Dar es Salaam. Afrika ni bara lenye historia ndefu ya mapambano ya ukombozi dhidi ya ukoloni, lakini pamoja na hatua zilizopigwa katika kujenga mshikamano wa kisiasa na kiuchumi, bado linaendelea kukumbwa na changamoto kubwa za kisiasa na kijeshi.
Hali hii imeendelea kuwapo licha ya kuanzishwa kwa Umoja wa Afrika (AU) na jumuiya mbalimbali za kikanda zilizolenga kuimarisha umoja, kulinda maslahi ya bara na kutatua migogoro ya ndani kwa njia za Kiafrika.
Baada ya mataifa mengi ya Afrika kupata uhuru mwanzoni mwa miaka ya 1960, wazo la kuunda jumuiya za kikanda lilichukuliwa kama mkakati wa kuimarisha mshikamano na ushirikiano.
Ndipo zikaanzishwa jumuiya kama Umoja wa Afrika (AU), Jumuiya ya Kiuchumi ya Mataifa ya Afrika Magharibi (ECOWAS), Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Soko la Pamoja la Nchi za Kusini na Mashariki mwa Afrika (COMESA) pamoja na Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC).
Lengo la jumuiya hizi lilikuwa wazi; kuimarisha sauti ya Afrika katika siasa za dunia, kukuza uchumi wa pamoja, kulinda heshima ya bara na muhimu zaidi, kuzuia na kutatua migogoro ya ndani.
Hata hivyo, kwa miaka mingi, Afrika imekuwa ikikosolewa kwa kushindwa kuonesha uwezo wa kumaliza migogoro yake bila msaada wa mataifa ya nje.
Udhaifu huu umeacha mwanya kwa mataifa ya Magharibi na jumuiya za kimataifa kuingilia migogoro ya Afrika, mara nyingine kwa nia ya kusaidia, lakini mara nyingi kwa maslahi yanayodhoofisha uhuru na mamlaka ya bara.
Ndoto ya Afrika yenye nguvu, umoja na uhuru kamili bado imekuwa ikikumbwa na changamoto nyingi. Migogoro ya kisiasa imeendelea kushamiri, vita vya wenyewe kwa wenyewe havijaisha katika baadhi ya nchi, na siasa za kijeshi zimeendelea kujijenga katika mataifa kadhaa.
Katika hali hii, AU na jumuiya za kikanda zimekuwa zikilaumiwa kwa kutoa matamko yasiyo na nguvu ya utekelezaji, hali inayowafanya wananchi na wanaharakati kuzitaja kama taasisi zisizo na meno.
Tangu enzi za waasisi wa uhuru wa Afrika, viongozi walisisitiza umuhimu wa umoja wa kweli wa bara. Hayati Mwalimu Julius Nyerere aliwahi kusema kuwa tatizo la Afrika si ukosefu wa rasilimali, bali ni ukosefu wa mshikamano na uongozi thabiti.
Kauli hiyo bado inaakisi hali ya sasa, ambayo migogoro mingi inaendelea na mataifa ya Afrika hulazimika kutegemea Ulaya na Marekani kuingilia kati.
Mifano ya misukosuko ya kisiasa na kijeshi ni mingi. Nchi kama Mali, Burkina Faso, Guinea, Niger na Madagascar zimekumbwa na mapinduzi ya kijeshi katika miaka ya karibuni, hali inayoonesha udhaifu wa taasisi za kidemokrasia na kushindwa kwa jumuiya za kikanda kuzuia au kudhibiti hali hiyo mapema.
Sudan imeendelea kuwa mfano wa wazi wa mapigano ya madaraka yaliyoigharimu nchi hiyo maelfu ya maisha na kuwalazimisha mamilioni ya raia kuyahama makazi yao.
Vivyo hivyo, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imekuwa katika vita vya muda mrefu licha ya juhudi za AU na SADC.
Somalia pia imeendelea kutajwa kama kielelezo cha kushindwa kwa jumuiya za Afrika kuleta amani ya kudumu, hali inayolazimisha utegemezi mkubwa wa vikosi vya kimataifa na msaada wa Magharibi. Katika migogoro hii yote, AU na jumuiya zake zimeonekana kuchelewa kuchukua maamuzi, na hata yanapotolewa, utekelezaji wake umekuwa dhaifu.
ECOWAS imejaribu kuingilia mapinduzi ya kijeshi Afrika Magharibi, lakini mara nyingi imekumbana na upinzani wa ndani na ukosefu wa rasilimali. SADC nayo imeshindwa kumaliza migogoro kama ya Zimbabwe katika miaka ya nyuma na mzozo wa muda mrefu wa DR Congo. Udhaifu huu umeimarisha hoja kwamba Afrika bado haina uwezo wa kujisimamia kikamilifu katika masuala ya amani na usalama.
Kutokana na hali hiyo, mataifa ya nje na jumuiya za kimataifa kama Umoja wa Mataifa (UN) zimeendelea kuwa kimbilio la mwisho katika migogoro ya Afrika.
Marekani, Ufaransa na Uingereza mara nyingi huingilia kwa kupeleka vikosi vya kulinda amani au kutoa misaada ya kifedha. Hata hivyo, misaada hiyo mara nyingi huambatana na masharti yanayoibua maswali kuhusu uhuru wa kisiasa na kiuchumi wa mataifa ya Afrika.
Kwa mujibu wa wanasiasa na wachambuzi, tatizo kubwa ni kushindwa kwa jumuiya za Afrika kuweka mifumo ya mapema ya kudhibiti viashiria vya migogoro.
Luhaga Mpina, mwanachama wa ACT-Wazalendo, amewahi kusema jumuiya hizo husubiri matatizo yatokee ndipo zijitokeze kukemea, badala ya kushughulikia chanzo cha migogoro.
Wachambuzi wa diplomasia, akiwemo Denis Konga, wanasema ukosefu wa rasilimali, uchumi dhaifu na kukosekana kwa utashi wa kisiasa miongoni mwa viongozi wa Afrika ni vikwazo vikuu vinavyolifanya bara kutegemea mataifa ya nje. Aidha, baadhi ya mataifa yenye uchumi imara hayatoi mchango wa kutosha katika kuimarisha bara kwa ujumla, badala yake huangalia zaidi maslahi ya nje.
Kwa mtazamo wa Profesa Issa Shivji, tatizo la msingi ni kukosekana kwa umoja wa kweli wa Waafrika.
Anasisitiza kuwa Afrika ina taasisi ya Umoja wa Afrika, lakini haina umoja wa dhati wa kutetea maslahi ya bara kwa pamoja.
Hatimaye, mustakabali wa Afrika utategemea kama viongozi na wananchi wake wataamua kujenga umoja wa kweli, kuheshimu maamuzi ya jumuiya zao na kuwekeza katika taasisi za Kiafrika.
Bila mshikamano huo, ndoto ya Afrika kujisimamia na kuwa na sauti yenye nguvu katika dunia itaendelea kuwa changamoto isiyokwisha.
