Unguja. Matukio ya udhalilishaji yameongezeka kwa asilimia 8.1 kufikia 107 kutoka 99 yaliyoripotiwa Oktoba, sababu ya ongezeko ikitajwa kuwa uhuru uliopitiliza wa wazazi kwa watoto wao.
Inaelezwa uhuru huo umesababisha watoto kufanya jambo lolote watakalo bila ya hofu, wala kujali athari za vitendo wanavyovifanya.
Akitoa taarifa leo Jumanne Desemba 23, 2025 Ofisa wa Divisheni ya Jinsia na Ajira kutoka Ofisi ya Mtakwimu Mkuu wa Serikali Zanzibar, Ahmada Hassan Suleiman, amesema matukio yaliyoripotiwa kupungua ni ya kutorosha, shambulio la aibu au kukashifu na usumbufu wa kingono.
Amesema waathirika wengi walikuwa watoto sawa na asilimia 81.3, wakifuatiwa na wanawake asilimia 17.8.
Wilaya ya Magharibi A, imeripotiwa matukio 17 sawa na asilimia 15.9 ikifuatia Wilaya ya Mjini, Magharibi B na Wilaya ya Wete ambazo zimeripotiwa matukio 15 sawa na asilimia 14.0 kwa kila wilaya.
Wilaya ya Kusini Unguja imeripotiwa kuwa na idadi ndogo ya matukio, yakiwapo mawili sawa na asilimia 2.0 ya matukio yote yaliyoripotiwa Novemba 2025.
Amesema, Wilaya ya Wete imeripotiwa kuwa na idadi kubwa ya matukio ya kubaka ikilinganishwa na nyingine, ambapo ina matukio ya kubaka 10 sawa na asilimia 16.9 kati ya matukio 59 ya ubakaji yaliyoripotiwa.
Ahmada amesema kati ya matukio 59 ya kubaka yaliyoripotiwa, tisa yameripotiwa kwa wanawake sawa na asilimia 15.3 na 50 yameripotiwa kwa wasichana sawa na asilimia 84.7.
“Matukio ya udhalilishaji yamefikia 107 ikilinganishwa na matukio 99 ya Oktoba. Kati ya hayo, matukio ya ubakaji yameshika kasi kutoka 47 hadi 59,” amesema.
Akitoa ufafanuzi kuhusu sababu za kuongezeka matukio ya udhalilishaji, Inspekta wa Polisi kutoka Makao Makuu ya Polisi Zanzibar, Makame Haji amesema ni uhuru uliopitiliza wa wazazi kwa watoto wao kufanya jambo lolote bila ya kujali yataleta athari kwao.
Hivyo, amewasihi wazazi wasitoe uhuru uliopitiliza kwa watoto, kwani husababisha kufanyiwa vitendo vya udhalilishaji kwenye jamii.
Pia, ameiasa jamii kutoa taarifa za udhalilishaji baada ya kutokea kwa matukio hayo ili kulinda ushahidi wa awali, hatua inayowezesha kukamilika kwa haraka kwa kesi.
Amesema matukio 91 kati ya 107 yaliyoripotiwa yapo chini ya upelelezi wa Jeshi la Polisi sawa na asilimia 85.0 ya matukio yote yaliyoripotiwa.
Vilevile, matukio 10 yapo mahakamani sawa na asilimia 9.3 na matukio sita yamepelekwa Ofisi ya Mkurugenzi Mashtaka.
Amesema mashauri 15 yaliyofunguliwa katika mahakama za udhalilishaji Zanzibar bado yanaendelea.
Fatma Serembe Khamis, kutoka Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora, amesema ili kupunguza vitendo vya udhalilishaji, Tume imekubaliana na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, kuanzisha programu mashuleni ili kutoa elimu kwa wanafunzi juu ya dhana nzima na namna ya kujilinda na udhalilishaji.
