WAKATI Ligi Kuu Bara ikiwa kwenye mapumziko kupisha Fainali za Kombe la Mataifa Afrika (AFCON) 2025 zinazofanyika Morocco, makipa Erick Johora wa Mashujaa, Omary Gonzo (JKT Tanzania) na Costantine Malimi (Mtibwa Sugar) wanaongoza kwa cleansheet nyingi msimu huu.
Johora ndiye kinara akiwa na cleansheet sita katika mechi tisa ambazo Mashujaa imecheza, kwa upande wa Gonzo, JKT ikicheza mechi 10, anazo cleansheet nne sawa na Malimi ambaye Mtibwa ina mechi nane.
Licha ya kikosi cha Mtibwa Sugar kutokuwa na matokeo mazuri kwenye ligi hiyo, lakini Malimi ameonyesha ubora mkubwa na kuwa miongoni mwa makipa walioruhusu mabao machache kwenye ligi hiyo msimu huu.
Akizungumza na Mwanaspoti, Malimi alisema ni jambo jema ameuanza msimu kwa mwendelezo bora aliotoka nao Ligi ya Championship alipoibuka kipa bora.
Alisema kiwango hicho na takwimu hizo zinampa nguvu ya kuendelea kupambana ili amalize na rekodi nzuri, huku akihitaji kumaliza miongoni mwa makipa bora pamoja na Djigui Diarra wa Yanga, Moussa Camara (Simba) na wengineo.
“Takwimu hizi zinanipa imani na kujiona naweza kufanya zaidi ya nilichokifanya Championship, naamini inawezekana kama nikijituma na kuboresha uwezo wangu,” alisema Malimi na kuongeza.
“Malengo yangu ni kuhakikisha naipambania timu pia napambania carrier (kazi) yangu niweze kufika mbali, lakini kwanza timu ifanye vizuri.”