AZAM inalitaka Kombe la Mapinduzi na kuhakikisha hilo linatimia, mastaa wa timu hiyo ambao wameanza mazoezi juzi wamefichua jambo.
Kikosi hicho chenye rekodi ya kubeba ubingwa wa Kombe la Mapinduzi mara nyingi zaidi (tano), juzi kilirudi mazoezini kuanza kujiandaa na michuano hiyo itakayoanza Desemba 28, mwaka huu kwenye Uwanja wa New Amaan Complex, Zanzibar.
Unaambiwa kwenye mazoezi hayo ya kwanza, Kocha wa Azam, Florent Ibenge amewapa hesabu hizo mastaa wake akiwaambia wanakwenda kwenye mashindano ya Mapinduzi na kila mechi wataicheza kwa akili kubwa bila kumchulia poa mpinzani.
Mmoja wa mabeki wa Azam, aliliambia Mwanaspoti, Ibenge anataka taji hilo liende viunga vya Azam Complex, huku akiwataka wachezaji ambao hawakupata nafasi kwenye mechi za mashindano msimu huu kujipanga sawasawa kuonyesha uwezo wao.
“Kocha anataka twende tukachukue hili Kombe la Mapinduzi, ametuambia hatutakiwi kuidharau mechi yoyote kama tunataka kufikia malengo,” alisema beki huyo.
Akizungumzia michuano hiyo ambapo Azam imepangwa kundi A ikitarajiwa kuanza dhidi ya URA ya Uganda, Ibenge alisema kila mashindano Azam inayokwenda kushiriki, hesabu ya kuchukua ubingwa ipo.
“Azam ni timu kubwa, hakuna shindano tunakwenda bila malengo ya kuchukua ubingwa, ni kweli nataka kila mchezaji kuwa tayari, kama hukupata nafasi kwenye ligi na mechi za CAF, hii ni sehemu ya kuonyesha uwezo wako kama mchezaji.
“Kama ninavyosema kila wakati nina wachezaji wazuri sana hapa, muhimu ni kila mtu kushindana ili kupata nafasi, tunataka kila mchezaji awe na akili ya namna hiyo,” alisema Ibenge.
