Dosari zamweka huru aliyedaiwa kusafirisha kilo 172.3 za bangi

Arusha. Mahakama Kuu Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, Masjala Ndogo ya Musoma, imemwachia huru Miriam Usire, aliyeshtakiwa kwa kosa la kusafirisha kilo 172.3 za bangi.

Hukumu imetolewa na Jaji Monica Otaru, aliyesema ushahidi uliotolewa na upande wa mashtaka umeshindwa kuhalalisha hatia dhidi ya mshtakiwa kwani unaacha shaka.

Jamhuri ilidai Oktoba 2, 2023, katika Kijiji cha Nkerege, wilayani Tarime mkoani Mara, mshtakiwa alisafirisha dawa hizo kinyume cha sheria.

Ili kuthibitisha shtaka hilo, upande wa Jamhuri uliita mashahidi wanane na kuwasilisha vielelezo tisa. Mshtakiwa aliyekuwa na uwakilishi wa wakili, alikuwa shahidi pekee wa utetezi.

Jamhuri ilieleza operesheni iliyoendeshwa na Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya (DCEA), ilipokea taarifa kuwa katika nyumba ya kulala wageni kijijini hapo kulikuwa na watu wanaouza bangi.

Shahidi wa nne, Inspekta Wamba na shahidi wa kwanza, Anastazia Lawrence, walifika kwenye nyumba hiyo, wakafunguliwa mlango na mhudumu, Damari Daniel, aliyekuwa shahidi wa tano katika kesi hiyo.

Baada ya kujitambulisha, aliwaruhusu kupekua vyumba ili kuwakamata wafanyabiashara waliokuwa wakiwatafuta, ikielezwa katika chumba alichokuwamo mshtakiwa dawa hizo zilipatikana.

Ilidaiwa mahakamani kuwa mshtakiwa alikiri kuhusika katika biashara ya dawa za kulevya na aliwapeleka maofisa hao kwenye vichaka alikokuwa ameficha magunia 14 yenye dawa hizo.

Baada ya magunia hayo kukamatwa na uchunguzi kufanyika ilibainika kuwa ni bangi yenye uzito wa kilo 172.3.

Ilidaiwa kutokana na wingi wa magunia, usafirishaji na uhifadhi wake ulikuwa na changamoto kwa timu, hivyo iliteketezwa lakini kabla ya kufanya hivyo yalipigwa picha na mpigapicha wa DCEA, Lilian Boniphace, ambaye alipiga picha tatu zilizopokewa mahakamani kama vielelezo.

Ilidaiwa mchakato wa kuchoma bangi uliongozwa na Hakimu Mkazi Mwandamizi, Stanley Julius, (shahidi wa pili wa Jamhuri) na kusimamiwa na shahidi wa tatu, Lusako Mwaiseke.

Baada ya uteketezaji, magunia 14 matupu yalihifadhiwa hadi yalipowasilishwa mahakamani kama kielelezo.

Mshtakiwa alikana kutenda kosa hilo akaiomba mahakama imuachie huru, akidai siku ya tukio Oktoba mosi 2023, alikuwa na mume wake, George Usire wakitokea kijijini kwao Kamageta wakielekea Nkerege, kwa ajili ya maziko ya jamaa yao.

Alidai waliamua kulala kwa Matete kutokana na mvua na usafiri kuwa wa shida. Asubuhi waliamshwa na kukamatwa yeye na mume wake wakidaiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya.

Mshtakiwa alidai pamoja na watu wengine waliokuwa wamelala katika nyumba hiyo walipelekwa kwenye vichaka, ambako magunia yalitolewa humo kisha majina yao kuandikwa kwenye magunia hayo kabla ya kilichokuwamo ndani hakijateketezwa.

Alikana kuandika maelezo ya onyo akiwa Kituo cha Polisi Tarime kama ilivyodaiwa mahakamani.

Jaji amesema suala lililopo mahakamani ni kuamua iwapo upande wa mashtaka umethibitisha kesi dhidi ya mshtakiwa bila kuacha shaka yoyote.

Amesema katika kuamua hilo, mahakama imebaini upungufu mkubwa wa kisheria katika mchakato wa uchunguzi na kuharibu vielelezo.

Jaji Otaru amesema upekuzi na ukamataji ulifanywa bila kuwapo shahidi, jambo ambalo ni kinyume cha matakwa ya sheria, hali iliyotia shaka juu ya uhalali wa ushahidi uliotolewa.

“Kwa mujibu wa kifungu cha 48(2) (d)(i) cha Sheria ya DCEA, uwepo wa shahidi huru wakati wa upekuzi na ukamataji ni lazima. Jukumu la shahidi huru ni kulinda na kuhakikisha hakuna upendeleo ila kuwa na haki na uwazi wa uchunguzi,” amesema.

Amesema mahakama imebaini mshtakiwa hakupata haki ya kusikilizwa kabla ya uteketezaji wa dawa hizo za kulevya, jambo linalokiuka taratibu za kisheria na kuathiri uaminifu wa ushahidi wa upande wa mashtaka.

Kutokana na dosari hizo, mahakama imehitimisha kuwa, upande wa mashtaka umeshindwa kuthibitisha kosa bila kuacha shaka yoyote, hivyo kumkuta mshtakiwa hana hatia na kumuachia huru.

“Kwa kuzingatia sababu zilizoelezwa hapo juu, mahakama hii inahitimisha kwamba, upande wa mashtaka umeshindwa kutekeleza jukumu lao la ushahidi na kwamba, uliotolewa hautoshi kuhalalisha hatia dhidi ya mshtakiwa, kwani umejaa mashaka,” amesema.