Dar/Unguja. Wakati waamini wa dini ya Kikristo nchini kesho wakiungana na wenzao duniani kote kusherehekea Sikukuu ya Krismasi, baadhi ya viongozi wa dini hiyo wamewataka kuitumia kwa kusameheana, kuwaunganisha na kujenga umoja wa kitaifa.
Wakizungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti leo Jumatano Desemba 24, 2025, viongozi hao wamesema licha ya changamoto na misukosuko iliyolikumba Taifa mwaka huu, Krismasi inapaswa kuwa kipindi cha tafakuri, toba, upendo na mshikamano, badala ya chuki na migawanyiko.
Mchungaji Titus Kiame, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Kamati ya Umoja wa Makanisa Dar es Salaam (KUMD). Picha na Maktaba.
Mchungaji Titus Kiame, ambaye pia ni Naibu Katibu Mkuu wa Kamati ya Umoja wa Makanisa Dar es Salaam (KUMD) inayojumuisha Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Umoja wa Madhehebu ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) pamoja na Jumuiya ya Kikristo Tanzania (CCT), amesema waamini wa Kikristo na Watanzania wote wenye mapenzi mema wanapaswa kuitumia Sikukuu ya Krismasi kama fursa ya kuimarisha mshikamano wa kifamilia.
Amesema maadhimisho ya sikukuu hiyo yanapaswa kuambatana na kuheshimu na kuzingatia mafundisho ya dini, sambamba na kudumisha mila na tamaduni za Kitanzania zinazolinda na kukuza tunu za Taifa, hususan katika misingi ya maadili, amani, mshikamano na upendo kwa jamii.
“Ukisoma Injili ya Mathayo sura ya kwanza, utaona ukoo wa Yesu umetajwa kwa kina. Ujumbe wangu kwa Krismasi hii ni kwamba Watanzania waheshimu koo zao, kwa sababu kila ukoo una mafundisho yake. Ukoo unapokua, huzaa kijiji, kijiji kinazaa wilaya, kisha mkoa na hatimaye Taifa,” amesema Mchungaji Kiame.
Amefafanua kuwa endapo Watanzania watajenga tabia njema ndani ya koo, Taifa nalo litakuwa na misingi imara ya maadili. Ameongeza kuwa mafundisho yanayotolewa na koo yanapaswa kuwa nguzo ya malezi ya vijana, ambao wanapaswa kuyaishi na kutambua nafasi yao katika kuitangaza vyema Tanzania ndani na nje ya nchi.
Akizungumzia maana ya Krismasi, amesema ni sikukuu ya kuenzi kuzaliwa kwa Yesu Kristo, ambaye ni mtakatifu, hivyo waamini wanapaswa kuuenzi utakatifu huo kwa matendo yao. Amesema licha ya machafuko na changamoto zilizotokea Oktoba 29, mwaka huu, Watanzania wanapaswa kuamini kuwa Mungu yupo pamoja nao na kila mmoja amrudie kwa imani yake.
“Tunapouanza mwaka 2026, tuuanze tukiwa tumesameheana na kushikamana kama Taifa moja. Katika Sala ya Bwana, tunaelekezwa kuwa wazalishaji wa uchumi wetu wa kila siku pale inaposema ‘utupe leo riziki yetu ya kila siku’, lakini pia tunafundishwa unyenyekevu na kusameheana tunapokoseana,” amesema.
Aidha, Mchungaji Kiame ameutaja mwaka 2025 Taifa limepitia mengi, ikiwamo makosa yaliyofanywa mbele za Mungu kama vurugu, uharibifu wa mali na mauaji, akitoa wito kwa kila Mtanzania kumrudia Mungu kwa toba na msamaha.
“Mwaka huu tumepitia mengi na tumemkosea Mungu. Kwa sikukuu hii ya kuzaliwa kwa Yesu Mwokozi wetu, tuombe msamaha na nasi tusameheane, ili tuingie mwaka 2026 tukiwa wasafi na kuepuka madhara ya damu iliyomwagika,” amesema.
Askofu William Mwamalanga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Pamoja ya Amani na Maadili ya Mashehe na Maaskofu. Picha na Maktaba
Kwa upande wake, Askofu William Mwamalanga ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Pamoja ya Amani na Maadili ya Mashehe na Maaskofu, amesema Krismasi hii inapaswa kutumiwa kujenga upya misingi ya amani na umoja wa kitaifa kwa kuachana na tofauti na migogoro iliyojitokeza mwaka huu 2025 unao elekea ukingoni.
“Jamii yetu inasherehekea sikukuu hii ikiwa imeghadhabika kutokana na misukosuko na matatizo mengi waliyopita mwaka huu. Krismasi itumike kama chanzo cha uponyaji. Hii si sikukuu ya Wakristo pekee, bali ni ya watu wote,” amesema Askofu Mwamalanga.
Amesema maana halisi ya Krismasi ni kuenzi kuzaliwa kwa Yesu Kristo, mkombozi wa ulimwengu, hivyo Watanzania wanapaswa kuitumia sikukuu hiyo kupata ukombozi wa kweli kwa kumrudia Mungu na kuondoa chuki, maumivu na visasi mioyoni.
“Kupitia sikukuu hii, hata wale waliokuwa wakitenda uovu waachane nao kwa kutubu na kusameheana. Mwaka huu uwe mwisho wa uovu na tunapoingia 2026 Taifa lirudi kwenye misingi yake ya amani, haki na maadili,” amesema.
Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Jackson Sosthenes. Picha na Maktaba
Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es Salaam, Jackson Sosthenes amewataka Watanzania kuadhimisha Krismasi kwa utulivu na amani, wakienzi tunu za haki, huruma na kusaidia wenye uhitaji.
“Tumshukuru Mungu kwa kutufikisha sikukuu hii, tuiadhimishe kwa kukumbuka uokovu na kuishi maisha yanayomtukuza Mungu. Krismasi iadhimishwe kwa amani na utulivu,” amesema.
Ameongeza kuwa mshikamano wa Taifa utajengwa pale kila mmoja atakapotekeleza wajibu wake kwa haki na kuwasaidia wenye mahitaji huku akisisitiza kuwa kufanya hivyo ni sehemu ya kumtukuza Mungu.
Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT), Dk Dickson Chilongani. Picha na Maktaba
Naye Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Central Tanganyika (DCT), Dk Dickson Chilongani amesema ujumbe mkuu wa Krismasi kwa Watanzania ni amani, hasa ikizingatiwa kuwa sikukuu hiyo inakuja wakati ambao watu wengi wana hofu na kutoaminiana.
“Watu wanalaumiana, viongozi hawaaminiani, raia na vyombo vya ulinzi hawana imani. Lakini Yesu anayezaliwa ni mfalme wa amani,” amesema.
Amefafanua kuwa Wakristo wanaelekezwa na maandiko matakatifu kutafuta amani kwa bidii, akitolea mfano Waebrania 12:14, unaosisitiza umuhimu wa kuishi kwa amani na watu wote.
“Tunapaswa kuwaza amani, kuomba amani na kuzungumza amani. Tukiomba na kuishi kwa amani, nchi yetu itakuwa ya amani,” amesema askofu huyo.
Kwa upande wake, Askofu Mkuu wa Kanisa la Zanzibar International Christian Center (ZICC), Dickson Kaganga amesema kusherehekea Krismasi si kufanya anasa, bali ni kutumia siku hiyo kutafakari ukuu wa Mungu na kuwasaidia wenye mahitaji.
“Tunaposherehekea sikukuu hii, tukumbuke muktadha wake. Tuhudhurie ibada, kisha tusherehekee kwa kiasi na kwa pamoja, hasa kwa kuwakumbuka wenye uhitaji,” amesema wakati Askofu Kaganga.
Amesema Krismasi ya mwaka huu iwe mwanzo mpya wa uponyaji wa Taifa, mshikamano wa kijamii na kujengwa upya kwa misingi ya haki, amani, maadili na utu wa Watanzania.
Imeandikwa na Pawa Lufunga, Bakari Kiango na Jesse Mikofu.

