Ziara ya Dk Mwigulu ilivyoibua kero hekaheka mikoani

Dar es Salaam. Ziara ya siku ya tano ya Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba katika mikoa mitatu imekuwa ya neema kwa wananchi, huku baadhi ya watendaji wa Serikali na makandarasi wakikumbana na wakati mgumu.

Wananchi walipata neema baada ya kupata fursa ya kuwasilisha kero zao kwa Dk Mwigulu aliyezipatia ufumbuzi papo hapo, huku zingine akibeba kwa hatua zaidi.

Hata hivyo, baadhi ya watendaji wa Serikali wameonja joto ya jiwe, baada ya Dk Mwigulu kuwataka kutoa majibu au ufafanuzi wa kina kuhusu utekelezaji wa miradi na kero zilizowasilishwa na wananchi.

Dk Mwigulu alifanya ziara hiyo kwa nyakati tofauti akianzia mkoani Songwe Desemba 17, 2025, kisha Mbeya (Desemba 18), kisha kumalizia mkoani Lindi (Desemba 19 hadi Desemba 21).

Akiwa Mji wa Tunduma mkoani Songwe, Dk Mwigulu aliagiza kuvunjwa kwa ukuta wa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA), uliopo pembezoni mwa Barabara ya Tunduma ili ipatikane nafasi ya upanuzi barabara hiyo. 

Barabara hiyo inayotajwa kubeba uchumi wa Mkoa wa Songwe kwa nyakati tofauti imekuwa ikilalamikiwa kutokana na msongamano wa malori yanayoingia na kutoka nchini.

Sambamba na hilo, akiwa mkoani humo, Dk Mwigulu aliwaonya watumishi na viongozi wa Serikali wasiojali wananchi, akisema watakumbana na fyekeo la kufukuzwa kazi, si kusimamishwa wala kuhamishwa.

Sio hao tu, aliwashukia pia makandarasi wazembe wasiotekeleza majukumu yao kwa uaminifu, ikiwamo kusuasua kwa utekelezaji wa miradi wanayokabidhiwa.

Agizo kama hilo, alilitoa Uyole mkoani Mbeya akiwataka watendaji wa Serikali kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi, ikiwamo kutatua kero zinazowasilishwa na wananchi kwenye ofisi zao bila kujali jinsia wala rika.

Hata hivyo, akiwa wilayani Rungwe mkoani Mbeya, wananchi walitumia mkutano wake wa hadhara kuwasilisha kero mbalimbali ikiwamo uhaba wa maji, umeme, barabara, ushuru, ardhi, mikopo na michango shuleni.

Zingine ni mfumo wa utoaji wa haki, upatikanaji wa huduma bora za afya na maji, ushuru na kufungwa biashara.

Baadhi ya kero zilijibiwa papo hapo huku zingine Dk Mwigulu akiagiza watendaji wake kuzishughulikia haraka.

Katika hatua nyingine, Dk Mwigulu alielekeza mikoa yote nchini kuanzisha vitengo maalumu vya kuchunguza taratibu za ununuzi na BQ badala ya kusubiri mbio za Mwenge wa Uhuru, hatua itakayolinda ustawi wa huduma na matumizi sahihi ya fedha za umma.

Alitoa agizo hilo, akiwa Ruangwa kisema takribani asilimia 70 ya bajeti ya Serikali hutumika kwenye ununuzi na ujenzi, hivyo lazima mifumo ya usimamizi iimarishwe ili kulinda fedha zinazotokana na kodi za Watanzania.

Akiwa Hospitali ya Wilaya ya Nachingwea, Dk Mwigulu aliwabana watalaamu wa afya akiwataka kumweleza kwa kina mchakato wanaotumia kuagiza dawa, sambamba namna wanavyowahudumia wagonjwa.

Dhumuni la Dk Mwigulu kutaka maelezo hayo, ilitokana na changamoto alizokumbana nazo alikopita maeneo mengine kuhusu dawa muhimu kutopatikana,badala yake wagonjwa wanaagizwa kununua nje ya hospitali.

Hata hivyo, akikagua ujenzi wa Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi, Dk Mwigulu aliagiza Wizara ya Afya kuhakikisha vituo vya afya na hospitali zote zinakuwa na dawa muhimu, akisema changamoto hiyo inaleta dosari.

Akizungumzia ziara ya Dk Mwigulu, mchambuzi wa masuala ya siasa, Samson Sombi amesema imekuwa na mchango mkubwa kwa wananchi akisema imeonesha kwa vitendo dhamira ya Serikali kusimamia uwajibikaji na thamani ya fedha za umma.

“Ziara haikuwa ya kawaida ya kusikiliza taarifa pekee, bali ilikuwa ya kuchimba kwa undani na kufichua maovu yaliyokuwa yamejificha kwa muda mrefu chini ya kivuli cha miradi ya maendeleo,” amesema.

Amesema uamuzi Dk Mwiguku kuchukua hatua kali dhidi ya mkandarasi aliyesababisha ucheleweshaji umeonesha wazi Serikali haifumbii macho uzembe, hujuma wala dharau dhidi ya Taifa.

“Hili limeimarisha imani ya wananchi kuwa viongozi wao wako tayari kusimama upande wao. Ziara ya Dk Mwigulu imewasaidia wananchi kwa kufichua maovu, kurejesha heshima ya Taifa na kuimarisha utawala wa sheria, hatua ambayo ni msingi muhimu wa maendeleo endelevu,” ameeleza.