Kilimanjaro mguu sawa, utekelezaji bima ya afya kwa wote

Moshi. Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dk Jairy Khanga, amewataka wataalamu na watoa huduma za afya mkoani humo kuanza mara moja utekelezaji wa majaribio ya bima ya afya kwa wote kwa maelekezo ya Serikali.

Amewataka kujikita katika utoaji wa elimu, uhamasishaji na maandalizi ya vituo vya kutolea huduma, ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora na endelevu.

Dk Khanga ametoa rai hiyo leo Jumatano, Desemba 24, 2025 wakati wa kikao kazi cha uhamasishaji wa bima ya afya kwa wote, ambapo amesema maelekezo hayo yanatokana na agizo la Rais Samia Suluhu Hassan la kuanza utekelezaji wa majaribio ndani ya siku 100 kwa makundi maalumu wakiwemo wajawazito, wazee, watu wenye ulemavu na watoto.

Kikao hicho kimewakutanisha watoa huduma za afya kuanzia ngazi ya usimamizi wa mkoa hadi ngazi ya vituo, ikiwemo timu za uendeshaji wa huduma za afya za halmashauri zote saba za mkoa huo, waganga wafawidhi wa hospitali za wilaya, vituo vya afya, zahanati pamoja na hospitali ya rufaa ya mkoa.

Kwa mujibu wa Dk Khanga, lengo la kikao hicho lilikuwa ni kuwajengea uelewa wa pamoja wataalamu na watoa huduma kuhusu sheria ya bima ya afya kwa wote, dhana yake na namna itakavyotekelezwa, ikiwemo kitita muhimu cha mafao kitakachotumika kuanzia ngazi ya msingi hadi hospitali ya wilaya.

Dk Khanga amebainisha kuwa tayari wameandaa mkakati maalumu kuhakikisha ifikapo Januari, 2026, Mkoa wa Kilimanjaro unaanza utekelezaji wa majaribio ya bima ya afya kwa wote, na hivyo kuwataka wataalamu na watendaji wa afya kuanzia ngazi ya msingi hadi mkoa kukamilisha maandalizi ya vituo vya kutolea huduma kwa kuhakikisha upatikanaji wa dawa, vifaa tiba na vitendanishi vya kutosha.

“Niwaelekeze wote muende mkakamilishe maandalizi ya vituo vya kutolea huduma za afya kwa maana ya zahanati, vituo vya afya, hospitali za wilaya, mkoa kuwa tayari kutoa huduma za bima ya afya kwa wote,” amesema Dk Khanga.

Katika maelekezo yake, Dk Khanga pia amewasisitiza watoa huduma kuzingatia utoaji wa huduma kwa upendo na weledi, huku wakiheshimu misingi ya huduma kwa mteja, akisisitiza kuwa mteja ni mfalme.

“Lakini pia niwaelekeze Mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya (NHIF) kutoa vitendea kazi vitakavyorahisisha uandikishaji wa wanachama katika maeneo yote ya mkoa ili utekelezaji kwa hayo makundi maalum uweze kuanza,” amesisitiza Dk Khanga.

Kuhusu mifumo ya Tehama, Dk Khanga amesema usimikaji umefikia asilimia 90 mkoani humo, huku vituo 32 vilivyobaki vikitarajiwa kukamilishwa ifikapo Januari 2, 2026 na kuhakikishia kuwa kufikia tarehe hiyo vituo vyote vitakuwa tayari kuanza utekelezaji wa bima ya afya kwa wote.

“Lakini jambo lingine muhimu ni suala la usimikaji wa mifumo ya Tehama katika vituo vya kutolea huduma za afya. Mkoa wa Kilimanjaro usimikaji wa mifumo ya Tehama umefika asilimia 90, tunadaiwa asilimia 10 ambayo ni sawa na vituo 32.”

“Sasa tumekubaliana ifikapo Januari 2, 2026 mifumo yote iwe imesimikwa katika vituo vyote na iwe inatumika. Na niwahakikishie ukifika wakati huo vituo vyote vitakuwa tayari kwa kuanza utekelezaji wa bima ya afya kwa wote,” amesema

Amesema mwananchi mwanachama atalipia Sh150,000 kwa mwaka, kiasi kitakachohudumia kaya moja yenye watu sita mzazi mmoja na wategemezi wanne wenye umri chini ya miaka 21, na hivyo kutoa uhakika wa kupata matibabu bila kikwazo cha malipo ya papo kwa papo.

Amesisitiza kuwa bima ya afya kwa wote ni ya lazima kwa kila Mtanzania, tofauti na ilivyokuwa awali, akieleza kuwa hatua hiyo inalenga kumhakikishia kila mwananchi upatikanaji wa matibabu wakati wowote bila kujali uwezo wa kifedha.

Meneja wa NHIF Mkoa wa Kilimanjaro, Dk Fikirini Mkwabi amesema wanaendelea kutoa elimu kwa makundi mbalimbali katika jamii ili kujenga uelewa kuhusiana na bima ya afya ili kuwawezesha wananchi wote kuona umuhimu wa kukata bima ya afya kabla ya kuugua.

Wakizungumza baadhi ya wananchi mkoani Kilimanjaro, wamesema bima ya afya kwa wote itakuwa na manufaa makubwa kwa wananchi kutokana na kwamba wengi wamekuwa wakishindwa kumudu gharama za matibabu za papo kwa papo pindi wanapougua.

“Wote tunafahamu ugonjwa haupigi hodi na wananchi wengi hawana kipato ambacho kitawawezesha kupata huduma za afya wakati wote wanapougua, lakini bima itamhakikishia kupata matibabu kwa uhakika hata kama hana kipato,” amesema Rose Noel mkazi wa Moshi.