MEYA wa Manispaa ya Kibaha, Dkt. Nicas Mawazo, ameitaka Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dar es Salaam (DAWASA) , Kibaha kuacha kigugumizi na kutoa majibu kuhusu kero ya muda mrefu ya ukosefu wa maji katika Kata ya Viziwaziwa, licha ya kuwepo kwa miundombinu ya maji .
Aidha, amekemea vitendo vya mafundi vishoka wanaowadanganya wananchi kwa kuwaunganisha mabomba kwa njia zisizo halali, hali inayochafua taswira na kuharibu sifa ya DAWASA.
Akizungumza wakati wa ziara yake ya kata kwa kata katika Kata ya Viziwaziwa, Disemba 23, 2025, Dkt. Nicas alisema endapo Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, ataona inafaa kutokana na mamlaka hiyo kukosa majibu ya kero mbalimbali irejeshwe chini ya Manispaa ili kuwabana watendaji wanaojificha kwenye mifumo isiyo na uwajibikaji.
Vilevile, aliwataka wasoma bili za maji kuacha tabia ya kubambikia wananchi bili ilhali hakuna maji.
Meya huyo aliwahimiza watendaji na mafundi waliokabidhiwa dhamana kujitathmini kwa utendaji wao wa kazi na kuhakikisha wanawahudumia wananchi kwa uadilifu.
Kwa mujibu wa Dkt. Nicas, endapo watendaji wanashindwa kutekeleza majukumu yao, waachie ofisi za umma, kwani Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Samia Suluhu Hassan, anataka kuona matokeo ya kazi, hasa wakati serikali ikiendelea na utekelezaji wa mikakati ya siku 100.
Dkt Nicas alimwagiza Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma za Jamii ,kukaa na wahusika wa DAWASA ili waeleze wazi chanzo cha changamoto hizo na hatua zinazochukuliwa.
Katika ziara hiyo, kero nyingine iliyoibuka ni migogoro ya ardhi, ambapo Dkt. Nicas alitoa onyo kali kwa wenyeviti wa serikali za mitaa kuacha mara moja vitendo vya kuuza ardhi na kuchochea migogoro hiyo.
Baadhi ya wananchi akiwemo Andrew Luweneko waliomba Manispaa ichunguze kwa kina utendaji wa DAWASA ili kuondoa migongano na wananchi.
“Tumejichangisha sh. milioni mbili ili kupata maji katika eneo la Dawasa–Kwagoda, DAWASA walileta bomba kutoka kwa Frank, lakini muda umepita hakuna maji,Tulipofukua mabomba tukakuta yamefukiwa bila kuunganishwa, “alielezea Luweneko.
Diwani wa Kata ya Viziwaziwa, Mohammed Chamba, alikiri kuwa changamoto ya maji ni kubwa katika mitaa yote ya kata hiyo.
Aliongeza kuwa mabomba yapo lakini maji hayatoki, hali inayofanya chanzo cha tatizo kutofahamika.
Kwa upande wake, Mhandisi kutoka DAWASA Kibaha, Eleminata Matinde Marwa, alisema Kata ya Viziwaziwa ina miundombinu ya maji inayohudumia takribani asilimia 40 , hali iliyosababishwa na miundombinu hiyo kuzidiwa na ongezeko la watumiaji.
Alieleza kuwa kuna mpango kazi wa mwaka 2025/2026 wa kumaliza kero ya maji kwa kujenga mtandao wa kilomita 38, unaotarajiwa kukamilika ndani ya miezi sita, ambapo hatua ya sasa ni kufanya makadirio ya vifaa na gharama za mradi.
