Kupanda kwa bei za bidhaa mbalimbali nchini kumeathiri kwa kiasi kikubwa biashara za msimu wa sikukuu, huku wafanyabiashara wa miti na mapambo mengine ya Krismasi wakilalamikia uhaba wa wateja.
Wafanyabiashara hao wamesema tofauti na miaka iliyopita nyakati kama hizi ambazo mauzo yalikuwa makubwa, msimu huu umekuwa tofauti kutokana na hali ya uchumi na mabadiliko ya tabia za wanunuzi.
Miongoni mwa biashara zilizokosa nguvu msimu huu ni pamoja na miti ya Krismasi na mapambo ambayo hayakununuliwa kama miaka ya nyuma.
Akizungumza na Mwananchi leo Desemba 24, 2025, mfanyabiashara wa mapambo Kariakoo, Monika Yohana, amesema miaka ya nyuma watu walijitokeza kwa wingi kufanya manunuzi, lakini mwaka huu idadi ya wateja imepungua kwa kiasi kikubwa.
“Mwaka huu hali ya biashara siyo nzuri kama mwaka jana; mazingira yamekuwa magumu kidogo na watu hawajitokezi kwa wingi kama ilivyokuwa awali,” amesema Monika. Amesema moja ya changamoto ni watu kuogopa kuingia katikati ya mji, hali inayosababisha biashara nyingi kukosa wateja.
Muuza miti ya asili ya Krismasi Msasani, Richard Mshama (maarufu kama Hovyo Hovyo), amesema kiwango cha mauzo kimeshuka hadi asilimia 40 kutokana na ongezeko la miti ya bandia. “Zamani ukifika msimu wa Krismasi na Mwaka Mpya, nilikuwa nauza miti karibu 100 au zaidi, lakini mwaka huu nimenunua miti 80 na nimeuza mitano tu,” amesema.
Wakati wafanyabiashara wa mapambo wakilalamika, upande wa vyakula bei zimekuwa zikipanda na kushuka hadi kufikia Desemba 24. Ikumbukwe katika jiji la Dar es Salaam, kipindi cha Desemba 8 hadi 9, bei ya nyama ilipanda hadi kufika Sh18,000 kwa kilo mtaani, wakati kwenye machinjio iliuzwa kwa bei ya jumla kati ya Sh14,000 kwa daraja la kwanza na Sh12,000 kwa daraja la pili.
Mfanyabiashara wa kitoweo hicho katika machinjio ya Vingunguti, Joel Meshack, amesema kwa sasa nyama daraja la kwanza inauzwa Sh10,000 huku ile ya daraja la pili ikiuzwa kwa Sh8,000 kwa kilo moja. Naye mfanyabiashara wa machinjio ya Kimara Suka, Issaya Zakaria, amesema kilo ya nyama kwa sasa wanauza Sh12,000, bei ambayo ilikuwepo awali, japo Desemba 8 kuelekea 9 ilipanda na kufika Sh15,000.
“Ng’ombe nanunua kati ya Sh1.7 milioni hadi Sh1.8 milioni kwa wenye uzito mkubwa, na uzito wa kati wanauzwa Sh700,000 hadi Sh1 milioni,” amesema Meshack.
Mtaani, bei ya rejareja inacheza kati ya Sh12,000 hadi Sh14,000 kwa maeneo ya Tabata, huku Chanika ikiwa ni Sh12,000 hadi Sh13,000 na Mbezi ni Sh13,000 hadi Sh14,000. Kwa upande wa kuku wa kisasa, maeneo mengi bei ya jumla imesalia Sh6,500, huku rejareja ikiwa kati ya Sh7,500 hadi Sh8,000. K
uku wa kienyeji wanauzwa kati ya Sh20,000 hadi Sh30,000 na mbuzi kilo moja ni Sh14,000. Samaki aina ya sato wanauzwa kati ya Sh15,000 hadi Sh16,000, huku sangara wakiuzwa kati ya Sh13,000 na Sh14,000.
Katika soko la mchele jijini Dar es Salaam na Iringa, bei imepanda kutoka Sh2,300 hadi Sh3,500 katika maeneo tofauti.
Mfanyabiashara wa soko la Tandale, Hemed Hussein, amesema bei hizo zimepanda kutoka Sh2,000 hadi Sh2,200 kutokana na ufikishwaji wa zao hilo sokoni kuwa mdogo.
Naye mfanyabishara wa nafaka wa Halmashauri ya Manispaa ya Iringa, Aloyce Mgaya, amesema mchele “supa” umepanda kutoka Sh2,600 hadi Sh3,500. Katika masoko ya Kihesa, Mlandege, na Soko Kuu la Iringa, bidhaa kama viazi, vitunguu, karoti, nyanya, tangawizi, mchele na mafuta ya kula vimepanda bei ikilinganishwa na mwezi uliopita.
Mfanyabiashara Emmanuel Tishu amesema bei ya viazi imepanda kutoka Sh60,000 hadi Sh100,000 kwa gunia.
Katika soko la Mabibo, Dar es Salaam, Masoud Fahamu amesema karoti zimepanda kutoka Sh30,000 hadi Sh140,000, wakati pilipili hoho imeshuka kutoka Sh250,000 hadi Sh90,000. Kwa upande wa vitunguu mkoani Iringa, bei ya gunia imepanda kutoka Sh90,000 hadi Sh150,000.
Mkoani Simiyu, bei za vyakula zimepanda katika masoko mbalimbali kama Bariadi na Maswa, ambapo mchele unauzwa kati ya Sh2,500 hadi Sh3,200 kwa kilo. Nyama ya ng’ombe imeongezeka kutoka Sh12,000 hadi Sh14,000.
Bidhaa nyingine zilizopanda ni viazi mviringo (kutoka Sh1,200 hadi Sh1,500), sukari (kutoka Sh3,000 hadi Sh3,500), na unga wa sembe (kutoka Sh2,000 hadi Sh2,500). Mkazi wa Maswa, Neema Masota, amesema hali hiyo imewashitua na kuathiri maandalizi yao ya sikukuu.
Mkoani Mbeya, plastiki ya kilo 20 ya mchele ambayo awali ilikuwa Sh35,000 sasa imepaa hadi Sh60,000. Nyama imepanda hadi Sh14,000 na mafuta ya kupikia ni Sh6,000 kwa lita.
Mfanyabiashara Rehema Joel ameeleza kuwa kupanda huku kunasababishwa na mwingiliano wa wafanyabiashara wakubwa wanaofuata bidhaa kwa wakulima na kupandisha bei ya ununuzi.
Jijini Dodoma, bei ya nyama imepanda kutoka Sh10,000 hadi Sh12,000. Mmiliki wa mabucha, Mnyausi Njamasi, amesema hali hiyo inatokana na changamoto ya upatikanaji wa ng’ombe wenye ubora kutokana na ukame wa malisho na maji.
Imeandikwa na Nasra Abdallah, Mariam Mbwana, Devotha Kihwelo (Dar) Samwel Mwanga, (Simiyu), Hawa Mathias (Mbeya) na Habel Chidawali.
