TRA United yamng’ang’ania Denis Nkane

MABOSI wa TRA United bado hawajakata tamaa juu ya kumnasa winga Denis Nkane anayeitumikia Yanga, baada ya sasa kuwasilisha maombi rasmi ya kutaka iwepe mchezahi huyo.

TRA inayojiandaa kushiriki michuano ya Kombe la Mapinduzi 2026 kwa mara ya kwanza itakayoanza Desemba 28 visiwani Zanzibar, ilisema imewasilisha ombi kwa Yanga ili wazungumze juu ya kumpata Nkane anayewaniwa pia na timu nyingine ikiwamo JKT Tanzania.

Nkane bado ana mkataba na Yanga na ametaka kutolewa kwa mkopo baada ya ugumu wa namba alioupitia kwa kipindi kirefu ndani ya kikosi hicho tangu aliposajiliwa kutoka Biashara United.

Taarifa za ndani zililiambia Mwanaspoti, Mabosi wa TRA wamepania kunasa saini na Nkane na wamewasilisha ombi la kufanya mazungumzo.

“Mchezaji akiwa anatafutwa na timu nyingi wakati mwingine anaweza kuyumba katika kufanya uamuzi, tunataka kutengeneza timu kubwa itakayokuwa na wachezaji wakubwa ndiyo maana tunamtaka Nkane, ni mchezaji mzuri,” kilisema chanzo hicho cha TRA na kuongeza;

“Tumewaomba viongozi wenzetu wa Yanga watupe nafasi ya kuongea na Nkane ili aelewe hesabu zetu kwake nadhani ataelewa dhamira ya TRA, tunasubiri majibu yao. Kama tukimpata Nkane tutakuwa na viungo bora hapo tutakuwa tumebakiza watu kama watatu wa maeneo mengine ambao kocha wetu anawataka.”

Mwanaspoti iliwahi kuandika timu ambazo zilipeleka maombi ya kumtaka Nkane zilikuwa mbili, JKT Tanzania na TRA United.

Lakini kwa sasa TRA ina nafasi kubwa zaidi, huku JKT ikiwa na ugumu kutokana na kudaiwa kuibania Yanga msimu uliopita kumpata kipa Yacoub Seleman ambaye anaichezea Simba kwa sasa.