Waombaji 14,433 wachaguliwa Veta 2026

Dodoma. Waombaji 14,433, miongoni mwao 134 wa elimu ya juu, wamechaguliwa kujiunga na mafunzo katika vyuo vya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (Veta).

Waliochaguliwa ni kati ya waombaji 18,875 waliowasilisha maombi wakitaka kujiunga na mafunzo hayo kwa mwaka 2026.

Mkurugenzi Mkuu wa Veta, Anthony Kasore, ametoa kauli hiyo leo Jumanne, Desemba 23, 2025, alipozungumza na waandishi wa habari.

Amesema mchakato wa uchaguzi umefanyika kwa kuzingatia miongozo na mifumo rasmi ya Serikali.

Kasore amesema kati ya waliochaguliwa, wanaume ni 8,776 na wanawake 5,657 na kwamba waombaji 12,942 wamepangiwa mafunzo ya asubuhi, huku 1,491 wakipangwa masomo ya jioni.

Fani ya umeme imeongoza kuwa na waombaji wengi, wakati uendeshaji mitambo ukiwa na idadi ndogo kuliko fani nyingine katika maombi hayo.

Akizungumzia waombaji wenye ulemavu, Kasore amesema wapo 195 wenye mahitaji maalumu na tayari wamepangwa kujiunga na mafunzo mwakani.

“Kati ya waombaji wenye ulemavu, 145 wamechaguliwa na kupangiwa kujiunga na vyuo 53 vya Veta, huku wengine 50 wakiendelea kusubiri kupangiwa, lakini tunaamini wote watapata nafasi ya kusoma,” amesema na kuongeza:

“Lengo la Serikali ni kuhakikisha kila mwananchi anapata fursa sawa za elimu bila kujali hali ya maumbile, jinsia au kabila. Serikali imeweka mazingira ya kila mmoja kufikia ndoto yake.”

Akizungumza kuhusu wahitimu wa vyuo vikuu, amesema wapo wenye Shahada na Shahada ya Uzamili waliovutiwa kujiunga na mafunzo ya ufundi stadi na tayari wamepangiwa vyuo, ingawa 11 wanasubiri kupangiwa fani na vyuo walivyoomba.

Machi 2025, kuliibuka mjadala kuhusu ushauri alioutoa Kassim Majaliwa, akiwa Waziri Mkuu, kwamba wahitimu wa vyuo vikuu waende kupata ujuzi Veta.

Machi 18, 2025, Majaliwa alieleza mjadala huo una mambo mazuri ya kuishauri Serikali namna ya kuboresha mfumo wa ufundi stadi nchini, akiagiza watendaji kuchukua yaliyo mazuri yanayoshauriwa kupitia mjadala huo.

Akiwa ziarani wilayani Nzega, mkoani Tabora, Majaliwa alizungumzia umuhimu wa Veta kwa wahitimu wa vyuo vikuu na kuibua mjadala mkubwa, uliojengwa kwenye dhana ya usomi na elimu ya Veta.

Mkazi wa Makulu, Iddi Maalim, amesema mafunzo ya ufundi stadi ni suluhisho kwa changamoto ya ajira kwa vijana, kwani yanalenga kuwajengea ujuzi wa moja kwa moja.

Maalim amesema si kila kijana ana nafasi ya kwenda chuo kikuu, hivyo Veta inawasaidia vijana kupata ujuzi wa vitendo unaowawezesha kujiajiri au kuajiriwa haraka.

Kwa upande wake, Asha Hassan, amesema kuwapo kwa idadi kubwa ya wahitimu wa vyuo vikuu na kuchaguliwa ni dalili ya mabadiliko chanya katika mifumo ya kuwaandaa vijana.

Amesema kitendo cha wahitimu wa vyuo vikuu kurudi Veta ni kiashiria kwamba elimu ya mafunzo ya ufundi ni muhimu, hasa kwa vijana, kwani itasaidia kupunguza dhana kwamba ufundi ni kazi ya wasio na elimu pekee.