Moshi yafurika, abiria wahaha kupata usafiri

Moshi. Ikiwa imebaki siku moja kabla ya kuingia Sikukuu ya Krismasi, hali ya usafiri katika mji wa Moshi, mkoani Kilimanjaro, imekuwa changamoto kubwa kutokana na ongezeko la wageni na wakazi wanaosafiri kuelekea vijijini kusherehekea sikukuu za mwisho wa mwaka.

Changamoto hii imeathiri zaidi abiria wanaosafiri kutoka Moshi Mjini kuelekea Rombo, Machame, Kibosho na Marangu, ambapo mahitaji ya usafiri yamezidi idadi ya magari yanayopatikana.

Leo Jumanne, Desemba 23, 2025, mwandishi wa Mwananchi amefika katika Kituo Kikuu cha Mabasi mjini Moshi na kushuhudia abiria wengi waliokuwa wakisubiri usafiri.

Baadhi ya abiria wamelazimika kukaa muda mrefu, wengine wakigombania kuingia kwenye magari pindi yanapofika, huku baadhi wakiwazimu kupanda kupitia madirishani kutokana na uhaba wa usafiri.

Baadhi ya abiria wakiwa katika Stendi ya Mabasi Moshi mjini, leo Desemba 23, 2025 wakisubiri usafiri kuelekea maeneo mbalimbali mkoani Kilimanjaro.

Agness Massawe, anayesafiri Rombo, amesema: “Tunataka kwenda nyumbani kwa sikukuu, lakini magari ni machache. Tunagombania usafiri kila gari linapofika. Tunamuomba Serikali kuongeza magari katika maeneo yenye changamoto ili tuweze kusafiri kwa usalama.”

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Magari yaendayo Rombo, Alfani Kupaza, amesema licha ya kuwepo kwa zaidi ya magari 100 yanayofanya safari kati ya Moshi na Rombo, idadi ya abiria leo ilikuwa kubwa kuliko kawaida.

“Tayari tumeongeza magari ya aina ya Coaster za utalii, lakini mahitaji bado ni makubwa. Tunaahidi kuhakikisha hakuna abiria anayekwama stendi,” amesema Kupaza.

Msimamizi wa magari ya Moshi–Marangu, Amini Msangi, amesema ongezeko la usafiri ni kawaida kipindi cha sikukuu, huku wakiendelea kuhakikisha abiria wote wanasafiri kwa wakati na kwa nauli rafiki.

Baadhi ya abiria wakiwa katika Stendi ya Mabasi Moshi mjini, leo Desemba 23, 2025 wakisubiri usafiri kuelekea maeneo mbalimbali mkoani Kilimanjaro.

Kwa upande wa Ofisa Mfawidhi wa LATRA Mkoa wa Kilimanjaro, Paulo Nyello, amesema mamlaka hiyo imechukua hatua kwa kutoa vibali kwa magari ya njia nyingine kusaidia kusafirisha abiria kuelekea wilaya zinazokumbwa na changamoto za usafiri, hususan Rombo.

Mbali na changamoto ya usafiri, mji wa Moshi umebaini msongamano mkubwa wa watu katika masoko na barabarani. Barabara zilizokumbwa na msongamano ni Nyerere, Sokoni, Boma, Kristu Mfalme, Rindi Lane, Stesheni na barabara kuu ya Njia Panda ya Himo–Arusha.

Hali hiyo inatarajiwa kuendelea hadi jioni ya Desemba 24, wakati wakazi wengi wakiwahi kuondoka mjini kuelekea vijijini kusherehekea Sikukuu ya Krismasi.