Askofu Ruwa’ichi: Watanzania hawashabikii haki, siyo wadau wa haki

Dar es Salaam. Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Dar es Salaam, Juda Thaddeus Ruwa’ichi, amesema Watanzania wengi hawashabikii haki wala siyo wadau wa haki.

Amesema wengi wao kwa ujinga, kwa kurubuniwa au vinginevyo wamekuwa wadau wa amani akiweka msisitizo kuwa pasipo na haki hakuna amani.

Askofu Ruwa’ichi   ametoa kauli hiyo leo Desemba 24,2025  katika misa maalumu ya mkesha wa Krismasi iliyofanyika katika Kanisa Kuu la Mtakatifu Joseph Jimbo Kuu la Dar es Salaam.

“Sisi tunaoadhimisha Krismasi kuzaliwa kwa mwokozi tunatakiwa kuwa watu wa haki, wewe mwana Dar es Salaam, Mtanzania je, wewe ni mtu wa haki…? Wewe ni mdau wa haki….? Naomba kuthubutu kusema kwamba Watanzania wengi hawashabikii haki siyo wadau wa haki, Watanzania wengi kwa ujinga au kutokujua wanajidai wadau wa amani,” amesisitiza.

Askofu Ruwa’ichi ameeleza kuwa hana ugomvi na mtu anayeshabikia amani lakini akiwakumbusha kuwa haiwezekani kuwepo kwa amani bila haki.

Amesema haki na amani ni vitu viwili vinavyotegemeana na vyote hivyo ni zawadi  inayofunganamana na Yesu mwokozi.

“Ewe Mtanzania kama utaka kujigamba kuwa mtu wa amani jitose kupigania haki, jitose kusema kweli, amani na yanayompendeza Mungu,”amesema. 

Askofu huyo amehitimisha mahuburi hayo akisema Yesu Kristo aliyezaliwa kwa ajili ya wanadamu na anatambulika kwa haki, mwokozi, mwenye upendo na huruma.

Akizungumzia mafundisho hayo muumini wa kanisa hilo, Barnaba Josephat amesema  hitaji la haki ni la msingi kwa binadamu kwa kuwa bila haki hakuna amani.

“Amani msingi wake mkuu ni haki, ukitenda haki amani lazima itakuwepo kwahiyo nimejifunza viongozi wetu wa kiroho wanatutaka kusimamia haki na kutoumiza watu wengine, unaweza kuishi katika utulivu lakini huna amani kwa sababu hujatendewa haki,” amesema.

Kwa upande wake, Lightness Samson amesema katika kusheherekea Sikukuu za Krismasi ni muhimu Watanzania kuendelea kutenda mema pamoja na kutenda haki.

“Tuishi kwa umoja na upendo kwenye jamii tuilinde amani yetu kwa kutenda haki.”