Video za kesi ya Lissu zilizokataliwa zamwamsha DPP

Dar es Salaam. Unamkumbuka shahidi muhimu katika kesi ya uhaini kati ya Jamhuri na Tundu Lissu, mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambaye video alizotaka kuzitoa kama kielelezo zilikataliwa na mahakama?

Kufuatia tukio hillo, Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP), Sylvester Mwakitalu amefanya jambo la kisheria ambalo litaruhusu ushahidi atakaoutoa shahidi huyo siku zijazo katika maeneo manne ya utaalamu kwenye kesi za jinai, uweze kupokewa na mahakama, pamoja na vielelezo.

Inspekta Samwel Kaaya mwenye namba PF.24595, alikuwa shahidi wa tatu wa Jamhuri katika kesi ya Lissu, alitaka kutoa kama kielelezo vifaa vya kutunza kumbukumbu ambavyo ni flash disk na memory card zenye video inayomuonyesha Lissu akitamka maneno yanayodaiwa kuwa ya uhaini.

Mahakama ilikataa kupokea vielelezo hivyo kwa kuwa shahidi huyo siyo mtaalamu wa picha mjongeo (video), hivyo hakuwa na sifa za kuvitoa kwa kuwa hata DPP hakuwa amemtangaza katika Gazeti la Serikali (GN) kama mtaalamu wa video.

Uamuzi huo unaonekana kumshtua DPP na sasa ameamua kurekebisha dosari hiyo ya kisheria kwa ajili ya ushahidi wake siku zijazo katika kesi za jinai, kwa kumtangaza Kaaya katika Gazeti la Serikali namba 655 ya Novemba 7, 2025 kuwa miongoni mwa maofisa 29 wenye sifa za kutoa ushahidi huo.

“Mtu ambaye jina lake limeainishwa katika jedwali anateuliwa kuwa mtaalamu wa picha za video (Videographic Expert) kwa madhumuni ya kutayarisha ripoti itakayotumika kama ushahidi wa kesi yoyote ya jinai au masuala yanayohusiana na hayo,” inasema sehemu ya tangazo hilo la Serikali.

Kwa mujibu wa GN hiyo iliyotolewa na DPP, Sylvester Mwakitalu na kuwekwa katika tovuti ya mahakama (TanzLII), uteuzi huo ni wa kipindi cha miaka mitano.

TanzLII ni tovuti ya Serikali ya Tanzania inayochapisha uamuzi, sheria na kanuni mtandaoni na inaruhusu ufikiaji bure wa uamuzi, sheria na kanuni za Tanzania na ni mwanachama wa Jumuiya ya Afrika ya LIIs.

DPP pia ametoa GN namba 652 ya tarehe hiyohiyo, akimteua Inspekta Samwel Kaaya kuwa mtaalamu wa picha (photographic Expert) sambamba na maofisa wengine 29 ambao watakuwa na sifa za kutoa vielelezo vinavyohusu picha.

Hakuishia hapo, DPP amemtangaza Inspekta Kaaya katika GN namba 654 iliyochapishwa Novemba 7, 2025 kuwa mtaalamu wa kutambua sauti (voice recognition expert) sambamba na maofisa wengine 29 wenye sifa hizo kisheria.

Inspekta Kaaya ametangazwa pia kupitia GN namba 653 kama mtaalamu mtambuzi wa sura (facial recognition experts) na kuhudumu kwa muda wa miaka mitano.

Vilevile, DPP ametangaza GN namba 650 ya maofisa wa Polisi 36 kuwa wataalamu wa uchunguzi wa makosa ya kimtandao (Cyber Forensic Experts), GN namba 649 ya wataalamu 31 wa nyaraka na GN 651 ya mtaalamu wa milipuko (Ballistic Expert) yenye maofisa 13.

Ushahidi wa Inspekta Kaaya

Shahidi huyo wakati akitoa ushahidi wake, alijitambulisha kama mtaalamu wa picha, kutoka kitengo cha Picha Kamisheni ya Uchunguzi wa Sayansi Jinai Makao Makuu ya Jeshi la Polisi Dar es Salaam.

Katika ushahidi huo, alieleza Aprili 8, 2025 alipokea flash disk na memory card zenye video ya Lissu, yenye maudhui yanayodaiwa kuwa ya uhaini, kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu Dar es Salaam ili achunguze uhalisia wake.

Shahidi huyo alieleza katika uchunguzi alibaini video hiyo ni halisi na haina pandikizi. Ijumaa Oktoba 17, 2025 aliiomba mahakama ivipokee vifaa hivyo vya kuhifadhi kumbukumbu viwe kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka.

Video hiyo alisema inamuonyesha Lissu akitoa hotuba inayodaiwa kuwa na maudhui (maneno) ya uhaini, katika mkutano na waliokuwa watiania kugombea nafasi mbalimbali katika Uchaguzi Mkuu wa Rais, wabunge na madiwani 2025.

Lissu alivyopinga vielelezo

Alipotaka kuwasilisha vielelezo hivyo, Lissu aliweka pingamizi la kupokewa kwake, akitoa sababu nne, miongoni mwa hizo ni kuwa shahidi hana ustahili wa kisheria wa kuwasilisha vihifadhi data hivyo vyenye picha jongefu (video) zinazojenga msingi wa kesi.

Alieleza shahidi huyo si mtaalamu aliyeteuliwa na mamlaka husika na kutangazwa katika Gazeti la Serikali (GN) kama kifungu cha 216(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Mashauri ya Jinai (CPA), urekebu wa mwaka 2023 inavyotaka.

Alibainisha kuwa, kwa mujibu wa kifungu hicho, mtaalamu wa aina hiyo huteuliwa na DPP na kutangazwa katika GN ili kuwa na sifa za kisheria kuwa mtaalamu.

Lissu alidai shahidi huyo ameteuliwa kuwa mtaalamu wa picha za mnato na si mtaalamu wa picha jongefu na kwamba, kwa kuwa vielelezo anavyokusudia kuviwasilisha vina picha jongefu, basi shahidi huyo hana mamlaka ya kuviwasilisha.

Jamhuri kupitia kwa Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, ilipinga hoja hiyo ikieleza shahidi huyo alieleza kuwa alitangazwa mtaalamu wa picha za mnato na jongefu katika GN namba 516 ya 2022 na DPP, Sylvester Mwakitalu kutoa taarifa.

Oktoba 22, 2025 jopo la majaji wanaosikiliza kesi hiyo likiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Iringa, Dunstan Ndunguru, akishirikiana na majaji James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde, walikubaliana na hoja ya Lissu.

Katika uamuzi uliosomwa na Jaji Ndunguru, mahakama ilikubaliana na hoja ya Lissu na kueleza imefuatilia na kuchunguza kwa umakini hoja za pande zote, imejiridhisha kuwa shahidi huyo hana mamlaka ya kuwasilisha vielelezo vya aina hiyo (video).

Jaji Ndunguru alisema shahidi huyo ni miongoni mwa wataalamu walioteuliwa na DPP kuwa mtaalamu wa picha na kutangaza kwenye G745/2022 Desemba 16, 2022.

Alisema katika aya ya pili ya Gazeti hilo, walioteuliwa ni wataalamu wa uchunguzi wa picha kwa madhumuni ya kutoa taarifa kama ushahidi kwenye kesi ya jinai.

Jaji Ndunguru amesema kifungu cha 216(1) cha CPA, kinachompa mamlaka DPP kuteua na kutanga za wataalamu hao, kinazungumzia shahidi kuandaa picha zinazozalishwa kutoka kwenye filimu.

Hivyo, amesema GN Namba 745 iliyomtangaza shahidi wa tatu kifungu cha 216(1) kinazungumzia mtaalamu wa picha za mnato.

Hata hivyo, Jaji Ndunguru alisema shahidi alichoomba kuwasilisha mahakamani ni vibebeo vya picha mjongeo vyenye picha mjongeo katika mfumo wa kidijitali.

Jaji Ndunguru kwa niaba ya jopo, alisema ingawa upande wa mashtaka ulijitahidi kuishawishi mahakama kuwa picha zinazozungumzia hapo ni pamoja na za mnato na video, lakini mahakama haikukubaliani na hoja hiyo.

Alisema kifungu cha 216(1) hakijazungumzia video na kwamba, vitu hivyo viwili (picha mnato na video) vina sifa tofauti na kwamba, mahakama imeona hiyo video si picha ambazo zimetokana na filimu.

Hivyo, akasema mahakama imeona kuwa shahidi huyo asingeweza kuwasilisha vitu hivyo. kwanza kwa mujibu wa uteuzi wake na pili, hivyo vifungashio na vilivyomo.

Jaji alisema mahakama inaona kwamba, mtaalamu wa picha mjongeo ndiye angeweza kutoa vielelezo hivyo na siyo mtaalamu wa picha mnato.

Katika kesi hiyo namba 19605 ya mwaka 2025, Lissu anakabiliwa na shtaka la uhaini akidaiwa kutoa maneno ya kuitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinyume cha kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu,

Anadaiwa kuwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania mwenye utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa maneno ya kuitishia Serikali na kuonyesha nia hiyo kwa kuchapisha meneno hayo katika mitandao ya kijamii.