TANZANIA YAJIPANGA KUWA KITOVU CHA UZALISHAJI DAWA AFRIKA

SERIKALI imetangaza rasmi mwelekeo mpya wa kimkakati wa kuharakisha uwekezaji wa viwanda vya bidhaa za afya nchini, ikiwa ni hatua ya kuimarisha usalama wa afya wa Taifa, kupunguza utegemezi wa dawa kutoka nje na kuliweka Taifa kwenye ramani ya uzalishaji wa dawa barani Afrika na duniani.

Mwelekeo huo umetangazwa leo Desemba 23, 2025 jijini Dar es Salaam na Waziri wa Afya, Mhe. Mohamed Mchengerwa, wakati wa kikao cha wazalishaji wa dawa na bidhaa za afya pamoja na uzinduzi wa Kikosi Kazi cha Uharakishaji wa Uwekezaji wa Viwanda vya Dawa nchini kilichofanyika katika Ofisi Ndogo za Wizara ya Afya.

Mhe. Mchengerwa amesema ujenzi wa viwanda vya dawa ni uamuzi wa kimkakati wa muda mrefu wa Serikali, akisisitiza kuwa usalama wa afya wa Taifa hauwezi kujengwa kwa kutegemea uagizaji wa dawa pekee.

“Ujenzi wa viwanda vya dawa si mpango wa majaribio bali ni uamuzi wa kimkakati uliokwishaamuliwa na Serikali. Usalama wa afya wa Taifa unahitaji uzalishaji wa ndani unaokidhi viwango vya kimataifa,” amesema Waziri Mchengerwa.

Amebainisha kuwa Serikali imeanzisha mfumo maalum wa kuharakisha uwekezaji unaojulikana kama Green-Lane Approval System, unaotekelezwa chini ya mpango wa Pharmaceutical Investment Acceleration Programme, sambamba na kuundwa kwa Pharmaceutical Investment Acceleration Taskforce (PIAT) itakayoratibu na kuboresha mazingira ya uwekezaji wa viwanda vya dawa nchini.

“Tumeondoa urasimu wa maamuzi ya mizunguko mirefu. Mwekezaji mwenye nia ya dhati atapata majibu ya haraka, ya wazi na yanayotabirika,” amesisitiza.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Wamiliki wa Viwanda vya Dawa nchini, Bw. Bashir Haroon, amesema wazalishaji wako tayari kushirikiana kikamilifu na Serikali ili kufikia ndoto ya uzalishaji wa ndani wa bidhaa za afya.

Amesema hatua hizo zitawanufaisha wananchi kupitia upatikanaji wa uhakika wa dawa kwa gharama nafuu, huku akiiomba Serikali kuendelea kushughulikia changamoto zinazowakabili wazalishaji ili kuongeza wigo wa uzalishaji wa bidhaa za afya nchini.