Karagwe. Askofu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Dayosisi ya Karagwe, Dk Benson Bagonza, amesema kuwa Mungu bado ndiye tumaini la pekee la kweli kwa kanisa na Taifa.
Amewahimiza waumini pamoja na Watanzania kwa ujumla kuacha kuwaweka matumaini yao kwa wanadamu na mifumo ya kidunia, ambayo imeendelea kukatisha tamaa na kuondoa amani katika jamii.
Akitoa salamu za Noel ya 2025 na heri ya mwaka mpya wa 2026, Askofu Bagonza amesema jamii ya sasa inaishi katika mazingira ya hofu, kukosa amani na kupoteza matumaini, hali inayofanana na kipindi cha kabla ya kuzaliwa kwa Yesu Kristo.
Askofu huyo amesema fedha, silaha, vyeo, umaarufu na mitandao ya mahusiano havijaweza kutoa uhakika wa usalama na amani ya kweli, jambo linaloifanya jamii kutamani kupata cha kuamini bila kusalitiwa.
Akinukuu maandiko mtakatifu kitabu cha Yeremia 29:11, Askofu Bagonza amesema Mungu anawawazia watu wake mema, ya amani na ustawi wa baadaye, na anastahili kuaminiwa licha ya changamoto na majeraha ya kijamii yaliyopo.
“Tumefika mahali ambapo kuamini kumekuwa kugumu, lakini Mungu hajawaacha watu wake, yuko pamoja nasi katika hali zote,” amesema.
Akieleza maana ya Noel, Askofu Bagonza amesema kuzaliwa kwa Yesu Kristo kulikuja katikati ya giza la hofu na kukata tamaa, na kurejesha tumaini jipya kwa wanadamu.
“Yesu Kristo ndiye mfalme wa amani, kuzaliwa kwake kulirejesha imani kwa Mungu aliyekuwa ameonekana kana kwamba amenyamaza,” amesema.
Askofu huyo amewahimiza waumini kumwamini Mungu na kumtegemea yeye pekee, akisema kuendelea kuwaamini wanadamu na mifumo kumeleta maumivu makubwa katika maisha ya wengi.
Kwa upande wa Taifa, Askofu Bagonza amesema Mungu analipenda Taifa la Tanzania na bado analifikiria kwa mawazo ya amani na maendeleo, akisisitiza kuwa hakuna mwingine anayelilinda zaidi ya Mungu.
“Ninyi mtanyamaza kimya na Bwana atawaletea ushindi,” amesema akinukuu Kutoka 14:14.
Amehimiza Watanzania kuliombea Taifa, kudumisha upendo na mshikamano, na kuishi kwa misingi ya imani, akisisitiza ndani ya Mungu bado kuna tumaini.
Askofu Bagonza amehitimisha ujumbe wake kwa kuwatakia waumini na Watanzania wote Noel njema ya 2025 na mwaka mpya wa 2026 uliojaa baraka kuliko balaa.
