Mloganzila kuwa kitovu cha uzalishaji dawa, mafunzo – Mchengerwa

Dar es Salaam. Serikali imetangaza eneo la Mloganzila jijini Dar es Salaam kuwa kitovu maalumu cha uzalishaji wa dawa, mafunzo ya vitendo, huduma za matibabu na utafiti wa kisayansi.

Hatua hiyo inalenga kutatua changamoto ya ukosefu wa maeneo mahususi ya uwekezaji kwa viwanda vya dawa nchini.

Akizungumza leo Jumanne, Desemba 23, 2025, na wazalishaji wa dawa nchini kuhusu mwelekeo mpya wa sekta ya dawa, Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa amesema Serikali imepokea maelekezo maalumu kutoka kwa Rais Samia Suluhu Hassan, kuhakikisha eneo la Mloganzila linafunguliwa rasmi kwa wawekezaji wa viwanda vya dawa.

“Tumepewa maelekezo mahususi kutoka kwa Rais. Eneo la Mloganzila lipo wazi na wawekezaji wote wa viwanda vya dawa watakaojitokeza wataelekezwa kwenda Mloganzila kuwekeza. Ni eneo kubwa sana na lina fursa nyingi,” amesema.

Amesema Serikali itaendelea kutoa nafuu na vivutio mbalimbali kwa viwanda vya dawa ili kuvutia wawekezaji wa ndani na nje ya nchi, huku ikilenga kuanzisha mkusanyiko wa viwanda (industrial cluster) utakaowezesha kushirikiana katika uzalishaji, uboreshaji wa ubora na upatikanaji wa masoko.

Katika mkakati huo, Mchengerwa amesema Hospitali ya Taifa Muhimbili inatarajiwa kushirikiana kwa karibu na wawekezaji pamoja na taasisi za mafunzo, kwa lengo la kuunganisha huduma za matibabu, mafunzo ya kitaaluma na uzalishaji wa dawa ndani ya eneo hilo.

“Mloganzila haitakuwa tu eneo la viwanda. Tutaendelea kutibu wananchi wetu pale, kutoa mafunzo na kufundisha kwa vitendo namna ya kutengeneza dawa au kumtibu mgonjwa. Mwanafunzi atapata mafunzo halisi akiwa kazini,” amesema.

Pia, Mchengerwa amesema changamoto kubwa inayokwamisha viwanda vya ndani vya dawa si kukosekana kwa soko, bali ni kushindwa kufikia viwango vya kimataifa vya uzalishaji, hususan vinavyotambuliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) na Good Manufacturing Practice (GMP).

Amesema viwango ndivyo kitovu cha mjadala wa sasa na maandalizi yanaendelea kuhakikisha Tanzania inazalisha dawa zenye ubora unaokubalika kimataifa.

Waziri wa Afya, Mohammed Mchengerwa akizindua kikosi kazi cha kuhakikisha na kuharakisha uwekezaji viwanda vya dawa.

“Hili si tatizo la soko, soko lipo. Tatizo ni viwango. Takwimu zinaonyesha bado hatujajipanga kikamilifu kufikia viwango vya kimataifa,” amesema.

Mchengerwa amesema kuna baadhi ya viwanda vya dawa vimekuwa sokoni kwa zaidi ya miaka 50 bila kufikia viwango vya WHO-GMP, hali inayodhoofisha ushindani wao ndani na nje ya nchi.

“GMP si cheti cha mapambo, ni tiketi ya kuingia sokoni. Hatuwezi kuendelea kuwavumilia wazalishaji wadogo pekee; lazima tufanye maamuzi magumu. Sekta ya dawa inahitaji uzalishaji wa kiwango kikubwa, mifumo madhubuti ya ubora na uwekezaji wa kimkakati,” amesema.

Kuhusu waagizaji wa dawa, Mchengerwa amesema Serikali haitavumilia biashara za uingizaji wa dawa kwa kisingizio cha kulinda masoko yaliyopo, huku baadhi ya waagizaji wakikaa kwenye biashara hiyo kwa miaka 10 hadi 20 bila mpango wa kuwekeza kwenye uzalishaji wa ndani.

“Wenye uwezo wanapaswa kujikita kwenye uzalishaji wa dawa kwa mustakabali wa Taifa. Hii ni ajenda ya Taifa ya kulinda uchumi wa viwanda kwa kizazi cha leo na kijacho,” amesema.

Ajibu hoja za wenye viwanda

Akijibu hoja zilizoibuliwa na wenye viwanda, Mchengerwa amesema Serikali imezipokea na kuzifanyia kazi hoja zote zilizoibuliwa ikieleza kuwa changamoto hizo ni za msingi, kwani zinagusa moja kwa moja gharama za uzalishaji na uwezo wa viwanda vya ndani kukua na kushindana.

Amesema baadhi ya maelekezo tayari yametolewa na hatua zimeanza kuchukuliwa ili kuimarisha uzalishaji wa ndani na kupunguza utegemezi wa dawa kutoka nje ya nchi.

Kuhusu hoja ya ukosefu wa soko la bidhaa za ndani, Serikali imesema imeanza kulishughulikia kwa vitendo kwa kutumia mfumo wa ununuzi wa umma, ikitaja mfano wa ununuzi wa maji tiba (IV fluids) ambapo zaidi ya bidhaa 20 sasa zinanunuliwa kutoka kwa wazalishaji wa ndani.

“Tutaielekeza Bohari ya Dawa (MSD) kununua bidhaa zinazozalishwa nchini mara tathmini ya ubora itakapokamilika. Lengo ni kuhakikisha fedha za Serikali zinachochea uzalishaji wa ndani,” amesema Mchengerwa.

Kuhusu Sheria ya Ununuzi wa Umma, amesema Serikali inaendelea kufanya marekebisho, ikianzia katika kuboresha mtiririko wa fedha kwa wazalishaji wa ndani kwa kutumia mifumo ya kielektroniki badala ya malipo ya fedha taslimu, ili kupunguza ucheleweshaji wa malipo.

Katika suala la gharama kubwa za uzalishaji, ikiwemo maji na umeme, amesema Serikali itafanya tathmini ya kutoa motisha na ruzuku maalumu kwa viwanda, vikiwemo vya dawa, ili kupunguza gharama hizo.

Serikali pia imeahidi kuratibu upatikanaji wa mikopo nafuu kwa viwanda vya dawa, ikitambua kuwa ukosefu wa mitaji ni moja ya vikwazo vikubwa vinavyokwamisha ukuaji wa sekta hiyo.

Kwa upande wao, wazalishaji wa dawa wakiongozwa na Mwenyekiti wa Wamiliki wa Viwanda vya Dawa nchini, Bashiru Haroun, wamesema vipo na uwekezaji umefanyika, hivyo mkazo unapaswa kuwa kuvikuza na kuongeza kasi ya uwekezaji uliopo.

Amesema kampuni 38 tayari zilionyesha nia ya kuwekeza katika sekta ya dawa, huku Watanzania wakiamua kujipiga kifua na kuhakikisha uwekezaji mkubwa unafanywa na wazawa.

“Lengo letu ni kuhakikisha tuna uwezo wa kuzalisha tembe ya aina yoyote. Tuliwekeza kwa imani kubwa, lakini tumekumbana na changamoto nyingi licha ya ushirikiano mzuri kutoka Wizara ya Afya, Mganga Mkuu wa Serikali na TMDA (Mamlaka ya Dawa na Vifaa Tiba),” amesema Haroun.

Ameeleza kuwa kwa sasa Tanzania inajitosheleza kwa dawa kwa kiwango cha takribani asilimia 10 pekee, akisisitiza umuhimu wa kuwepo sera maalumu zitakazolinda na kukuza viwanda vya dawa ili kuongeza kiwango hicho kwa manufaa ya Taifa.

“Haiwezekani bidhaa kama drip, ambayo zaidi ya asilimia 90 ni maji, kuendelea kuagizwa kutoka nje. Tunahitaji sera inayosema chochote kinachoweza kuzalishwa ndani kisiagizwe nje,” amesema.

Amezitaja Kenya na Uganda kama mifano ya nchi zilizolinda viwanda vyao vya dawa, huku akisema kukosekana kwa ulinzi huo ndiko kunakozorotesha viwanda vya ndani nchini.

Wazalishaji pia wamelalamikia mfumo wa ununuzi wa dawa unaoendeshwa na MSD, wakidai kutokuwepo kwa malipo ya awali (advance payments) kwa wazalishaji wa ndani, huku wakidai viwanda vya nje kunufaika zaidi na mfumo huo.

Kuhusu kodi, Haroun amesema viwanda vya ndani vinakabiliwa na changamoto ya kulipa VAT na tozo mbalimbali, akitaka Wizara ya Afya ikae na wizara nyingine ikiwamo Wizara ya Fedha ili kuweka mkakati wa pamoja wa kulinda viwanda vya dawa.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Seif Shekalaghe amesema changamoto zote zilizoibuliwa zinaonyesha wazi kuwa bado kuna nafasi kubwa ya kuboresha mazingira ya uzalishaji.

Amesema idadi ya viwanda vya dawa nchini imeongezeka kutoka vinane mwaka 2022 hadi viwanda 13 kwa sasa, hatua inayodhihirisha dhamira ya Serikali kukuza sekta hiyo.

Dk Shekalaghe ameongeza kuwa Serikali imeboresha mifumo ya usajili wa dawa, ambapo muda   umepunguzwa kutoka siku 180 hadi   60, ili kuharakisha uingizwaji wa bidhaa sokoni.