Dakika mbili zaitibulia Stars dhidi ya Nigeria, AFCON 2025

Ni dakika mbili tu zilizoyeyusha uwezekano wa Taifa Stars kuishtua Afrika kwa kutoka sare na Nigeria katika mchezo wa Fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) 2025 uliochezwa kwenye Uwanja wa FES, Morocco leo.

Stars ilishindwa kulinda bao la kusawazisha ililopata kwenye mchezo huo kupitia Charles M’Mombwa katika dakika ya 50 na kuiruhusu Nigeria kuongeza bao la pili katika dakika ya 52 ambalo liliamua mchezo huo.

Nigeria ilianza kutangulia kupata bao katika mechi hiyo kupitia kwa Semi Ajayi aliyeunganisha vyema kwa kichwa krosi ya Alex Iwobi katika dakika ya 36.

Lakini dakika tano baada ya filimbi ya kuanza kipindi cha pili kupulizwa, M’mombwa aliipachikia Taifa Stars bao la kusawazisha kwa shuti la wastani la mguu wa kulia akimalizia pasi ya Novatus Miroshi.

Kwa kupachika bao hilo, M’Mombwa anakuwa ameifungia Taifa Stars mabao mawili katika mechi mbili mfululizo rasmi tangu ilipoanza kunolewa na Miguel Gamondi.

Hata hivyo shuti kali la mguu wa kulia la Ademola Lookman katika dakika ya 52, liliipa Nigeria bao la pili na la ushindi kwao ikiendeleza rekodi nzuri ya ushindi iliyonayo dhidi ya Taifa Stars.

Hiyo ni mechi ya nane kwa Nigeria kutopoteza mbele ya Taifa Stars ambapo imepata ushindi katika michezo mitano na kutoka sare tatu.

Katika mchezo huo, Refa Beida Dahane kutoka Mauritania alitoa kadi moja tu ya njano ambayo ilienda kwa Ademola Lookman kwa kosa la kumchezea rafu M’mombwa.

Stars imeendeleza rekodi yake isiyovutia ya kutopata ushindi katika AFCON ambapo mchezo wa leo ulikuwa wa 10 kwake kucheza bila kushinda katika mara nne tofauti ilizocheza fainali hizo.