Kwa Jina la Mwenyezi Mungu (Allah S.W.T), Mwingi wa Rehema, Mwenye Kurehemu
Yeye ndiye Muumba wa mbingu na ardhi na vyote vilivyomo.
Humpa ufalme amtakaye na humwondolea amtakaye, humruzuku amtakaye bila ya hisabu na huwakadiria wengine riziki zao kwa hikima Yake. Yeye pekee ndiye anayestahili kuabudiwa, kutegemewa, kushukuriwa na kuombwa msaada katika kila jambo.
UTANGULIZI
Swali kuu kwa Watanzania wote ni: Nini kifanyike ili kuliponya Taifa letu? Waraka huu wa pili wa Umoja wa Kiislamu Tanzania (UWAKITA) unalenga kutoa mwongozo, ushauri na ufafanuzi wa kisheria na kikatiba kuhusu yaliyotokea kabla na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Tanzania wa tarehe 29 Oktoba 2025, pamoja na jaribio la maandamano ya tarehe 9 Disemba 2025.
1. MSINGI WA WARAKA
Lengo kuu la waraka huu ni kuwashirikisha Watanzania wote kujadili kwa busara swali la msingi: Ni bora kuipinga au kuiunga mkono Serikali halali kwa maslahi ya Taifa, amani na ustawi wa nchi?
Baada ya Uchaguzi Mkuu, kumekuwepo vitendo, matamko na vuguvugu lililotikisa misingi ya amani ya Taifa, likichochewa na fitna na unafiki wa kisiasa, ikiwemo matishio na jaribio la maandamano yaliyoshindikana tarehe 9 Disemba 2025.
2. FITNA NA UNAFIKI WA KISIASA
Kabla na baada ya matukio ya tarehe 29 Oktoba na 9 Disemba 2025, kumekuwepo mtazamo potofu unaodai kuwa:
• Kuunga mkono Serikali na chama tawala ni “uchawa” au ukada;
• Kuipinga Serikali ndiyo kigezo pekee cha uzalendo wa kweli.
Mtazamo huu ni hatari, unakiuka misingi ya demokrasia na uhuru wa mawazo, na unapaswa kupingwa kwa nguvu zote za kimaadili na kisheria.
3. ATHARI ZA FITNA ZA KISIASA
Hatupaswi kuruhusu fitna hizi kuendelea kupandikizwa katika jamii, kwani zinaweza:
• Kuzalisha chuki za kisiasa;
• Kugawa wananchi kwa misingi ya kikanda, kidini au kikabila;
• Kuhatarisha mshikamano wa Taifa.
Mfano hai ni madhara yaliyowakumba baadhi ya wafanyabiashara, wasanii na wananchi wengine wakati wa machafuko ya tarehe 29 Oktoba 2025.
4. KUPINGA SERIKALI NA ATHARI ZA KISHERIA
Kwa mujibu wa Katiba na sheria za nchi, kuipinga Serikali kwa njia ya maandamano yasiyo halali, yanayosababisha vurugu, uharibifu wa mali za umma na binafsi, uchomaji moto na matamko ya kumlazimisha Rais aondoke madarakani nje ya mchakato wa uchaguzi, ni vitendo vinavyoweza kufasiriwa kama makosa ya jinai au hata uhaini.
5. HISTORIA YA MALALAMIKO KATIKA SERIKALI ZOTE
Tangu awamu ya kwanza hadi ya sita ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, hakujawahi kukosekana malalamiko ya kijamii kutoka kwa makundi mbalimbali, ikiwemo viongozi wa dini, wanasiasa, wafanyakazi, wafanyabiashara, wakulima na wafugaji.
Matukio kama Zanzibar 2001, Mwembechai, Kibiti, Kilindi, Handeni na machafuko ya Oktoba 29, 2025 yote ni ushahidi kuwa maumivu ya wananchi hayajawahi kuwa ya awamu moja pekee.
6. UDHAIFU WA SERIKALI NI HALI YA KIBINADAMU
Serikali zote za wanadamu huwa na mapungufu. Kuanza kulinganisha awamu kwa misingi ya chuki za kidini, kikabila, kikanda au kisiasa kunaweza kuvunja mshikamano wa Taifa na kuibua uadui hatari.
7. WAJIBU WA KULIPONYA TAIFA
Njia pekee ya kuziba nyufa na kutibu majeraha ya Taifa ni:
• Kulinda amani;
• Kudumisha umoja wa kitaifa;
• Kukataa kuwa sehemu ya chanzo cha migawanyiko na vurugu.
Kila Mtanzania ana wajibu wa kimaadili na kitaifa wa kulinda mshikamano wa nchi.
8. KUSIKILIZA MAONI NA MALALAMIKO
Tunashauri viongozi na wananchi wasipuuze maoni na malalamiko ya wananchi. Kila hoja inapaswa kusikilizwa kwa umakini na kujibiwa kwa nia njema, hasa katika kipindi hiki cha kutafuta maridhiano ya kitaifa.
9. MSAMAHA NA MARIDHIANO
Kama kweli dhamira ni kuliponya Taifa, basi kulaumiana si suluhisho. Njia bora ni kusameheana, kujadili chanzo cha matatizo na kutafuta suluhu ya kudumu.
10. MDAI NA NJIA ZA KISHERIA
Kudai haki kwa kutumia nguvu, kuwahamasisha wananchi kuvunja sheria na kujichukulia sheria mkononi ni kinyume na Katiba. Waislamu na Watanzania wengine wamekuwa na madai halali kwa miaka mingi, lakini hawakuwahi kuchagua njia ya vurugu kama ilivyotokea Oktoba 29 na jaribio la Disemba 9.
11. MSIMAMO WA SERIKALI NA ULINZI WA AMANI
Serikali ina wajibu wa kulinda raia na mali zao. Pale maandamano yanapogeuka kuwa vurugu, uporaji na uharibifu wa mali, vyombo vya ulinzi hulazimika kuchukua hatua za kisheria.
12. KUEPUKA KULAUMIANA
Hakuna upande unaopaswa kubebeshwa lawama zote. Funzo kubwa ni kujifunza subira, busara na kuheshimu sheria.
13. USHAURI KWA JUMUIYA ZA KIKANDA NA KIMATAIFA
Tunazikumbusha jumuiya za kikanda na kimataifa kuwa Tanzania ni Taifa huru lenye Katiba, sheria na tamaduni zake. Ushauri wowote unapaswa kuheshimu misingi hiyo na kuhimiza utekelezaji wa wajibu wa kikatiba kabla ya kudai haki.
14. HATARI YA KUJICHUKULIA SHERIA MKONONI
Kuhamasisha watu wasipige kura au kuvuruga uchaguzi kwa njia ya vurugu ni kitendo cha kihalifu na cha kuhujumu maslahi ya Taifa, kama ilivyoshuhudiwa Oktoba 29, 2025.
15. HALALI YA SHERIA NA KATIBA
Hata kama Katiba au sheria zina mapungufu, bado zina uhalali wa kisheria hadi zitakapobadilishwa kwa utaratibu uliowekwa. Hakuna haki ya kuvunja sheria kwa kisingizio cha kudai haki.
16. KUEPUKA KUTUMIWA KISIASA
Watanzania waepuke kutumiwa na watu wachache wenye nia ya kuvuruga amani ya nchi kwa maslahi binafsi au ya kisiasa.
17. MABADILIKO YA KISHERIA
Mabadiliko ya Katiba na sheria hayapatikani kwa nguvu au vurugu, bali kwa njia za kisheria, maridhiano na ridhaa ya Watanzania wote.
18. UFAFANUZI WA KIKATIBA
Katiba ya Tanzania, hasa Ibara ya 26, 29 na 30, inaweka wazi wajibu wa kila raia kutii sheria na kuheshimu mamlaka halali za nchi.
19. WITO WA MWISHO
Tunawaomba Waislamu na Watanzania wote kwa maslahi ya Taifa kuepuka maandamano na vitendo vya kuvunja sheria, kama ilivyokuwa Oktoba 29 na Disemba 9, 2025.
HITIMISHO
Tunatoa pole kwa waathirika wote wa matukio ya tarehe 29 Oktoba 2025. Kwa nia njema, tunaunga mkono juhudi za Mheshimiwa Rais za kuimarisha maridhiano ya kitaifa, ikiwemo:
• Kuundwa kwa Tume ya Maridhiano;
• Maboresho ya Katiba;
• Tume Huru ya Uchaguzi;
• Msamaha kwa waliohusika kwa kufuata taratibu za kisheria.
Tunawaomba Watanzania kumuunga mkono Mheshimiwa Rais na Serikali yake katika juhudi zote njema za kutafuta suluhu ya migogoro ya kitaifa.
Mungu ibariki Tanzania, Afrika na Dunia. Atudumishe katika amani, upendo, umoja na mshikamano wa haki na kweli.
Imetolewa na:
Mussa Ally Chengula
Mwenyekiti wa Umoja wa Kiislamu Tanzania (UWAKITA) – Taifa
Tarehe: 22 Disemba 2025.
Kutoka kushoto. Katibu Mkuu wa Uwakita Ramadhani Mhando, Mwenyekiti Uwakita Wakili Mussa Chengula, Harubu Othuman Mkurugenzi wa Dini Taifa na Sheikh mselemu Ali mfasiri maarufu wa Qur’an tukufu Afrika Mashariki walipokutana hivi karibuni katika ufunguzi rasmi wa ofisi ya UWAKITA Makao Makuu jijini Dar es Salaam
