Kulandana atabiriwa kuibeba Mbeya City

SIKU chache baada ya kuripotiwa kutua Mbeya City kuelekea usajili wa dirisha dogo utakaofunguliwa Januari Mosi 2026, kiungo Abdallah Yasin Kulandana ametabiriwa kufanya vizuri akiwa na kikosi hicho katika mechi zilizosalia msimu huu 2025-2026.

Hayo yamesemwa na mchezaji wa zamani wa Mbeya City, Abasirim Chidiebere aliyeonyesha kuwa na imani na uwezo wa mchezaji huyo kutokana na kiwango alichokionesha akiwa Fountain Gate.

“Ni mchezaji mwenye akili kubwa ya mpira, nililiona hilo wakati akiwa na Fountain, ana uwezo wa kusaidia timu kujilinda na kushambulia,” alisema Chidiebere.

Chidiebere aliyewahi kucheza Stand United na Coastal Union, aliongeza, Mbeya City imefanya uamuzi sahihi kumnasa Kulandana kipindi hiki, akisisitiza uzoefu wake wa ligi utakuwa msaada mkubwa kwa timu hiyo wakati msimu ukiendelea.

“Katika kipindi hiki ambacho ligi iko katikati na ushindani ni mkubwa, unahitaji wachezaji wanaoelewa mazingira ya ligi na Kulandana ana hilo,” aliongeza.

Mbeya City ambayo ipo nafasi ya 13 katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi nane, imemchukua kiungo huyo kama mchezaji huru baada ya kuvunja mkataba wake na klabu ya Fountain Gate.

Kukamilika kwa usajili huo kunatajwa kuwa nyongeza muhimu kwa Mbeya City katika kujiimarisha ikiwa ni siku chache baada ya kumtambulisha kocha Mecky Maxime akichukua nafasi ya Malale Hamsini.