JESHI la Polisi Mkoa wa Mbeya linamshikilia Furaha Mwile Nyelele, mkazi wa Kijiji cha Shilanga kwa tuhuma za mauaji ya mtoto wa jirani yake aliyekuwa Mwanafunzi wa Shule ya Msingi Shilanga darasa la saba aitwaye Boniventure Elia Lazaro [12] mkazi wa Shilanga.
Awali kabla ya tukio hilo tarehe 21.12.2025 saa 10:15 jioni huko Kijiji cha Shilanga, Kata ya Ilembo, Tarafa ya Isangati, Wilaya ya Mbeya Vijijini mtuhumiwa Furaha Mwile Nyelele alimpiga kwa kipande cha mti kichwani mtoto Boniventure Elia Lazaro [12] ambaye kwa sasa ni marehemu na kumsababishia jeraha ambapo alikimbizwa katika Hospitali Teule ya Ifisi kwa matibabu.
Tarehe 22.12.2025 saa 6:30 mchana akiwa anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali Teule ya Ifisi alifariki dunia. Uchunguzi wa awali umebaini kuwa chanzo cha tukio hili ni kujichukulia sheria mkononi baada ya mtuhumiwa kumtuhumu mtoto kuiba mayai ya kuku.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linatoa kwa jamii kuacha tabia ya kujichukulia sheria mkononi ili kuepuka madhara. Aidha, wazazi na walezi wanakumbushwa kuzingatia suala la ulinzi na usalama wa mtoto kwa kuhakikisha haki za mtoto zinaheshimiwa na kulindwa.
Imetolewa na:
Kamanda wa Polisi,
Mkoa wa Mbeya.