WINGA wa zamani Yanga, Mahlatse Makudubela ‘Skudu’ amesema Simba imefanya uamuzi sahihi kumchukua Steve Barker kama kocha wa kikosi hicho, lakini kuna ‘code’ amewatembezea mapema mastaa wa kikosi hicho kama wanataka nafasi ya kucheza akiwemo Elie Mpanzu, Jonathan Sowah na Jean Charles Ahoua.
Skudu raia wa Afrika Kusini, amewahi kunolewa na kocha huyo katika timu ya University of Pretoria ya Sauzi na aliitumikia kwa muda mfupi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Skudu alisema Simba ilifanya uamuzi sahihi kumchukua kocha huyo kwani atakwenda kuisaidia hasa katika michuano ya kimataifa.
Alisema Barker ni kocha anayetaka wachezaji wenye nguvu, ‘professional’, wenye uwezo wa kuipigania timu na nidhamu uwanjani.
“Unaweza ukaona rekodi yake sio kocha ambaye amezifundisha timu kubwa, lakini zina uwezo wa kupata matokeo mazuri kutokana na mbinu zake za ufundishaji.
“Simba kumchukua Steve Barker ni uamuzi sahihi na imepata kocha mzoefu anayejua soka la Afrika, lakini wachezaji wanatakiwa kujiandaa na maisha ya Barker kwani ni kocha anayetaka kufanya mambo kwa weledi mkubwa.
“Ana mbinu nyingi na kwa ubora wa wachezaji wa Simba atabadilisha mambo katika kikosi hicho ambacho kinashiriki michuano ya kimataifa na kusaka ubingwa wa ligi ambao hawajaupata kwa muda mrefu.”
Aliongeza: “Ni kocha ambaye wakati wote anataka kushinda ubingwa wa Ligi na mashindano makubwa, baada ya kufanya vizuri na Stellenbosch, sasa ni wakati wa Simba kuona ufundi wake.
“Kwa wachezaji wakitaka kupenya kwenye kikosi chake lazima uwe mbunifu, mwenye nidhamu, nguvu na uwezo mkubwa uwanjani ili kuisaidia timu kupata matokeo mazuri.”
Kutokana na mambo hayo anayoyaangalia zaidi Barker kwa nyota wake, ni wazi mastaa wa Simba watakuwa na kazi kubwa ya kufanya ili kulinda nafasi zao katika kikosi cha kwanza.
Nyota kama Mpanzu, Sowah, Kibu Denis, Rushine De Reuck, Steven Mukwala, Yusuf Kagoma, Morice Abraham, Naby Camara na nahodha Shomaru Kapombe, wanaonekana kuingia katika kundi la wachezaji wenye nguvu na uwezo wa kuipambania timu nyakati ngumu za kusaka matokeo mazuri. Hatua hiyo inaweza kuwafanya kupata muda mwingi wa kucheza lakini wakilegeza tu, itakula kwao.
Kwa upande wa nidhamu, nyota wengi kikosini hapo wanaweza kumridhisha Barker akiwemo Naby Camara na Kapombe.
Ikumbukwe kuwa, Barker ametangazwa na Simba Desemba 19, 2025 kuwa kocha mkuu wa kikosi hicho akichukua nafasi ya Dimitar Pantev aliyeondoka Desemba 2, 2025 kwa makubaliano ya pande mbili.
Ikumbukwe, Barker anajiunga na Simba akitokea Stellenboch ya Afrika Kusini aliyoiongoza kutinga nusu fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika msimu uliopita na hatua hiyo ilicheza dhidi ya Simba na kutolewa kwa jumla ya bao 1-0.
Wakati huohuo, imeelezwa uamuzi wa Simba kumbakisha Matola, ulifanywa na Barker kwani ndiye aliyependekeza kufanya naye kazi katika benchi la ufundi analokuja kuliunda, huku akitaja sababu ya kufanya hivyo.
Chanzo cha kuaminika kutoka ndani ya Simba, kililiambia Mwanaspoti, Matola ataendelea kufanya kazi na kocha huyo kama msaidizi wake namba mbili baada ya Barker kusisitiza anamhitaji licha ya kwamba atakuja na wasaidizi wake wengine.
Mtoa taarifa huyo aliendelea kueleza kuwa, urafiki wa Barker na Matola wa siku nyingi uliounganishwa na Fadlu Davids, ndiyo sababu ya kocha huyo Msauzi kupendekeza kufanya naye kazi akiamini uzoefu wake wa kukaa na wachezaji muda mrefu utamsaidia kurahisisha kazi yake ya kuijenga Simba imara.
“Ni kweli Matola ataendelea kuwa sehemu ya benchi la ufundi, hii ni baada ya mapendekezo ya Barker kuomba kuendelea kufanya naye kazi na inaelezwa wawili hao walikuwa wanawasiliana kabla,” kilisema chanzo hicho na kuongeza;
“Atakuwa kocha msaidizi namba mbili kwani tayari Barker anamsaidizi wake ambaye atakuja naye siku chache zijazo tayari kwa ajili ya kuungana na timu, hivyo hakuna mpango wa kuachana na Matola kama ilivyokuwa inaripotiwa endapo kocha atakuja na benchi la ufundi, atawapisha.”
Chanzo hicho kilisema msaidizi Barker, Matola na kocha msaidizi namba mbili anayekuja, wanafahamiana na walikuwa wakiwasiliana kabla hata ya mpango wa makocha hao kutajwa kutua Simba.
Inaelezwa, kiunganishi wa hayo yote ni aliyekuwa kocha wa Simba, Fadlu Davids ambaye hivi sasa anainoa Raja Athletic ya Morocco.
Baada ya Barker kubariki Matola kubaki kuendelea kuwa katika benchi la ufundi la Simba kama kocha msaidizi namba mbili, mzawa huyo ataendelea kuandika rekodi ya kufanya kazi na makocha wengi zaidi tangu mwaka 2019 alipotua Msimbazi akitokea Polisi Tanzania.
Katika miaka sita ya Matola akiwa kocha msaidizi Simba, amefanya kazi na chini ya makocha 10 tofauti, wakiwamo tisa wa kigeni na mmoja mzawa, timu ikitwaa mataji mawili ya Ligi Kuu Bara, Kombe la Muungano na Kombe la FA na kufika fainali ya michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika iliyopoteza kwa RS Berkane ya Morocco kwa jumla ya mabao 3-1.
Simba inatarajiwa kurejea tena uwanjani mapema mwakani kwa mechi mbili mfululizo za Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Esperance iliyopo nafasi ya tatu kundini na pointi mbili na malengo ya klabu ni kutaka kocha mkuu mpya atue mapema aiandae timu sambamba kusajili dirisha dogo.
