SERIKALI YAWATAKA VIJANA WAACHANE NA UCHUUZI, WAINGIE UZALISHAJI

::::::::::::

Na Mwandishi Wetu

SERIKALI imewataka vijana wa Tanzania kuachana na uchumi wa uchuuzi na usambazaji wa bidhaa kutoka nje, na badala yake kuelekeza nguvu kwenye uzalishaji na utengenezaji wa bidhaa ndani ya nchi.

Wito huo umetolewa na Waziri wa Ofisi ya Rais, Maendeleo ya Vijana, Joel Mnanauka, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu dira ya Serikali katika kuwawezesha vijana kiuchumi.

Mnanauka amesema maono ya Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan ni kuona vijana wanakuwa wamiliki wa uchumi na watengenezaji wa ajira.


Amesisitiza kuwa vijana hawapaswi kubaki wachuuzi wa bidhaa za nje, bali wawe wazalishaji na wachakataji wa rasilimali za ndani.

Ameeleza kuwa mwelekeo huo ndio msingi wa kaulimbiu ya wizara isemayo “Vijana Tuyajenge Tanzania Yetu.”

Kwa mujibu wa waziri huyo, kwa mara ya kwanza Serikali imeunda wizara maalum ya maendeleo ya vijana chini ya Ofisi ya Rais, hatua inayodhihirisha dhamira ya dhati ya Serikali kwa kundi hilo.

Amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha vijana wanasikilizwa, wanafikiwa walipo na wanashirikishwa kikamilifu katika maendeleo ya taifa.

Akizungumzia takwimu za sensa ya mwaka 2022, Mnanauka amesema vijana wenye umri wa miaka 15 hadi 35 ni zaidi ya milioni 20.6 kati ya Watanzania milioni 60.

Ameeleza kuwa hali hiyo inaibua wajibu mkubwa kwa Serikali kuwekeza kwenye mifumo ya kuwawezesha vijana kiuchumi.


Amesema Serikali inaelekeza nguvu kwenye uzalishaji, viwanda vidogo na vya kati pamoja na biashara zenye kuongeza thamani.

Kuhusu hatua mahsusi, Mnanauka amesema utekelezaji wa sheria za manunuzi ya umma umeimarishwa, zikihitaji taasisi za Serikali kutenga asilimia 30 ya bajeti ya ununuzi kwa makundi maalum yakiwemo makampuni ya vijana.

Amesema kuanzia mwaka 2021 hadi 2025, zaidi ya Sh bilioni 10.8 zimeelekezwa kwenye kampuni ndogo za vijana ili kuziimarisha kibiashara.

Amefafanua kuwa lengo si kutoa fedha ndogondogo, bali kukuza kampuni zenye uwezo wa kudumu na kuajiri wengine.

Vilevile, amesema Serikali imeanzisha mpango wa Youth Investment Program pamoja na mpango wa Maeneo Maalum ya Uzalishaji kwa Vijana (Youth Special Economic Zones).

Amesema maeneo hayo yatawawezesha vijana kupata mitaji, mitambo, umeme, maji na huduma zote za Serikali sehemu moja.

Lengo, amesema, ni kuwa na kampuni za vijana laki moja ndani ya miaka mitano, huku kampuni 20,000 zikiwa ndani ya maeneo hayo maalum.

“Tunataka kutoka kwenye uchumi wa uchuuzi kwenda uchumi wa uzalishaji na utengenezaji,” amesema Mnanauka.