Menejimenti Temesa kikaangoni | Mwananchi

Dar es Salaam. Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, ameagiza kufutwa kazi na kufikishwa katika vyombo vya sheria kwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Ufundi na Umeme Tanzania (Temesa), Lazaro Kilahala, na menejimenti ya wakala huo kutokana na tuhuma za ubadhilifu wa zaidi ya Sh2.5 bilioni.

Agizo hilo la Dk Mwigulu linakuja wiki mbili baada ya Waziri wa Ujenzi, Abdallah Ulega, kuagiza kusimamishwa kazi kwa mtendaji mkuu huyo na watendaji wengine baada ya ripoti ya taarifa ya fedha kubainisha ubadhilifu wa kiasi hicho cha fedha.

Katika ziara yake ya Desemba 7, mwaka huu, Magogoni jijini Dar es Salaam, Ulega alisema ripoti ya taarifa ya fedha ya wakala huo imebainisha kutoonekana kwa Sh2.5 bilioni, ambazo alidai kumefanyika ubadhilifu.

Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, akifanya ukaguzi leo Desemba 24, 2025 katika shughuli za usafiri katika eneo la Magogoni, jijini Dar es Salaam. Picha na Ofisi.

Hata hivyo, Mwananchi iliwahi kufanya uchunguzi katika huduma za vivuko na utendaji wa wakala huo na kuonesha uzembe wa kiutendaji unavyokwamisha matengenezo ya vivuko, huku vingine vikikwama Mombasa, nchini Kenya, kwa mwaka wa tatu sasa.

Dk Mwigulu ametoa maelekezo hayo leo, Jumatano, Desemba 24, 2025, alipofanya ziara ya kukagua hali ya shughuli za usafiri katika eneo la Magogoni, jijini Dar es Salaam, kunakotolewa huduma za vivuko.

Amemtaka Ulega kumwelekeza Katibu Mkuu wa wizara hiyo kuwafuta kazi na kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria Mtendaji Mkuu wa Temesa na menejimenti ya wakala huo kutokana na ubadhilifu huo.

“Ili kivuko kifanye kazi tunahitaji Sh800 milioni, tumeikosa fedha hiyo, halafu tuliowapa dhamana wamekwapua Sh2.5 bilioni. Haya ndiyo mambo yanayosababisha huduma iwe mbovu.

“Wananchi wetu tunawatoza nauli kubwa, halafu watumishi wetu wamegawana Sh2.5 bilioni. Waziri, uchukue hatua zaidi,” Waziri Mkuu ametoa madai hayo.

Ametaka uchunguzi huo ufanywe kwa kina, kwa kuwa kuna madai vivuko hivyo vinatengenezewa mazingira ya kuharibika ili watu wapige kile alichokiita ‘dili’ wakati wa matengenezo.

Dk Mwigulu amesema bila umakini, Serikali itajikuta inatengeneza kivuko kwa bei kubwa zaidi ya gharama ya kutengeneza kipya.

Hata hivyo, kauli hiyo ya Dk Mwigulu inaakisi mjadala uliowahi kuibuka kuhusu matengenezo ya kivuko cha MV Magogoni nchini Kenya. Gharama za matengenezo ya kivuko hicho ilikuwa Sh7.5 bilioni, huku gharama ya ununuzi wa kivuko chenyewe ni Sh8 bilioni.

“Vyombo husika vichukue hatua kwa wahusika, haya mambo ya kutoheshimu fedha za umma, kutokuwa na huruma kwa Watanzania lazima yafike mwisho,” amesema.

Amesema ubadhilifu uliofanyika ni sawa na watendaji hao kugawana vivuko pamoja na kuiba nauli zinazotolewa na wananchi.

Kwa kuwa uchunguzi uliobaini ubadhilifu wa fedha hizo umefanywa na wataalamu kutoka idara mbalimbali za Serikali, Dk Mwigulu amesema hakuna haja ya kuchunguza zaidi, bali wahusika wafutwe kazi na kupelekwa mahakamani.

Waziri Mkuu, Dk Mwigulu Nchemba, akifanya ukaguzi leo Desemba 24, 2025 katika shughuli za usafiri katika eneo la Magogoni, jijini Dar es Salaam. Picha na Ofisi.

“Katibu Mkuu aelekezwe awafukuze kazi mara moja, na vitengo vinavyohusika viwapeleke kwenye vyombo vya sheria,” amesema mtendaji mkuu huyo wa Serikali.

Pia, amemuagiza Ulega afanye mawasiliano na Wizara ya Fedha kuhakikisha fedha za malipo ya utengenezaji wa vivuko zinatolewa kwa wakati ili ukarabati ukamilike na vivuko vitoe huduma.

Serikali ina vivuko vitatu (MV Kazi, MV Magogoni na MV Kigamboni) katika eneo la Kivukoni/Kigamboni, lakini kinachofanya kazi ni MV Kazi pekee.

Kwa upande wake, Kaimu Mtendaji Mkuu wa Temesa, Moses Mabamba, amesema Serikali inamiliki vivuko vitatu kwa ajili ya Kivukoni na Kigamboni, ambapo kwa sasa kinachotoa huduma ni kimoja tu, cha MV Kazi, huku kivuko cha MV Magogoni kikiwa kwenye matengenezo Mombasa tangu 2023.

Amesema matengenezo hayo, ambayo yanagharimu takribani Sh7.5 bilioni, yamefikia asilimia 70, huku kivuko kingine cha MV Kigamboni kikiwa katika matengenezo kwenye kampuni ya Songoro Marine, Kigamboni.

“…Kabla ya kuharibika kwa vivuko hivyo tulikuwa na uwezo wa kukusanya Sh20 milioni 20 kwa siku, ila kwa sasa tunakusanya Sh3.61 milioni hadi shilingi milioni nne,” amesema.

Naye, Mkurugenzi wa Uhusiano na Mawasiliano wa Bakhresa Group, ambao wameingia ubia na Serikali kutoa huduma ya vivuko, Hussein Sufian, amesema walianza kutoa huduma mwanzoni mwa mwaka huu baada ya vivuko vya Serikali kupata hitilafu, wakaanza na vinne na sasa vipo nane, kila kimoja kikiwa na uwezo wa kubeba watu 200.

Amesema awali walikuwa wakisafirisha abiria 20,000 kwa siku, na sasa wanasafirisha kati ya 50,000 hadi 100,000 kutokana na wingi wa abiria, na wanakusudia kuongeza kivuko kingine ili kukidhi mahitaji. Vivuko hivyo, amesema, vinatumia muda wa dakika tano hadi 10, ikitegemea hali ya bahari.