaa,” amesema.
Amesema hali hiyo ni tofauti na ilivyokuwa kati ya Desemba 10 na 19, kulikuwa na uhaba wa abiria uliosababisha biashara ya usafiri kuwa ngumu.
“Mabasi yalikuwa yanaondoka na abiria 20 au 30 tu. Kipindi hicho ndipo nauli zilikuwa zinashuka,” amesema.
Kwa mujibu wa Kimaro, kwa sasa nauli zimebaki katika viwango vya kawaida, zikianzia Sh42,000 kwa mabasi ya kawaida na kufikia Sh60,000 kwa mabasi ya daraja la VIP, kutegemeana na aina ya huduma.
Hata hivyo, katika kukabiliana na changamoto ya usafiri, Mamlaka ya Udhibiti Usafiri Ardhini (Latra) imesema hadi Desemba 20, 2025 ilitoa vibali 252 vya muda kwa ajili ya kusaidia kuongeza upatikanaji wa usafiri.
Mkurugenzi Mkuu wa Latra, Habibu Suluo amesema kati ya Desemba mosi na Desemba 20, 2025, jumla ya tiketi milioni 1.978 ziliuzwa, huku nauli zilizolipwa zikifikia Sh71.347 bilioni.
Hata hivyo, changamoto bado zinaendelea kuwepo. Dereva wa gari la ‘special hire’, Shaaban Nguruka, amesema kuanzia Desemba 20 wanapata abiria wengi, hususan wanaoelekea mikoa ya Kaskazini.
Amesema nauli kwa safari hizo hufikia hadi Sh55,000, akieleza kuwa hulazimika kufidia gharama za safari ya kurudi ambayo mara nyingi huwa na abiria wachache.
Baadhi ya wasafiri wanaoelekea Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro wakisubiri usafiri leo Desemba 22, 2025 katika Stendi Ndogo ya Mabasi Moshi Mjini. Picha na Omben Daniel
Akizungumza na Mwananchi leo Jumatatu Desemba 25, 2025 kuhusu hatua zilizochukuliwa na TRC, Mkuu wa Kitengo cha Uhusiano na Mawasiliano cha shirika hilo, Fredy Mwanjala amesema ongezeko la mahitaji ya usafiri kuelekea sikukuu hizo limewalazimu kuongeza treni moja ya abiria kutoka Dar es Salaam kuelekea mikoa ya Kaskazini.
Amesema kwa upande wa reli ya kisasa (MGR), ratiba ya kawaida ya safari za kuelekea Arusha na Moshi ni kila Jumatatu na Ijumaa, na treni huondoka saa nane mchana.
Hata hivyo, kuanzia sasa hadi Januari 2026, amesema TRC imeongeza treni nyingine itakayokuwa ikifanya safari kila Jumamosi.
“Tumelazimika kuongeza treni moja nzima ambayo itakuwa inaondoka saa nane mchana kila Jumamosi hadi Januari 2026. Lengo ni kuhakikisha tunawahudumia Watanzania wanaosafiri kwenda mikoa ya Kaskazini kwa ajili ya sherehe za Krismasi na Mwaka mpya bila shida,” amesema Mwanjala.
Ameongeza kuwa uamuzi huo umezingatia makundi mbalimbali ya wasafiri, wakiwamo watumishi wa umma na wanafunzi wanaosafiri wakati wa likizo na kurejea kazini au shuleni ifikapo Januari.
Kwa upande wa reli ya kati inayounganisha Dar es Salaam na Kigoma, Mwanjala amesema TRC imeongeza idadi ya mabehewa kutoka 16 ya kawaida hadi 20, baada ya kukarabati mabehewa manne ya ziada.
“Katika kipindi hiki cha kuelekea sikukuu za Krismasi na Mwaka mpya, tutatumia mabehewa 20 badala ya 16. Hatua hii inalenga kubeba abiria wengi zaidi na kupunguza msongamano,” amesema.
Baadhi ya wasafiri wanaoelekea Wilaya ya Rombo, mkoani Kilimanjaro wakisubiri usafiri leo Desemba 22, 2025 katika Stendi Ndogo ya Mabasi Moshi Mjini. Picha na Omben Daniel
Hali ya msongamano wa watu na magari imeonekana pia katika Mkoa wa Kilimanjaro, hususan katika Manispaa ya Moshi.
Uchunguzi wa Mwananchi umebaini katika nyakati za mchana na jioni, maeneo ya katikati ya mji wa Moshi kumekuwa na msongamano mkubwa wa watu na magari hali inayosababisha foleni ndefu barabarani.
Mkazi wa Moshi, Ebenezer Swai akizungumzia hilo amesema hali hiyo ni ya kawaida kila unapofika msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka.
“Kipindi hiki, mji wa Moshi hufurika watu. Magari ni mengi, watu pia ni wengi, na wengine wanaegesha magari barabarani kwa sababu hakuna maeneo ya kutosha,” amesema.
Kwa upande wa usafiri wa ndani, abiria anayesafiri kutoka Moshi kwenda Wilaya ya Rombo, Anna Shayo amesema ongezeko la watu limesababisha magari mengi kujaa mapema, hivyo abiria kulazimika kusubiri kwa muda mrefu.
“Magari ni machache na watu ni wengi, wakati mwingine tunasubiri gari kwa muda mrefu kabla ya kupata nafasi,” amesema.
