Dar es Salaam. Wananchi wa Mtaa wa Shimo la Udongo Kata ya Kurasini wilayani Temeke, waliokuwa wamezika ndugu zao katika makaburi ya Bongulo wameanza kulipwa fedha kwa ajili ya kuhamishwa huku udanganyifu ukitawala.
Makaburi hayo zaidi ya 4,000 yatahamishwa kupishwa ujenzi wa bandari kavu inayojengwa na mwekezaji, huku kila moja likilipwa Sh300,000.
Hatua hiyo inakuja ikiwa imepita mwaka mmoja tangu kufanyika kwa kikao kati ya mwekezaji na wananchi kuwaeleza nia ya kuchukua eneo hilo, ambacho kilivurugika baada ya baadhi kugomea kupesa rambirambi ya Sh200,000 waliyoambiwa watalipwa kwa kila kaburi huku wenyewe walitaka kulipwa Sh2 milioni.
Kutokana na mgomo huo, mwekezaji alisema ataongeza iwe Sh300,000 fedha ambayo pia waliigomea hadi kikao kulazimika kuahirishwa bila ya muafaka.
Baadhi ya wananchi waliofika Mtaa wa Shimo la Udongo Kata ya Kurasini wilayani Temeke wakionyesha maeneo yalipo makaburi ya ndugu zao leo Jumatatu Desemba 22, 2025.
Hata hivyo, siku chache baadaye wananchi wengi walifika ofisi ya Mtendaji Kata na kutaka walipwe kiasi hichohicho kilichoamuliwa na mwekezaji, na wengine kufikia hatua ya kwenda kulalamika halmashauri kuchelewa kulipwa fedha hizo.
Leo Desemba 22,2025 Mwananchi imeshuhudia shughuli ya ulipaji fidia ikiendelea kwa wafiwa pembezoni mwa makaburi hayo, ambayo eneo lake lilikuwa limezungushiwa uzio na walikuwa wakipewa pesa taslimu kulingana na idadi ya makaburi mtu aliyokuwa nayo.
Akizungumza na Mwananchi Mwenyekiti wa Mtaa wa Shimo la Udongo, Stanley Lima, aliyekuwa akisimamia shughuli hiyo amesema ulipaji fidia huo ilianza tangu Alhamisi ya juma lililopita leo ikiwa ni awamu ya pili ambapo mpaka sasa tayari watu 2,000 wameshalipwa fedha zao.
Hata hivyo amesema wamekumbana na changamoto mbalimbali katika utekelezaji wake ikiwemo mtu mmoja kujitokeza na kusema ana makaburi 27 na mwingine kusema anayo ya ghorofa saba kwenda chini.
Ulipaji fidia ukiwa unafanyika kwa baadhi ya ndugu leo Jumatatu Desemba 22, 2025.
Pamoja na kuwasikiliza watu hao, Lima amesema baadhi wameshindwa kuyatambua makaburi yao yalipo huku wengine wakishindwa kuonyesha idadi ya waliyoyataja.
“Kuna ambao wanasema wana makaburi 27,lakini ukiwaambia waonyesha hata sita hayafiki. na mwingine akiona zoezi limekuwa gumu kutambua makaburi ya ndugu zake aliyoyasema yapo, anaonyesha ya wengine na hivyo kuleta mgongano kwa waliostahili kulipwa,”amesema Lima.
Changamoto nyingine walioibaini amesema kuna muhtasari imeandikwa zaidi ya 60 huku mwandiko ukionekana ni wa mtu mmoja na kuonyesha wazi kuwa kuna janjajanja zinafanyika ili kupata fedha hizo.
Wakati mwisho wa kuwasilisha muhtasari ulikuwa Agosti,2025, Lima amesema ajabu walipoanza kulipa, wengine ndio wanaleta muhtasari wao.
Vilevile amesema katika shughuli hiyo pia ndugu wenyewe wanazungukana kila mmoja anaenda na nyaraka zake kudai na wote wakiwa na nyaraka sahihi
“Katika kushughulikia hili endapo inatokea kuna aliyelipwa halafu akaja ndugu mwingine kulalamika huwa tukiwaonyesha picha na kitambulisho chake kujua wanawatambua au la,”ameeleza Lima.
Moja ya vigezo ili upewe pesa ni lazima uende na Kitambulisho cha uraia, leseni ya udereva na barua ya utambulisho kutoka kwa mwenyekiti wa serikali ya mtaa.
Kwa upande wake Mwakilishi wa mwekezaji, Mohammed Kamilagasa, amesema hadi kufikia leo tayari wameshalipa Sh500 milioni kwa zaidi ya watu 2,000.
Kamilagasa pia likiri uwepo wa changamoto zilizoelezwa na Lima na kueleza katika hilo watu saba walikamatwa na kunyang’anywa fedha lakini baadaye waliamua kuwasamehe.
Hata hivyo katika shughuli inayoendelea leo ambayo itafika tamati Desemba 24 amesema watakaobainika kufanya utapeli huo hatua kali zitachukuliwa dhidi yao ikiwemo kutakiwa kulipa gharama zote sio tu hela walizochukua, bali hadi kesi hizo zitakavyoendeshwa na usumbufu waliowapatia.
Kwa upande wao wananchi akiwemo Theodesia Nkunda, amesema alifika hapo leo asubuhi na kuliona kaburi la mama yake, lakini baada ya kutoka nje kwenda sehemu wanapotolea malipo akaambiwa limeshalipwa.
“Baada ya kupewa majibu hayo ilibidi tena nirudi kuliangalia, kweli nikakuta limetikiwa lakini nashukuru kwa kuwa nina nyaraka zote, mwakilishi wa mwekezaji alinielewa ila kiukweli watu hawana ubinadamu wanadanganya hadi kwenye makaburi kisa pesa,”amesema Theodesia.
Abdulrahaman Mninga, katika shughuli hiyo amesema amelipwa fedha ya makaburi manne na kueleza japo ni ndogo lakini wanashukuru hata kwa sadaka hiyo.
Ukiacha ulipaji wa fidia mwekezaji huyo eneo lingine tayari ameshaanza kufanya ujenzi wa bandari hiyo, ambayo kulikuwa na magari maalumu yaliyokuwa yakichimba, kuzoa na kusambaza udongo na eneo lote tayari limezungushiwa uzio.
Akieleza sababu ya kuendelea na ujenzi, amesema ni kwa kuwa eneo la makaburi ni dogo ukilinganisha na lililobaki hivyo wakaona lisiwacheleweshe.
Eneo lote lililochukuliwa na mwekezaji huyo lina heka 8.6 kati ya hizo mbili ndio zilikuwa za makaburi.
