Dodoma. Wakulima nchini wamehimizwa kuacha matumizi ya viuatilifu vyenye sumu kali na badala yake kuzingatia kilimo salama kisichohatarisha afya za walaji, ili kulinda mazingira na kuongeza fursa za kupata masoko ya ndani na ya kikanda.
Akizungumza leo, Desemba 24, 2025, jijini Dodoma, Mtafiti kutoka Mamlaka ya Viuatilifu na Afya ya Mimea Tanzania (TPHPA), Dk Jones Kapeleka, amesema hayo wakati wa kongamano lililoandaliwa na Shirikisho la Vyama vya Wakulima Wadogo Tanzania (Shiwakuta).
Kongamano hilo lililenga kuwawezesha wakulima, wafugaji na wavuvi kupata uelewa mpana na fursa za kuyafikia masoko ya ndani na kikanda kupitia uzalishaji wa mazao ya kilimo ikolojia.
Dk. Kapeleka amesema tafiti zilizofanywa na TPHPA zinaonesha kuwa wakulima wengi hutumia viuatilifu bila kuzingatia maelekezo ya kitaalamu, hali inayohatarisha afya zao, walaji wa mazao wanayozalisha, pamoja na kuharibu ubora na rutuba ya udongo.
“Unakuta mkulima kachanganya viuatilifu takribani aina sita tofauti bila kuchukua tahadhari na ukiangalia vyote vina kazi moja isipokuwa majina tofauti lakini kazi ni moja ya kuua wadudu kwenye mazao,” amesema Dk Kapeleka
Mtaalamu hiyo amesema viuatilifu vinavyotumika ni sumu hivyo vinatakiwa kutumiwa kwa maelekezo maalumu, ingawa wakulima wengi hawafanyi hivyo jambo linalosababisha madhara ya kiafya ambapo wanawake huathirika zaidi kuliko wanaume.
Mtafiti huyo amesema mazao ambayo yamewekwa viuatilifu yana madhara takribani kwa asilimia 70 wakati yasiyowekwa hatari yake ni asilimia 30 pekee.
Kwa upande wake mtafiti wa mbegu za asili, Ayesiga Buberwa amesema wameshaanza kuzifanyia utafiti mbegu za asili kwa mazao ya mikunde na mazao mengine ili kuzisambaza kwa wakulima kwani zinastahimili magonjwa na rahisi kupatikana.
Buberwa amesema mbegu za asili ni salama na hazihitaji viuatilifu kwa ajili kuua wadudu tena zinastahimili ukame na magonjwa hivyo kumpatia mkulima mavuno ya uhakika.
Amesema wameshafanyia utafiti mbegu za asili kutoka Mkoa wa Manyara ambazo zimesambazwa kwa wakulima na zinafanya vizuri kwa kutoa mavuno mengi.
Naye Ofisa ushawishi na utetezi kutoka Shiwakuta, Thomas Laiser amesema lengo la kongamano hilo ni kuwawezesha wakulima kuzalisha mazao yenye uhakika sokoni.
Laiser amesema mpango huo unalenga wakulima wazalishe kibiashara bila kutumia sumu wala kuharibu mazingira.
Amesema kuna wakati hata asali inayozalishwa kutokana na maua yenye viuatilifu ikipimwa inakutwa na sumu, hivyo kushusha soko la asali inayotoka nje ya mipaka ya nchi.