Dar es Salaam. Kanisa la Anglikana Tanzania linaomboleza kifo cha Kasisi Edward Komba, aliyekuwa Mkuu wa Chuo cha Theolojia cha Mtakatifu Marko (St. Marks) Dar es Salaam.
Komba ambaye ni Canon wa Dayosisi ya Tanga, aliyefariki dunia kwa ajali ya gari jana Desemba 22, 2025 katika eneo la Mbezi, jijini Dar es Salaam.
Taarifa iliyotolewa leo Jumanne Desemba 23, 2025 na Mwenyekiti wa Bodi ya chuo hicho kilichopo Buguruni Malapa, ambaye pia ni Askofu Mkuu wa kanisa hilo Tanzania, Dk Maimbo Mndolwa, imeeleza kuwa Komba alikuwa njiani kuelekea Kanisa Kuu la Korogwe, mkoani Tanga, kwa ajili ya ibada ya misa ya kuhuisha sakramenti.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, ibada aliyokuwa akielekea kuiongoza ilikuwa ni ya waumini waliovunja maagano ya sakramenti zikiwamo za ubatizo, toba, kipaimara, ushirika mtakatifu na daraja takatifu, iliyopangwa kufanyika leo Desemba 23, 2025 katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Mikaeli na Malaika Wote, Korogwe.
Taarifa imeeleza Desemba 25, 2025, Dayosisi ya Dar es Salaam itaandaa mwili wa marehemu na jioni utapelekwa Chuo cha Theolojia cha St. Marks kwa ajili ya mkesha.
Desemba 26, 2025 mchana, kutafanyika misa kuaga mwili katika kikanisa cha St. Marks, ikiongozwa na Askofu wa Kanisa Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Jackson Sostenes kabla ya mwili kusafirishwa kuelekea Korogwe, mkoani Tanga.
Baada ya kuwasili Korogwe, mwili utapokewa na Kasisi Kiongozi wa Dayosisi ya Tanga, Ven. Canon Kiango na kuingizwa katika Kanisa la Mtakatifu Andrea, Manundu kwa ajili ya sala fupi ya usiku, kabla ya kupelekwa nyumbani kwa marehemu Kwamkole Manundu, kwa ajili ya mkesha.
Desemba 27, 2025, saa mbili asubuhi kutakuwa na ratiba ya chakula na kuaga mwili nyumbani kwa marehemu Kwamkole, kabla ya saa nne asubuhi mwili kupelekwa Kanisa Kuu la Mtakatifu Mikaeli na Malaika Wote Korogwe kwa ibada ya misa ya mazishi itakayoanza saa 5:30 asubuhi hadi saa 7:30 mchana.
Desemba 29, 2025 saa tatu asubuhi, itafanyika ibada ya misa ya kumaliza msiba katika Kanisa la Mtakatifu Dominick Korogwe.
Kasisi Komba alizaliwa Juni 13, 1967. Kitaaluma alikuwa mwalimu, mchumi na mtawala.
Amefariki dunia akiwa mhazini wa Baraza la Kanuni la Kanisa Kuu na mshauri wa masuala ya uchumi wa Dayosisi ya Kanisa Anglikana Tanga.
Katika maisha yake ya utumishi, aliwahi kuhudumu kama Katibu wa Dayosisi ya Tanga na kutumikia maeneo mbalimbali.
Elimu yake aliipata katika vyuo vya TTC Korogwe, Lutheran Junior Seminary Training for Christian Education Morogoro, St. Marks Theological College Dar es Salaam, Chuo cha Kumbukumbu ya Mwalimu Nyerere na Uganda Christian University.
Kitaaluma na kiuongozi, aliwahi kufanya kazi kama Mratibu wa Mafunzo ya Elimu ya Kikristo katika shule za msingi, sekondari na vyuo na Naibu Mkurugenzi wa Utafiti, Fedha, Mipango na Uchumi katika Chuo cha St. Augustine Muheza Institute of Health and Allied Sciences (Samihas).
