Baresi aanza kazi kimyakimya KMC

KOCHA Abdallah Mohammed ‘Baresi’ ni kama ameanza kazi kimyakimya KMC kwani hivi sasa kuna jambo analifanya chini kwa chini na akikamilisha tu, basi atatangazwa rasmi.

Taarifa zinabainisha KMC ilimalizana na Baresi na kinachofanyika sasa ni kocha huyo ameanza kazi ya kuliunda upya benchi la ufundi kabla ya kutangazwa.

Mmoja wa viogozi wa KMC, aliliambia Mwanaspoti, kocha huyo ambaye anatokea Zimamoto ya Zanzibar, anatarajiwa kuanza kazi wiki ijayo ili kukiandaa kikosi hicho mapema kipindi hiki ligi imesimama.

“Kocha tulishapata ila aliomba nafasi kwanza atengeneze benchi lake la ufundi, anataka kuunda watu anaowaamini na akikamilisha atatujulisha na hapo ndipo tutamtangaza,” kimesema chanzo.

Alipotafutwa Kaimu Afisa Mtendaji Mkuu wa KMC, Daniel Madenyeka aliliambia Mwanaspoti klabu hiyo ipo hatua za mwisho kumtangaza kocha mpya atakayekuja kukibadilisha kikosi kwa ujumla.

“Ni kweli kocha tulishampata na kuna mambo tulikuwa tunamalizia kuyaweka sawa na baada ya hapo wakati wowote kuanzia sasa tutamtangaza rasmi,” alisema.

Baresi anatua KMC kurithi nafasi ya kocha Marcio Maximo ambaye aliifundisha timu hiyo kwa kipindi cha miezi minne na kufikia makubaliano ya pande mbili kusitisha mkataba Desemba 6, 2025 baada ya kikosi hicho kusalia mkiani mwa msimamo wa Ligi Kuu Bara kikiwa na pointi nne katika mechi tisa ilizocheza.