Matumaini mapya NHIF bima ya afya kwa wote

Dar es Salaam. Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) umebainisha kuwa upo tayari kuanza utekelezaji wa bima ya afya kwa wote ifikapo Januari Mosi, 2026, kufuatia maboresho ya mifumo, maandalizi ya kifedha na ushirikishwaji wa wadau mbalimbali.

Hayo yamesemwa leo Jumatatu Desemba 22, 2025 na Mkurugenzi Mkuu wa NHIF, Dk Irene Isaka wakati wa mahojiano maalumu aliyoyafanya na Mwananchi, kuelekea utekelezaji wa bima ya afya kwa wote.

Amesema maandalizi yote muhimu yamekamilika kwa kushirikiana na Wizara ya Afya pamoja na Ofisi ya Rais – Tamisemi.

“Kwa maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan aliyoyatoa bungeni na msisitizo wa Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba matarajio ni kuanza utekelezaji Januari 2026. NHIF tupo tayari na  utekelezaji umeanza kwa baadhi ya makundi maalumu,” amesema.

Dk Isaka amesema NHIF imeboresha mifumo yake ya Tehama ili kuwezesha wananchi kujisajili binafsi, waajiri kusajili wafanyakazi wao na kutuma michango kwa njia ya mtandao.

Aidha, amesema mifumo hiyo imejaribiwa na kuthibitishwa kuwa na uwezo wa kuchakata madai kwa ufanisi.

Amefafanua kuwa mfumo mpya wa malipo umebadilika kufikia malipo ya mkupuo kabla ya huduma, awali, kulikuwa na malipo baada ya huduma kutolewa jambo lililohitaji maboresho makubwa ya mifumo ya ndani.

“Tumehakikisha mifumo yetu inasomana na mifumo ya taasisi nyingine za Serikali kama Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), Mamlaka ya Vitambulisho vya Taifa nchini (Nida), Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), Mfuko wa Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma (PSSSF), vyuo vikuu, Tume ya Vyuo Vikuu Tanzania (TCU), vyama vya ushirika pamoja na Wizara ya Afya na Tamisemi hadi kwenye vituo vya kutolea huduma,” amesema.

Amesema wamehakikisha vituo vya afya sasa vinaweza kusomana taarifa na makundi mengine mbalimbali.

Kaya zisizo na uwezo wa vifurushi

Akizungumzia kaya zisizo na uwezo, Dk Isaka amesema mchakato wa kuzitambua umefanyika kwa kushirikiana na Tamisemi na Mpango wa Kunusuru Kaya Maskini (Tasaf).

Amesema Serikali itachangia michango yao kwa mujibu wa kifungu cha 25 cha sheria ya bima ya afya kwa wote.

Amesema tayari Wizara ya Afya imeandaa kifurushi maalumu chenye huduma 372 kitakachohudumia kaya zisizo na uwezo pamoja na kaya za sekta isiyo rasmi.

“Kwa kaya masikini tunasubiri orodha pamoja na malipo yao, kwa sasa taarifa tulizonazo Serikali tayari imeshatenga fedha kwa ajili ya kulipia hizi kaya, naamini Januari tutakua tayari kuanza kutoa bima ya afya kwa wote,” amesisitiza.

Kwa wananchi wengine, mkurugenzi huyo amesema NHIF imeandaa vifurushi mbalimbali kulingana na uwezo na mahitaji, vikiwemo vifurushi vya Tarangire, Mikumi, Serengeti, Ngorongoro na Tanzanite.

Kwa kifurushi cha Tarangire mtu mmoja analipia  Sh168,000 kaya ya watu sita italipia Sh796,560 na kifurushi cha Ngorongoro kwa mtu mmoja ni Sh432,000 kaya ya watu sita ni Sh1,684,800.

Imeelezwa kifurushi cha Mikumi kwa mtu mmoja atapaswa kulipia Sh480,000 na kwa kaya yenye watu sita italipia Sh2,621,760 huku kifurushi cha Serengeti kwa mtu mmoja atalipia Sh792,000 na kaya yenye watu sita italipia Sh3,880,800.

Pia, kifurushi cha Tanzanite ambacho kwa mtu mmoja ni Sh2,712,000, kaya ya watu sita italipia Sh11,162,640.

Hata hivyo, Dk Isaka amefafanua kuwa kwenye kila kifurushi, awe ni mtoto, mtu mmoja wanandoa, na watoto wawili au watatu inategemea na idadi ya wanufaika.

“Kifurushi cha msingi cha kaya ya watu sita ni Sh150,000 kwa mwaka. Kwa vikundi au kaya kubwa zaidi, gharama hubadilika, ndiyo maana tunahamasisha wananchi kujiunga kwa mfumo wa vikundi. Mkiwa kwenye kikundi vifurushi vingine kwa kaya ya watu sita inakuwa 660,000 ndiyo maana tunahamasisha watu wajiunge,” amesema.

Dk Isaka amesema NHIF pia imeanza kusajili vikundi vya ushirika, Saccos, vikundi vya wakulima na wafanyabiashara kwa kushirikiana na msajili wa vyama vya ushirika.

Aidha, amesema mashirika ambayo Serikali ina umiliki wa zaidi ya asilimia 30 yameelekezwa kujiunga na NHIF kuanzia Januari 2026, bila kuondolewa haki ya kutumia bima binafsi.

“Kuna mashirika ambayo Serikali ina zaidi ya asilimia 30 hayo mashirika tumeyaandikia barua kwamba kuanzia Januari wanapaswa kuwa wanachama wa NHIF pia tumehamasisha wananchi kujiunga kwa hiari, na watachangia mfumo wa asilimia sita ya mwajiriwa na sita ya mwajiri,” amesema.

Pia, amesema kwa wale wa Bima ya Afya ya Jamii (CHF), wameanza kuwasajili na wengine ambao si kaya maskini.

Dk Isaka amesema hali ya kifedha ya NHIF imeimarika kwa kiasi kikubwa, akibainisha kuwa mfuko umetoka kwenye nakisi na kufunga hesabu za mwaka wa fedha 2024/2025 ukiwa na ziada ya Sh225 bilioni.

“Muda wa kulipa madai ya watoa huduma umepungua kutoka siku 120 hadi siku 55. Uhimilivu wa mfuko umeongezeka kutoka uwezo wa kulipa madai ya miezi saba hadi mwaka mmoja na nusu,” amesema.

Ameongeza kuwa uwiano wa matumizi dhidi ya michango umeshuka kutoka asilimia 172 hadi karibu asilimia 69, hali inayoonyesha uthabiti wa mfuko, ukilinganisha na kiwango kinachopendekezwa kimataifa cha asilimia 70.

Kwenye uwekezaji na maboresho ya huduma, Dk Isaka amesema NHIF imewekeza zaidi ya Sh50 bilioni katika ununuzi wa vifaa tiba, vitendanishi, ukarabati wa majengo na kuimarisha mifumo ya vituo vya afya, ikiwa ni pamoja na kuhamia kwenye matumizi ya kadi za kielektroniki kupitia simu.

Kwa mujibu wa Dk Isaka, katika kipindi cha miaka minne iliyopita NHIF imelipa zaidi ya Sh470 bilioni kwa watoa huduma.

Usimamizi, malalamiko na ufuatiliaji

Amesema akaunti maalum ya Bima ya Afya kwa Wote tayari imefunguliwa na ipo Benki Kuu ya Tanzania kwa ajili ya kulipa madai, huku mifumo ya ufuatiliaji ikitumia alama za vidole au utambuzi wa sura (facial recognition).

“Vituo vitatumia alama za vidole na utambuzi wa sura kwa ambao alama zao za vidole zitaonekana kufutika watatumia alama za sura kwenye utambuzi,” amefafanua.

Amesema katika utoaji wa huduma watakuwa wakifanya tathmini na ufuatiliaji kila mwezi kujua nani alitibiwa na magonjwa yapi kwa kuangalia kituo kimetibu idadi ipi na kilitumia kiasi gani katika fungu walilopewa.

“Tutafuatilia karibu, wakisema tumemlaza mgonjwa kwa siku 10 tutaenda kuangalia kama ni kweli kupitia alama za vidole na sura tutafuatilia na kufanya tathmini.”

Aidha amesema kwa wananchi wenye malalamiko watawasiliana kupitia namba ya dharura 199 au kituo cha huduma kwa wateja 0800 787 800, huku maofisa wa NHIF wakiwepo vituoni kusaidia wanachama papo hapo.

Alipoulizwa iwapo kifurushi cha watu sita cha Sh150,000 kina huduma zote muhimu, amesema  mwanachama atatibiwa magonjwa yote kulingana na kifurushi chake cha msingi, huku akisisitiza kuwa Serikali imeweka fungu kushughulikia magonjwa yasiyoambukiza ambayo mara nyingi yamekuwa mwiba kwa wanufaika wengi.

“Wanachama wetu watapewa punguzo kwenye baadhi ya vipimo vikubwa na huduma zote muhimu, kifurushi hiki kimechukua historia ya magonjwa yaliyopo katika vituo vya afya vya msingi, imechukua magonjwa yote muhimu ambayo mwanachama anaweza kuyapata katika ngazi hiyo.”

Kwa upande wa wanafunzi, amesema usajili unaendelea vyuoni na shuleni, ambapo gharama ya kifurushi hupungua endapo bima itakatwa kupitia taasisi ya elimu, akitaja ni kiasi cha Sh50,400.

Amesisitiza kuwa huduma muhimu kwa mama na mtoto zitaendelea kutolewa bila kikwazo, hususan kupitia mifumo ya Serikali iliyo chini ya Wizara ya Afya.

Alipoulizwa kuhusu kaya yenye watu zaidi ya sita, Dk Isaka amesema wataanzisha kaya nyingine ndani ya kaya, akisisitiza kuwa bima ya afya kwa wote haitajali ndugu wa damu hivyo hata watumishi wa ndani wanaweza kuungwa kwenye mfumo.

Dk Isaka amesema NHIF ina uwezo wa kusimamia utekelezaji wa Bima ya Afya kwa Wote nchi nzima, huku zoezi hilo likianza kwa majaribio katika maeneo yote ya kiutawala ili kujifunza na kuboresha zaidi mfumo.

“Tumefanya maandalizi ya kina. Tunaanza huku tukijifunza na kufanya maboresho pale inapobidi, lengo likiwa kumhakikishia kila Mtanzania haki ya kupata huduma za afya,” amesema.