Meya Zanzibar awauma sikio madiwani

Unguja. Meya wa Jiji la Zanzibar, Kamal Abdulsatar Haji, amesema mafanikio ya Baraza la Jiji yanategemea zaidi ushirikiano na heshima katika kutekeleza majukumu yake.

Amesema bila ya ushirikiano kati ya baraza, kamati na watendaji wake hakutakuwa na utoaji huduma nzuri kwa wananchi.

Kamal ametoa kauli hiyo leo Jumanne Desemba 23, 2025 wakati akifungua mafunzo ya madiwani wa Baraza la Jiji yaliyofanyika katika ukumbi wa mikutano wa baraza hilo, Michenzani Mall, Mjini Unguja. 

“Mafunzo haya yatatoa fursa ya kujifunza mbinu za uongozi shirikishi, utatuzi wa migogoro, usimamizi wa rasilimali za umma na kushirikiana na wadau wa maendeleo,” amesema.

Amesema ni wajibu wa kila mmoja wao kuzingatia maadili ya uongozi kwa kuepuka vitendo vya rushwa, upendeleo na matumizi mabaya ya madaraka, kwani wananchi wanawatazama na wanatarajia kuona mfano bora wa uongozi unaozingatia masilahi ya umma kuliko binafsi.

Meya Kamal amewataka madiwani kufuata misingi ya kiuongozi, kwani wao ni kiungo muhimu kati ya Serikali na wananchi katika kutatua changamoto zao.

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Jiji la Zanzibar, Salmini Abdallah Amour, amewasihi madiwani kuwa watulivu ili kufanikisha lengo la mafunzo hayo.

Amesema mafunzo hayo ni njia mojawapo ya kudumisha umoja, mshikamano na usawa kwao na hilo litawasaidia kufika wanapostahili, ikiwemo kuwa karibu na wananchi wakati wa utoaji huduma.