Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma, Brigedia Jenerali Ahmed Abbas Ahmed, ameagiza zao la soya litumike kikamilifu katika mpango wa chakula mashuleni kama njia ya kupunguza udumavu na kuboresha afya ya watoto.
Akizungumza katika kikao kazi cha mkakati wa kuendeleza zao la soya, RC Ahmed Abbas Ahmed amesema matumizi ya vyakula na maziwa ya soya katika shule zote za mkoa yataimarisha lishe na uwezo wa kujifunza kwa wanafunzi.
👉 Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi wa Halmashauri wameelekezwa kuhakikisha chakula kinachotokana na soya kinaingizwa rasmi kwenye mpango wa chakula mashuleni.
👉 Maafisa Kilimo wameagizwa kuhamasisha wakulima kuongeza uzalishaji wa zao la soya.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kanda ya Kusini wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), Bi. Agnes Kimaro, alikabidhi kilo 1,000 za mbegu za soya kama mbegu mama kwa Mkoa wa Ruvuma, hatua inayolenga kupunguza changamoto ya upatikanaji wa mbegu bora kwa wakulima.
Bi. Kimaro alisema upatikanaji wa mbegu bora utawezesha mkoa kufikia lengo la kuongeza uzalishaji wa zao la soya kutoka tani elfu tano za sasa hadi tani elfu hamsini kwa mwaka ifikapo 2030.
Aliongeza kuwa COPRA ina jukumu la kusimamia mazao mchanganyiko yasiyo na bodi, ikiwemo kusimamia kilimo cha mkataba kati ya mkulima na mnunuzi wa mazao.
“Kwa mujibu wa sheria, COPRA ndiyo msimamizi wa kilimo cha mkataba, ambapo mkulima na mnunuzi wanapaswa kujisajili, na mkataba kuwa wazi kwa taasisi zote za serikali ikiwemo Ofisi ya Mkuu wa Mkoa na Wilaya,” alisema Bi. Kimaro.
Pia Agnes Kimario aliendelea kutoa elimu kwa wadau hao juu ya umuhimu wa wakulima kutumia mifumo rasmi ya mauzo ya mazao yao ikiwemo mfumo stakabadhi za ghala.
COPRA pia ilitoa kilo 2,772 za mbegu za Ufuta kwa mkoa wa Ruvuma ambazo zitolewe kwa ruzuku ya bure lengo ni kuhamasisha wakulima kutumia mbegu bora.
Naye Katibu Mtendaji mkuu MCODE Ahsante Zenda alisema kikao kazi hicho ni fursa muhimu kwa wakulima na wadau wa kilimo kuelewa thamani ya zao la soya katika kuboresha maisha ya wananchi.
Kikao kazi hicho kilihusisha wadau mbalimbali wakiwemo COPRA, PASS, MCODE na AGCOT, ikiwa ni sehemu ya jitihada za serikali ya Mkoa wa Ruvuma kuboresha lishe, afya na uchumi wa wananchi wake.
.jpeg)

.jpeg)

