Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) 2025 zinaendelea nchini Morocco kwa mataifa 24 kushindania ubingwa unaoshikiliwa na Ivory Coast.
Ufunguzi wa fainali hizo ulifanyika Desemba 21, 2025 huku ukiteka hisia za watu wengi si ndani ya Morocco pekee, bali hata waliokuwa mbali wakishuhudia kupitia matangazo ya moja kwa moja yaliyorushwa mubashara na vituo tofauti vya runinga.
Msisimko zaidi wa ufunguzi wa fainali hizo haukusubiri mechi ya kwanza iliyozikutanisha Morocco dhidi ya Comoros, bali mapema tu ilionekana kitu cha kuvutia zaidi pale sherehe zilipoanza kwa burudani za hapa na pale, kisha mgeni rasmi, Mwanamfalme Moulay Hassan ambaye ni mtoto Mfalme Mohammed VI wa Morocco kuchukua nafasi yake.
Mwana mfalme, Moulay Hassan ndiye aliyefungua mashindano hayo kwa kuupiga mpira katika sherehe zilizofanyika kwenye uwanja uliopewa jina lake uliopo kilomita saba kutoka katikati mwa mji mkuu wa Morocco Rabat.
Uwanja wa Michezo wa Moulay Abdellah unasimama kama moja ya kivutio maarufu zaidi nchini humo ambapo dimba hilo la kisasa, hutumika kama kitovu cha michezo huko Rabat.
Licha ya mvua kubwa kunyesha wakati wa tukio hilo, lakini haikumzuia mwana mfalme huyo, kuingia sehemu ya kuchezea mpira kuungana na wageni wengine waalikwa kufanya tukio hilo, ikiwa ni ishara ya ufunguzi.
Ilivutia zaidi pale alipokuwa akisalimiana na wachezaji wa timu zote mbili, akianza kwa Comoros, kisha kwa wenyeji Morocco ambapo alikuwa akitumia muda kidogo kuzungumza na kila mchezaji, huku akipewa salamu ya heshima na vijana wa taifa hilo.
Mwanamfalme Moulay mwenye umri wa miaka 23 alionekana mwenye utulivu, kujiamini na heshima inayostahili hadhi yake ya kifalme, hali iliyowavutia wengi na kuibua mijadala mikubwa kwenye mitandao ya kijamii.
Mwonekano wake wa heshima, utulivu na kujiamini ulimfanya kuwa gumzo kubwa, si tu ndani ya uwanja wa michezo bali pia katika mitandao ya kijamii, picha na video zake zilisambaa kwa kasi, zikimfanya kutawala mitandaoni na kuonekana kama mfano wa kizazi kipya cha viongozi wa Afrika.
Usiyoyajua kuhusu Mwanamfalme Moulay
Ni mtoto wa kwanza wa Mfalme wa Mohamed VI, aliyezaliwa Mei 8, 2013 katika Ikulu ya Kifalme ya Rabat, Morocco akizaliwa katika kipindi kinachotajwa vijana kukutana na teknolojia na dunia ya mtandao ambapo kundi hilo linajulikana Generetion Z au maarufu Gen Z. Moulay alipewa jina la babu yake, aliyekuwa Mfalme wa Morocco (marehemu Hassan II).
Mwanamfalme Moulay El Hassan akiwa kwenye mazungumzo na Rais wa Jamhuri ya Watu wa China, Xi Jinping, wakati alipowasili jijini Casablanca kwa ziara fupi nchini Morocco, Novemba 2024.
Prince Moulay ana dada wake anayeitwa Princess Lalla Khadija aliyezaliwa Februari 28, 2007. Mama yao anaitwa Princec Lalla Salma.
Moulay Hassan ni miongoni mwa viongozi vijana wanaofuatiliwa kwa karibu barani Afrika, alipata elimu yake ya msingi, sekondari ya chini na sekondari ya juu katika Chuo cha Kifalme cha Rabat.
Anajulikana kama mtu mwenye ujuzi wa lugha nyingi, akizungumza Kiarabu, Tamazight (lugha inayozungmzwa Morocco), Kiingereza, Kifaransa na Kihispania, jambo linaloonyesha maandalizi yake kwa majukumu ya kimataifa ya uongozi.
Mwanamfalme huyo ameanza kuandaliwa rasmi kwa majukumu ya uongozi wa taifa, hatua iliyomfanya kushiriki katika hafla mbalimbali za kitaifa na kimataifa tangu mwaka 2013, akiambatana na baba yake au akimwakilisha.
Sambamba na hilo, Moulay Hassan amepewa vyeo vya kijeshi katika vikosi mbalimbali vya ulinzi vya Morocco, ikiwemo Jeshi la Walinzi wa Kifalme, Jeshi la Taifa na Jeshi la Anga.
Mwaka 2025, alipandishwa cheo na kuwa Kanali Meja katika vikosi vya Wanajeshi wa Kifalme wa Morocco.
Mwaka 2020, alipata cheti chake cha kuhitimu elimu ya sekondari kwa ufaulu wa juu kutoka Chuo cha Kifalme, baada ya kufanya mitihani yake katika shule ya Sekondari ya Umma ya Lycée Dar es Salaam mjini Rabat.
Mwanamfalme Moulay Hassan. Picha na Mtandao
Baadaye mwaka huo huo, Moulay alijiunga na Kitivo cha Utawala Bora, Uchumi na Sayansi za Jamii katika Chuo Kikuu cha Mohammed VI Polytechnic (UM6P), kilichopo Salé, akichagua masomo ya uhusiano wa kimataifa kama fani yake kuu.
Moulay Hassan amekuwa akitekeleza majukumu mbalimbali ya kitaifa na kimataifa, akifuata nyayo za baba yake, Mfalme Mohammed VI.
Mwaka 2017, Moulay alikuwa ni mmoj wa washiriki wenye umri mdogo zaidi katika Mkutano wa Kimataifa wa One Planet Summit uliofanyika nchini Ufaransa, tukio lililompatia sifa na kutambuliwa kimataifa kutokana na ushiriki wake katika masuala ya mazingira na maendeleo endelevu.
Aidha Juni 28, 2019, Moulay Hassan alimwakilisha baba yake katika hafla ya uzinduzi wa shughuli za bandari mpya ya Tanger Med II, hatua iliyoimarisha bandari kuwa mojawapo ya eneo muhimu zaidi katika ukanda wa Bahari ya Mediterania.
Mwanamfalme Moulay Hassan. Picha na Mtandao
Vivyo hivyo, Septemba 30, 2029 mwanamfalme huyo alihudhuria mazishi aliyekuwa Rais wa Ufaransa, Jacques Chirac, jijini Paris yaliyofanyika katika Kanisa la Saint-Sulpice.
Siku hiyo hiyo, Moulay alishiriki pia katika chakula cha mchana kilichoandaliwa na Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron katika Ikulu ya Élysée, kwa heshima ya wakuu wa nchi waliokuwepo kuhudhuria mazishi hayo.
Wakati Novemba 17, 2022, Moulay Hassan alizindua maonesho ya Kimataifa na Makumbusho ya Wasifu wa Mtume Muhammad (S.A.W) na Ustaarabu wa Kiislamu katika makao makuu ya Shirika la Elimu, Sayansi na Utamaduni la Ulimwengu wa Kiislamu (ICESCO) Rabat.
Desemba 20, 2022, akiambana na baba yake Mfalme Mohammed VI na mjomba wake Prince Moulay Rachid, Moulay Hassan aliwapokea wachezaji wa timu ya taifa ya soka ya Morocco ukumbi wa Enzi wa Ikulu ya Kifalme ya Rabat.
Katika mwaka huo, timu ya Taifa ya Morroco ‘Atlas Lions’ ilipata mafanikio ya kuingia hatua ya nusu fainali katika michuano hiyo iliyokuwa ikifanyika Doha Qatar.
Kwa jumla, maandalizi ya Moulay Hassan yanaakisi mfumo wa kifalme wa Morocco unaolenga kumkuza ili kurithi kiti cha ufalme ambaye anakuwa kiongozi mwenye elimu, maadili, uwezo wa kijeshi na mtazamo wa kisasa, huku akihifadhi misingi ya mila na utamaduni wa taifa.
Amekidhi vigezo kurithi ufalme
Mwanamfalme Moulay ana sifa zote zote za kurithi kiti cha ufalme wa Morroco ikiwamo kuwa mtoto wa kiume wa Mohamed VI, umri wa uwezo wa kisiasa ambapo kijana ameandaliwa kieimu ya siasa, kijeshi na kidiplomasia.
Mwanamfalme Moulay Hassan akisalimia wakati wa ufunguzi wa michuano ya AFCON 2025 baina ya Morocco dhidi ya Comoro. Picha na Mtandao
Pia, Prince Moulay ana uelewa wa mila na utamaduni wa kifalme kwa sababu amelindwa na kuandaliwa katika mazingira yanayomhimiza heshima, nidhamu na utamaduni wa kifalme.
Sio hilo tu hata hatua ya kupewa mamlaka rasmi na ushiriki wake katika shughuli za kifalme ikiwemo hafla ya za hafla za kitaifa, kimataifa na kijeshi unathibitisha maandalizi yake rasmi.
Aidha kupitia vyeo vya kijeshi na kushiriki hafla za kitaifa, anapata uzoefu wa vitendo unaomuwezesha kutimiza jukumu la Mfalme baadaye.
Kwa nini anakataa wananchi kubusu mikono yake
Katika video mbalimbali mitandaoni zimemuonyesha Mwanamfalme Moulay akirudisha mikono nyuma kukataa kubusiwa na wananchi au kwenye dhimba mbalimbali alizomuwakilisha baba yake.
Hata hivyo kwa mujibu wa vyanzo mbalimbali mtandaoni hasa akimaanishwa Moulay anaporudisha nyuma mikono wakati watu wanapotaka kuibusu huwa ni kwa sababu za kiitifaki, kitamaduni na mtazamo wa kifalme wa kisasa na si kwa dharau.
Katika ufalme wa Morocco, hasa kwa kizazi kipya cha kifalme, kuna mwelekeo wa kupunguza vitendo vinavyoonyesha utiifu uliopitiliza. Badala ya kuibusu mkono, kusalimiana kwa kuinamisha kichwa au kupeana mkono kwa heshima kunahimizwa.
Pia, kuonyesha unyenyekevu na ukaribu na raia ambapo, Moulay anapoondoa mkono, anajaribu kuonyesha kuwa hahimizi kuabudiwa au kutengwa sana na wananchi, bali anataka heshima ionyeshwe kwa njia ya kawaida zaidi.
Imeandaliwa na Bakari Kiango kwa msaada wa mitandao.
