Moshi. Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Nurdin Babu, amewahakikishia wananchi na wageni wanaotarajiwa kutembelea mkoa huo kipindi cha sikukuu za mwishoni mwa mwaka, kuwa hali ya ulinzi na usalama imeimarishwa.
Vilevile, ametoa rai kwa viongozi wa dini kushirikiana na Serikali kuhubiri amani, utulivu na mshikamano katika maeneo ya ibada ili sikukuu hizo zisherehekewe kwa amani na usalama.
Amesema vyombo vya ulinzi na usalama vimejipanga kikamilifu kuhakikisha amani na utulivu vinaendelea kutamalaki, huku akiwataka wananchi na wageni kushirikiana na vyombo hivyo kwa kuheshimu sheria, mila na desturi za maeneo wanayotembelea ili sherehe za mwisho wa mwaka zifanyike bila vurugu au viashiria vya uvunjifu wa amani.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maandalizi ya sikukuu hizo, Babu amesema kila ifikapo Desemba, hususani kuelekea Krismasi na Mwaka Mpya, wakazi wa Mkoa wa Kilimanjaro walio katika shughuli za kibiashara na ajira mikoa mingine hurejea nyumbani kwa mapumziko na kusherehekea sikukuu hizo pamoja na familia zao.
Amewataka wote wanaorejea nyumbani au kuutembelea mkoa huo kuungana na wakazi wake kudumisha utulivu uliopo.
“Nitoe wito kwa viongozi wa dini, kushirikiana na Serikali kwa kuhubiri amani katika maeneo ya ibada, Serikali itatoa ulinzi wa kutosha wakati wa mikesha ya Krismasi, sikukuu na shamrashamra za Mwaka Mpya,” amesema.
Amesema wanaorejea nyumbani mwishoni mwa mwaka si kwa ajili ya sherehe pekee, bali pia ni fursa kwa familia kujadiliana masuala mbalimbali ya kimaendeleo.
“Hakuna mbege nzuri kama inayopatikana nyumbani Kilimanjaro. Kila kabila lina utamaduni wake, na huu ni utamaduni wa watu wa Kilimanjaro. Niombe tusiuache, kila mwisho wa mwaka tuje kwa wingi, tusherehekee na familia zetu, tujadili masuala ya maendeleo na kupanga mikakati mizuri ya mwaka mpya,” amesema.
Kuhusu burudani, amewataka wamiliki wa kumbi za starehe na wafanyabiashara wanaotoa burudani kuhakikisha wanazingatia ulinzi wa watoto kwa kutowaruhusu kuingia katika maeneo yasiyowahusu.
“Watoto wabaki katika maeneo yanayowafaa na warejee nyumbani mapema, waendelee kulindwa na wazazi na walezi wao,” amesema.
Babu akizungumzia usalama barabarani, amewahimiza madereva kuzingatia sheria za usalama barabarani, kuheshimu alama na viwango vya mwendo vilivyowekwa, pamoja na kuepuka matumizi ya vilevi wanapoendesha vyombo vya moto.
Baadhi ya wananchi wameeleza mikusanyiko ya kifamilia na kijamii inayofanyika mwishoni mwa mwaka inachangia kuimarisha uhusiano, kudumisha udugu na kufufua mshikamano miongoni mwa familia na jamii kwa ujumla.
Hilda Kisanga, amesema kipindi cha mwisho wa mwaka hutumika kujenga upya uhusiano na kuimarisha mshikamano wa kifamilia na kijamii.
Amesema mikusanyiko hiyo hutumika pia kama fursa ya kupatanisha, kusuluhisha migogoro ndani ya familia na jamii, pamoja na kujadili masuala ya kiuchumi na maendeleo.
Rashid Juma, amesema mbali ya hujadili masuala ya maendeleo ya kiuchumi, hubadilishana uzoefu wa kibiashara na kuimarisha mshikamano wa kusaidiana kijamii.
“Tunapokutana katika sikukuu za mwisho wa mwaka pia tunatumia muda huo kutambulishana, kujenga mitandao ya kijamii na kuweka mikakati ya kimaendeleo kwa mwaka mpya unaoanza,” amesema.
